STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 30, 2013

Miyeyusho, Mkenya kumaliza ubishi kesho Msasani


BINGWA wa Ngumi za Kulipwa wa Kimataifa anayetambuliwa na UBO, Francis Miyeyusho na Mkenya David Chalanga wanatarajiwa kupima uzito na afya zao asubuhi hii kabla ya kesho kupanda ulingoni kupigana jijini Dar es Salaam.
Mabondia hao watapigana kesho kwenye ukumbi wa New Msasani Club katika pambano lisilo la ubingwa la kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 ambalo litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Kwa mujibu wa Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited), Yasin Abdallah 'Ustaadh' mabondi wote watakaopanda kesho ulingoni watapimwa uzito wao leo kuanzia saa 3 asubuhi.
Ustaadh alisema zoezi hilo la upimaji wa afya na uzito litafanyika kwenye ukumbi huo wa New Msasani na kuwasisitizia mabondia hao kuwahi mapema.
Mkenya David Chalanga aliwasili nchini juzi usiku akitokea kwao Kenya tayari kwa ajili ya pambano hilo la uzani wa Bantam.
"Bondia David Chalanga ameshatua nchini kwa ajili ya kupigana na Miyeyusho na Jumatatu (leo) watapima uzito na afya zao kabla ya kupanda ulingoni Desemba 31," alisema Ustaadh.
Ustaadh alisema wengine watakaopima uzito na afya zao leo kabla ya kusindikiza pambano la Miyeyusho ni Kalama Nyilawila atakayecheza na  Ibrahimu Maokola,  Ibrahimu Class 'King Class Mawe' atakayevaana na Mohamed Kashinde.
Mabondia wengine watakaopigana hiyo kesho ni Cosmas Cheka dhidi ya Idd Mnyeke, Anthony Mathias atakayepimana ubavu na Fadhili Majiha na Nyota wa muziki wa Hiphop, Karama Masoud 'Kalapina' ataonyeshana kazi na Kimbunga Noma .
Kocha wa Ibrahim Class, Rajab Mhamila 'Super D' aliiambia NIPASHE bondia wake yupo tayari kumtoa nishai mpinzani wake kwa jinsi alivyomuandaa.
Super D, alisema anaamini bondia wake atamshinda Kashinde mapema ili kuendeleza rekodi yake na kuuaga vyema mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment