STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, November 25, 2013

Watano wamwaga wino Yanga, Yondani apongezwa


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhNMyVKtqT3WPzKt5HLtbq8FHl6g9BGflumehITr8kvDY9vjdr_1M9tLapAVbNgQxWu6qwyoAPojN0fECt7CByEWUPeieZRpMl6r1ghkJ9IrBOdwR1nTYSsecyuKluImHFy2BgGWm6pKMU/s1600/Kelvin-Yondani-akiwa-katika-mazoezi-yna-timu-yake-mpya-ya-Yanga-baada-ya-kusajiwa-kwa-ajili-ya-msimu-ujao-wa-Ligi-Kuu-2012-131.jpg
Kelvin Yondani mmoja wa waliomwaga wino, akiwa pia ameula Kili Stars kwa kuteuliwa nahodha
WACHEZAJI watano wa timu ya Young Africans wameongeza mikataba ya muda mrefu ambapo sasa wataendelea kuitumikia klabu yenye maskani yake mitaa ya Twiga/Jangwani mpaka mwaka 2016, hili limefanywa na uongozi kwa mapendekezo ya benchi la ufundi.
Wachezaji ambao mpaka sasa wameshaongeza mikataba ya kuitumikia klabu ya Young Africans ni walinzi Kelvin Yondani (2014-2016), Nadir Haroub "Cannavaro" (2014-2016), kiungo Athuman Idd (2014-2016), mshambuliaji Saimon Msuva (2014-2016) na Jerson Tegete (2014-2016). 
Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Young Africans Abdallah Bin Kleb amesema hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao wameshamaliza taratibu zote na kusaini mikataba mipya itakayowafanya waitumikie Yanga mpaka mwaka 2016.
"Tupo katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji wetu wengine, mazungumzo yanaendelea vizuri na tunaamini muda si mrefu nao tutakua tumeshamalizana nao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga tena kwa muda mrefu "alisema Bin Kleb.
Wakati huo huo kikosi cha Young Africans leo kimeanza mazoezi asubuhi katika uwanja wa Bora - Mabatini Kijitonyama kujiandaa na mchezo wa hisani dhidi ya Simba SC Disemba 14, 2013, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Aidha Uongozi wa klabu ya Young Africans unampa pongezi beki wake wa kati Kelvin Patrick Yondani mchezaji bora wa mwaka 2012/2013 kwa kuteuliwa kuwa nahodha mpya wa timu ya Taifa Tanzania bara (Kilimanjaro stars) inayokwenda kushiriki mashindano ya Chalenji jijini Nairobi.
Kelvin Yondani ametambulishwa rasmi leo na kocha mkuu wa timu ya Taifa Kim Poulsen kwa waandishi wa habari  katika hafla ya kuwaaga wachezaji wa timu ya Taifa wanaokwenda nchini Kenya katika hoteli ya Accomondia eneo la gerezani jijini Dar es salaam.
Tunapenda kumpa pongezi kijana wetu, mchezaji wetu Yondani kwa kupewa nafasi hiyo kubwa katika timu ya Taifa, tunamtakia kila la kheri na awe kiongozi bora kwa wachezaji wenzake na kuiwakilisha vizuri nchi yetu na timu yake ya Young Africans.

Young Africans Official Website

Unyama! Mwanamke achomwa kisu na kuuwawa na mumewe wodini, kisa....!

Gervas Kadaga(25) anayetuhumiwa kumuua mkewe akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.

MAMA mkubwa wa Gervas aliyejitambulisha kwa jina la Martha Lugenge alisema kuwa vijana hawa walikutana Madibila kila mmoja akiwa katika shughuli zake ndipo walipoamua kuishi pamoja.


MWANAMKE mkazi wa kijiji cha Mahango kata ya Madibila wilayani Mbarali mkoani Mbeya aliyefahamika kwa jina la Jitihada Mamga(20) ameuawa kwa kuchomwa kisu na mumewe aliyefahamika kwa jina Gervas Kadaga(25) ambaye pia ni mkazi wa kijijini hapo.


Tukio hilo limetokea Novemba 21 majira ya saa 1:00 jioni baada ya kutokea ugomvi baina ya wapenzi hao ambapo marehemu alikutwa na majeraha tisa ya kisu katika sehemu mbalimbali za mwili wake.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Diwani Athumani alisema kuwa marehemu alifia nyumbani kwake ambapo mtuhumiwa ambaye amelazwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya naye amejeruhiwa kwa kuchomwa na kisu tumboni.


Hata hivyo Kamanda Athumani alisema kuwa hadi sasa hakijafahamika chanzo halisi cha ugomvi huo ambapo Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku mtuhumiwa akiwa amewekwa chini ya ulinzi wa polisi katika hospitali ya rufaa ya Mbeya alikolazwa.


Akizungumza katika hospitali ya rufaa alikolazwa mama mkubwa wa Gervas aliyejitambulisha kwa jina la Martha Lugenge alisema kuwa vijana hawa walikutana Madibila kila mmoja akiwa katika shughuli zake ndipo walipoamua kuishi pamoja.


Alisema yeye alipewa taarifa za tukio hilo siku inayofuata na kwamba alipofika alikuta ndugu wa marehemu wameuchukua mwili wa mtoto wao kwa ajili ya taratibu za mazishi na kwamba hajui chanzo cha ugomvi uliosababisha wapigane visu.


Mama huyo alisema kuwa vijana hao hawajawahi kupata mtoto na kwamba hawajaanza kuishi pamoja muda mrefu; 

''Wote ni watoto, kwani wameanza kuishi muda mrefu? wamekutana kila mmoja akiwa katika kazi zake, ndipo walipoanza kuishi kama mke na mume,''alisema.

Mbeya yetu

Wahitimu kidato cha nne waaswa kuepuka dawa za kulevya

Meza Kuu ikifuatilia maonyesho ya wahitimu wa kidato cha nne Mwandege Boys (hawapo pichani)
DC Mercy Sillah akihutubia
DC Mkuranga akiendelea kutoa nasaha zake kwa wahitimu na wazazi na walezi waliohudhuria mahafali ya tano ya Kidato cha nne Shule ya Mwandege Boys.

MKUU wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Sillah, amewaasa wahitimu ya Kidato cha Nne wa mwaka 2013 wasishawishike kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa lengo la kupata utajiri wa haraka.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya, aliwataka wazazi na walezi kusaidia kuwalea watoto wao kwa maadili ya kidini ili kulisaidia taifa kuwa na vijana waadilifu ambao watalisaidia taifa.
Akizungumza kwenye Mahafali ya Tano ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari ya Mwandege Wavulana, DC Mercy, alisema kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wengi kuingia tamaa ya kutajirika na kujihusisha na dawa za kulevya kitu alichodai ni hatari kwa taifa.
Alisema kutokana na hilo wahitimu wa shule hiyo na wengine nchini wanapaswa kuepuka vishawishi na tamaa za njia ya mkato ya maisha na badala yake wajikite katika kujiendeleza kielimu na kudumisha nidhamu walizokuwa nazo shuleni ili wafanikiwe maishani.
"Dawa za Kulevya zimekuwa ni kishawishi kibaya kwa sasa kwa vijana wetu, msijiingize huko mkaharibu maisha yenu, jiendelezeni na tumieni nidhamu mliyojengewa kujitengenezea maisha mazuri, mkikaa bure ni rahisi shetani kuwaingiza majaribuni," alisema.
DC Mercy aliwakumbusha kuwa pia kuzingatia sheria za nchi sambamba na kutambua kuwa kuhitimu kidato cha nne siyo kumaliza kila kitu, kwani wana fursa ya kujiendeleza kwa masomo ya juu ya sekondari au ufundi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kujiajiri.
Mkuu huyo wa wilaya aliwakumbusha wazazi na walezi kuvitambua na kuviendelezxa vipaji vya watoto wao, sambamba na kuwalea kwa malezi bora na mazuri yanayozingatia maadili na mafunzo ya kidini ili kuwajenga kimaadili na uchaji Mungu kwa vijana hao.
Naye Mkuu wa Shule ya Mwandege Wavulana, Mwl Enock Walter, kupitia risala aliyosoma aliomba serikali kuacha kufanya majaribio katika elimu kwa kila anayeingia madarakani kujaribu mambo yake na kuacha mengine aliyoyakuta kwani yanayumbisha elimu nchini.
"Kufanya majaribio katika elimu ni kuliua taifa, utashi na maamuzi ya wanaoingia madarakani kama ilivyotokea siku za nyuma kwa kufutwa kwa baadhi ya masomo na kisha kurejeshwa kunatuyumbisha watu wa chini hasa walimu kuzalisha wasomi wazuri wa kulisaidia taifa," alisema.
Katika mahafali hayo wahitimu 105 walitunukukiwa vyeti na kuzawadiwa kwa waliofanya vyema katika masomo yake shuleni hapo na mwanafunzi Marijani Karanda, aliibuka kidedea kwa kuongoza katika masomo sita kiasi cha kumfanya DC Mercy kumzawadia fedha taslimu.

Shule ya Mwandege Boys yatoa msaada wa vitabu vya Sh Mil 3 Mwandege SM


Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Sillah (kushoto) alianza kwa kusalimiana na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwandege., Joseph Awino kabla uya makabidhiano ya vitabu hivyo. Picha ni hatua kwa hatua mpaka vitabu hivyo vyenye thamani ya Sh. Milioni Tatu vilipokabidhiwa.










UONGOZI wa Shule ya Sekondari ya Mwandege Wavulana iliyopo Mkurunga, Pwani imetoa msaada wa vitabu mbalimbali vyenye thamani ya Sh. Milioni Tatu kwa Shule ya Msingi ya Mwandege ili kusaidia na kukuza kiwango cha taaluma kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Vitabu hivyo vinavyohusisha kamusi na vile vya masomo mbalimbali kwa Shule ya Msingi vilikabidhiwa juzi kwa shule hiyo katika sherehe za mahafali ya tano  ya kidato cha nne ya Shule ya Mwandede Wavulana yaliyofanyika jana katika shule yao wilayani humo.
Mkuu wa Shule wa Mwandede Wavulana, Enock Walter, alisema uongozi wa Shule yao chini ya Bodi ya Wakurugenzi wametoa vitabu hivyo kwa lengo la kusaidia kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi wa shule ya Mwandege ambayo ipo jirani nayo.
Mwl Walter, alisema kwa kuwa wao ni wadau wakubwa wa elimu na wanatambua kufanya vyema kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi ni kuzisaidia Shule za Sekondari kupata wanafunzi bora ndiyo maana wamejitolea kutoa zawadi hiyo aliyoamini itasaidia japo ni ndogo.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Mercy Sillah, aliyevikabidhi vitabu hivyo kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwandege, Joseph Awino, alisema kilichofanya na uongozi wa Shule ya Mwandege Wavulana ni mfano wa kuigwa na wadau wengine wa elimu nchini.
DC huyo, alisema lau wadau wengine wa elimu wangekuwa wakifanya kama ilivyofanya Shule ya Mwandege Wavulana ni wazi kiwango cha elimu ya Tanzania kingepaa, huku akifichua miongoni mwa shule za msingi wilayani humo zinazofanya vyema ni Mwandege.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwandege, Joseph Awino aliishukuru shule ya Mwandege Wavulana kwa msaada huo na kuahidi kuvitumia kwa lengo la kuongeza kiwango cha elimu na ufaulu kwa wanafunzi wake zaidi na ilivyo sasa.
"Tunashukuru kwa msaada huu na Mungu awazidishie Mwandege Boy's na tunaahidi kutumia vitabu hivyo kama vilivyokusudiwa kwa lengo la kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wetu ambao baadhi wanaweza kusoma hapa, ahsanteni sana," alisema Mwl Awino.

Kili Stars yaagwa, wachezaji waahidi makubwa Chalenji 2013

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Henry Lihaya,(kulia) akipeana mkono na kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen kwenye hafla kukabimkabidhi bendera kwa Kilimanjaro Stars inayokwenda kushiriki mashindano ya Chalenji yanayotarajiwa kuanza kesho nchini Kenya. Katikati ni nahodha wa Kilimanjaro Stars Kelvin Yondani. 

Wachezaji wa Kilimanjaro stars
Nahodha mpya wa Kili Stars, Kelvin Yondani 'Vidic' akizungumza huku kocha wake, Kim Poulsen akisikiliza kwa makini
Hiki ndicho kikosi cha Kili Stars
Kikosi cha Kilimanjaro Stars imeagwa leo tayari kwa safari ya Nairobi, Kenya kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza kutimua vumbi Novemba 27 mwaka huu.
Hafla ya kuiaga timu hiyo imefanyika saa 5 asubuhi kambini kwao katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam. Msafara wa Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager unaongozwa na Ahmed Idd Mgoyi. Timu itaondoka saa 10 alasiri kwa ndege ya RwandAir.
Wachezaji waliomo katika msafara huo ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).
Hata hivyo, washambuliaji Samata na Ulimwengu watajiunga na timu hiyo jijini Nairobi, Desemba Mosi mwaka huu wakitokea Lubumbashi ambapo Novemba 30 mwaka huu TP Mazembe itacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Benchi la Ufundi la timu hiyo linawajumuisha Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa Makipa), Leopold Tasso (Meneja wa Timu), Dk Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa Timu), Frank Mhonda (mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza Vifaa).
Kilimanjaro Stars ambayo ipo kundi B katika michuano hiyo itacheza mechi yake ya kwanza Novemba 28 mwaka dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Machakos.