STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 30, 2013

Kocha Logarusic 'afagiliwa' Simba

Ibrahim Twaha, katika mazoezi ya siku za nyuma
Kocha Logarusic aliyefagiliwa
KIUNGO Mshambiliaji wa klabu ya Simba, Ibrahim Twaha 'Neymar', amemwagia sifa kocha mpya wa klabu hiyo, Zdravko Logarusic 'Loga' kwamba ni bonge na kocha na kuwa na imani ya kuipa Simba ubingwa katika Ligi Kuu msimu huu.
Aidha mchezaji huyo amesema anashukuru ameanza mazoezi mepesi baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu, japo anajisikia vibaya kuikosa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza rasmi kesho visiwani Zanzibar.
Akizungumza na MICHARAZO, Twaha aliyesajiliwa na Simba kutoka Coastal Union akifahamika kwa jina la utani kama 'Messi' na kubadilishiwa jina kuwa 'Neymar', alisema japo hajaanza kufundishwa na kocha huyo lakini amekuwa akihudhuria mazoezi ya timu hiyo na kuvutiwa na ufundishaji wa Logarusic.
Twaha alisema Mcroatia huyo ni bonge la kocha na hataki mchezo na anayependa timu kucheza kwa kasi kitu ambacho kwa wachezaji waliopo Simba akiwemo yeye wataimudu na kuiletea klabu yao mafanikio.
"Siyo siri kocha wetu mpya ni kocha mzuri, anataka timu icheze kwa kasi na wachezaji kujituma na kujitambua bila kusubiri kusukwa kitu ambacho ni kizuri na nina imani ataisaidia Simba kutwaa ubingwa msimu huu," alisema Twaha.
Twaha, alisema kitu cha muhimu kwa wachezaji wenzake kuzingatia maelekezo ya mwalimu huyo aliyedai ni mmoja wa makocha wasiotaka masihara kazini kitu ambacho anaamini kitajenga nidhamu nzuri kwa timu yao.
Mchezaji huyo aliyekuwa majeruhi wakati duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara likielekea ukingoni, alisema anashukuru hali yake imeanza kutengemaa kwa kufanya mazoezi mepesi akisubiri ripoti kamili ya daktari wa timu yao ili kama aanze kujumuika na wenzake.
"Nashukuru nimeanza kufanya mazoezi mepesi, na leo jioni natarajia kuonana na daktari kunikagua, ila najisikia vibaya kuyakosa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, lakini kama hali itaimarika zaidi naamini nitaanza mechi za duru la pili la ligi kuu mwakani," alisema Twaha.
Simba ilimnyakua Logarusic aliyewahi kuinoa Gor Mahia-Kenya baada ya kumtimua Abdallah Kibadeni mara baada ya kumalizika kwa duru la kwanza.

No comments:

Post a Comment