STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 30, 2013

Rais Kikwete akabidhiwa Rasimu ya Katibu Mpya

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete leo amepokea rasmi Rasimu ya Katiba Mpya ambayo itajadiliwa hapo baade na Bunge maalum la Katiba. 
Rais Kiwete aliipokea Rasimu hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba katika makabidhiano yaliyofanyika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam. Kuisoma zaidi rasimu hiyo Bofya hapa RASIMU YA KATIBA

Miyeyusho abadilishiwa mpinzani toka Kenya

Bondia Joshua Amukulu (kushoto) kutoka Kenya akitunishiana misuli na Francis Miyeyusho wakati wa upimaji uzito kwa ajili ya mpambano wao utakaofanyika kesho Desemba 31. Awali ilitangazwa Miyeyusho angepigana na David Chalanga.

Bondia Kalama Nyilawila kushoto akitunishiana misuli na Ibrahimu Maokola  baada ya kupima uzito kwa ajili ya mpambano wao utakaofanyika Desemba 31 siku ya jumanne katika ukumbi wa New Msasani Club.
Bondia Francis Miyeyusho akipima uzito kwa ajili ya mpambano wake  Joshua Amukulu kutoka Kenya utakaofanyika kesho jumanne katika ukumbi wa Msasani Club.
BONDIA FRANSIC MIYEYUSHO AKIHOJIWA NA WAANDISHI WA HABARI BAADA YA KUPIMA UZITO KWA AJILI YA MPAMBANO WAKE NA MKENYA JOSHUA AMUKULU UTAKAOFANYIKA DESEMBA 31 KATIKA UKUMBI WA MSASANI CLBU (PICHA ZOTE NA SUPER D)
Bondia Ibrahimu Class 'king Class Mawe'  kushoto akitunishiana misuli na Mustafa Dotto  baada ya kupima uzito kwa ajili ya mpambano wao utakaofanyika kesho jumanne katika ukumbi wa Msasani Club.
IBRAHIMU CLASS 'KING CLASS MAWE AKIPIMWA AFYA
 IDDY MNYEKE AKIPIMWA AFYA

TBF yapata viongozi wapya, Maluwe, Phares chali Dodoma

Michael Maluwe (kushoto) na Magessa waliangushwa jana Dodoma
SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) limefanikiwa kupata safu mpya ya uongozi baada ya John Bandie kuchaguliwa kuwa Rais Mpya wa shirikisho hilo.
Uchaguzi huo ulifanyika jana mjini Dodoma na kutangazwa na Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Jamal Rwambow.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Dodoma na kuthibitishwa na mmoja wa makocha maarufu wa mchezo huo aliyechaguliwa kuwa Kamishna wa Ufundi na Mashindano Manase Zablon kupitia akaunti yake ya facebook, Rais huyo mpya alipata ushindi huo akimgaragara Phares Magessa.
Magessa alikuwa Makamu wa Rais katika uongozi uliomaliza muda wake ambaye alijikuta akipata kura 19 dhidi ya kura 24 za mpinzani wake aliyeibuka mshindi.
Katika nafasi ya Makamu wa Rais ilienda kwa Hamis Jafar aliyepata kura 39 za Ndiyo huku nne zikimkataa kwani alikuwa mwenyewe katika nafasi hiyo.
Kiongozi maarufu wa zamani wa mchezo huo, Saleh Zonga aliibuka kidedea kwenye nafasi ya Katibu Mkuu, akimshinda aliyekuwa Katibu Mkuu Msaidizi, Michael Maluwe kwa kupata kura 24 dhidi ya 13 za mpinzani wake.
Amina Ahmed alifanikiwa kuchaguliwa kuwa Mhazini wa shirikisho hilo kwa kupigiwa kura za ndito 43, huku Manase Zablon akichaguliwa kuwa Kamishna wa Ufundi na Mashindano kwa kupata kura 37 za ndiyo na mbili kumkataa.
Wengine walishinda katika uchaguzi huo ambao awali ulipangwa kufanyika Desemba 10 mjini Mbeya na kukwama kabla ya kuhamishiwa Dodoma ni Michael Mwita aliyechaguliwa Kamishna wa Mipango kwa kura 39, huku Kamishna wa Watoto na Shule ikienda kwa Patrick Matete, Angela Bondo akichaguliwa Kamishna ya Wanawake na upande wa Walemavu nafasi ilienda kwa Aziz Mtogole.

Swagger sasa aja na Bongo Series Extra

Swagger katika pozi
MTAYARISHAJI wa filamu aliyewahi kutamba kwenye muziki wa kizazi kipya akiwa na kundi la Crime Busters, Hussein Ramadhani 'Swagger' anatarajiwa kuibuka na kipindi kipya cha burudani cha kwenye runinga kiitwacho 'Bongo Series Extra'.
Akizungumza na MICHARAZO, Swagger alisema kipindi hicho kitakachokuwa kikionyesha tukio kali la wiki, onyesho 'live' la burudani jukwaani, mahojiano ya msanii mkali wa wiki pamoja na kuangalia watoto wa mitaani waishivyo na pamojana mapitio ya filamu, kimeshakamilika ingawa bado hajajua kitarushwa kwenye kituo gani.
"Kila kitu kimekamilika na tayari nipo kwenye mazungumzo na baadhi ya vituo vya televisheni kwa ajili ya kuruhusu kurushwa hewani, hivyo wapenzi wa burudani wakae mkao wa kula kupata burudani ya aina yake kwani Bongo Series Extra imeshiba vya kutosha," alisema.
Swagger aliyeanza kuigiza michezo ya kwenye runinga kupitia kundi la Niger Theare akiwa na mmoja wa waasisi wa michezo ya kwenye televisheni kupitia kituo cha DTV, Qudrat Olomoda 'Chombeza', alisema aliamua kuja na kipindi hicho chenye mambo mseto ili kuwakamata mashabiki ambao walikuwa wanakosa kipindi cha namna hiyo.
Alisema ukiondoa masuala ya muziki na filamu pia kipindi hicho kitakuwa kinamulika maisha halisi ya watoto wa mitaani ili kusaidia kuizundua jamii na serikali kwa ujumla kujua tatizo hilo namna lilivyo na kuangalia jinsi ya kuwasaidia.
"Hakuna asiyejua tatizo la watoto wa mitaani au wanaoishi katika mazingira magumu, lakini nani anayejua ugumu wanaokutana nao mitaani, watasaidiwaje ili kuwafanya wafurahie maisha kama watoto wengine. Hivyo tumeona tuje namna hiyo," alisema Swagger.
Swagger ambaye kwa sasa yupo mbioni kukamilisha filamu yake mpya iitwayo 'Nyaraka' iliyowashirikisha wasanii mbalimbali wakiwemo Mzee Magari na wengine alisema anatarajia maombi yake ya kurusha kipindi hicho yakikamilika na kukubaliwa mashabiki wa burudani na jamii nzima itaburudika vya kutosha.

Kocha Logarusic 'afagiliwa' Simba

Ibrahim Twaha, katika mazoezi ya siku za nyuma
Kocha Logarusic aliyefagiliwa
KIUNGO Mshambiliaji wa klabu ya Simba, Ibrahim Twaha 'Neymar', amemwagia sifa kocha mpya wa klabu hiyo, Zdravko Logarusic 'Loga' kwamba ni bonge na kocha na kuwa na imani ya kuipa Simba ubingwa katika Ligi Kuu msimu huu.
Aidha mchezaji huyo amesema anashukuru ameanza mazoezi mepesi baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu, japo anajisikia vibaya kuikosa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza rasmi kesho visiwani Zanzibar.
Akizungumza na MICHARAZO, Twaha aliyesajiliwa na Simba kutoka Coastal Union akifahamika kwa jina la utani kama 'Messi' na kubadilishiwa jina kuwa 'Neymar', alisema japo hajaanza kufundishwa na kocha huyo lakini amekuwa akihudhuria mazoezi ya timu hiyo na kuvutiwa na ufundishaji wa Logarusic.
Twaha alisema Mcroatia huyo ni bonge la kocha na hataki mchezo na anayependa timu kucheza kwa kasi kitu ambacho kwa wachezaji waliopo Simba akiwemo yeye wataimudu na kuiletea klabu yao mafanikio.
"Siyo siri kocha wetu mpya ni kocha mzuri, anataka timu icheze kwa kasi na wachezaji kujituma na kujitambua bila kusubiri kusukwa kitu ambacho ni kizuri na nina imani ataisaidia Simba kutwaa ubingwa msimu huu," alisema Twaha.
Twaha, alisema kitu cha muhimu kwa wachezaji wenzake kuzingatia maelekezo ya mwalimu huyo aliyedai ni mmoja wa makocha wasiotaka masihara kazini kitu ambacho anaamini kitajenga nidhamu nzuri kwa timu yao.
Mchezaji huyo aliyekuwa majeruhi wakati duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara likielekea ukingoni, alisema anashukuru hali yake imeanza kutengemaa kwa kufanya mazoezi mepesi akisubiri ripoti kamili ya daktari wa timu yao ili kama aanze kujumuika na wenzake.
"Nashukuru nimeanza kufanya mazoezi mepesi, na leo jioni natarajia kuonana na daktari kunikagua, ila najisikia vibaya kuyakosa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, lakini kama hali itaimarika zaidi naamini nitaanza mechi za duru la pili la ligi kuu mwakani," alisema Twaha.
Simba ilimnyakua Logarusic aliyewahi kuinoa Gor Mahia-Kenya baada ya kumtimua Abdallah Kibadeni mara baada ya kumalizika kwa duru la kwanza.

Oscar Joshua 'aigwaya' Al Ahly Ligi ya Mabingwa Afrika

Oscar Joshua
BEKI kisiki wa timu ya Yanga, Oscar Joshua ameibuka na kuitahadharisha klabu yake kwa kuitaka kuwa makini na kujiandaa vyema kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili ising'olewe mapema kwenye michuano hiyo.
Joshua, beki wa pembeni alisema mechi ambayo Yanga inapaswa kuwa makini nayo ni ile dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri watakaocheza nao iwapo watafanikiwa kuing'oa Komorozine ya Comoro.
Joshua alisema Al Ahly ndiyo timu pekee inayoonekana kuwa kikwazo kwa Yanga na kama itajipanga na kuitoa itajifungulia njia ya kufanya vyema kwenye michuano hiyo itakayoishiriki mwakani.
Akizungumza na MICHARAZO, Joshua alisema Al Ahly ni hatari sana kwa Yanga, lazima klabu yao ijiandae na kujipanga vyema.
"Al Ahly ni hatari sana wale, ni muhimu kwetu kujipanga vyema ili kuweza kuwatoa. Hii ndiyo timu tishio kwa Yanga michuano ya mwakani," alisema.
Beki huyo anayemudu nafasi nyingi uwanjani mbali na kucheza kama beki wa kushoto alisema, kwa kikosi kilichopo Yanga ikijipanga inaweza kufanya maajabu.
Yanga inatarajiwa kuvaana na Al Ahly katika mechi ya raundi ya kwanza mapema mwezi Machi, na hii ni iwapo tu watafanikiwa kuindosha mashindanoni Komorozine ya Comoro wanaotarajiwa kuanza nao kwenye hatua ya awali kati ya Februari 7-9 na kuridiana nao wiki mbili baadaye.
Rekodi pekee ya Yanga ya kujivunia kwenye michuano hiyo ya Afrika ni kucheza hatua ya makundi mwaka 1998 na kucheza Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili mfululizo 1969 na 1970.

Miyeyusho, Mkenya kumaliza ubishi kesho Msasani


BINGWA wa Ngumi za Kulipwa wa Kimataifa anayetambuliwa na UBO, Francis Miyeyusho na Mkenya David Chalanga wanatarajiwa kupima uzito na afya zao asubuhi hii kabla ya kesho kupanda ulingoni kupigana jijini Dar es Salaam.
Mabondia hao watapigana kesho kwenye ukumbi wa New Msasani Club katika pambano lisilo la ubingwa la kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 ambalo litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Kwa mujibu wa Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited), Yasin Abdallah 'Ustaadh' mabondi wote watakaopanda kesho ulingoni watapimwa uzito wao leo kuanzia saa 3 asubuhi.
Ustaadh alisema zoezi hilo la upimaji wa afya na uzito litafanyika kwenye ukumbi huo wa New Msasani na kuwasisitizia mabondia hao kuwahi mapema.
Mkenya David Chalanga aliwasili nchini juzi usiku akitokea kwao Kenya tayari kwa ajili ya pambano hilo la uzani wa Bantam.
"Bondia David Chalanga ameshatua nchini kwa ajili ya kupigana na Miyeyusho na Jumatatu (leo) watapima uzito na afya zao kabla ya kupanda ulingoni Desemba 31," alisema Ustaadh.
Ustaadh alisema wengine watakaopima uzito na afya zao leo kabla ya kusindikiza pambano la Miyeyusho ni Kalama Nyilawila atakayecheza na  Ibrahimu Maokola,  Ibrahimu Class 'King Class Mawe' atakayevaana na Mohamed Kashinde.
Mabondia wengine watakaopigana hiyo kesho ni Cosmas Cheka dhidi ya Idd Mnyeke, Anthony Mathias atakayepimana ubavu na Fadhili Majiha na Nyota wa muziki wa Hiphop, Karama Masoud 'Kalapina' ataonyeshana kazi na Kimbunga Noma .
Kocha wa Ibrahim Class, Rajab Mhamila 'Super D' aliiambia NIPASHE bondia wake yupo tayari kumtoa nishai mpinzani wake kwa jinsi alivyomuandaa.
Super D, alisema anaamini bondia wake atamshinda Kashinde mapema ili kuendeleza rekodi yake na kuuaga vyema mwaka 2013.