STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, November 9, 2014

Borussia Dortmund yapumua kwa bao la 'kupewa'

Christoph Kramer
Safi sana! Wachezaji wa Borussia wakimpa pole Kramer baada ya kujifunga bao lililowapa pointi tatu muhimu
BAO pekee la kujifunga la Borussia Monchengladbach la dakika ya 58 liliwapa ushindi muhimu timu ya Borussia Dortmund katika mechi ya Ligi ya Ujerumani Bundesliga.
Christoph Kramer alijifunga bao wakati akirudisha pasi ya nyuma kwa kipa wake Yann Sommer na kuifanya Dortmund iliyokuwa mkiani kuchupa hjadoi nafasi ya 15 kwa kufikisha pointi 10.
Wapinzani wao wamesaliwa kwenye nafasi ya tatu nyuma ya timu za Bayern Munich inayoongoza na pointi 27 na Wolfsburg walio na pointi 23 baada ya kuifunga Hamburger  kwa mabao 2-0 katika mechi nyinmgine wakati ligi ikimaliza mzunguko wa 11.

Newz Alert!Rais JK afanyiwa Upasuaji nchini Marekani

 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na  Dkt.Edward Shaeffer wa  hospitali ya Johns Hopkins (kushoto) na Daktari wa Rais Profesa Mohamed Janabi  (kulia) muda mfupi baada ya kuwasili ili kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyopo Baltimore Maryland Marekani Jumamosi asubuhi.Upasuaji huo uliochukua muda wa saa moja na nusu ulifanyika salama.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na daktari Bingwa Mpasuaji Edward Shaeffer muda mfupi kabla ya kuingia kwenye chumba cha upasuaji uliofanyika katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyopo Baltimore Maryland nchini Marekani Jumamosi asubuhi(picha na Freddy Maro)
=======  ======  ======
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete alfajiri ya jana, Jumamosi, Novemba 8, 2014, alifanyiwa
upasuaji wa tezi dume (prostrate) katika Hospitali ya Johns Hopkins
iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.
Rais Kikwete amefanyiwa upasuaji huo baada ya madaktari waliomfanyia
uchunguzi wa afya yake kujiridhisha kuwa Rais alikuwa anahitaji
matibabu ya aina hiyo.
Upasuaji huo uliofanyika alfajiri na kuchukua kiasi cha saa moja
unusu, umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa. Hali ya Mheshimiwa Rais Kikwete inaendelea vizuri, bado yuko wodini akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba.
Wananchi wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais Kikwete
kwa kadri zitakavyokuwa zinapatikana.
Imetolewa na
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU
DAR ES SALAAM,
NOVEMBA 9, 2014

Arsenal yagongwa 2-1 na Swansea


Lukasz Fabianski
Kipa wa zamani wa Arsenal, Lukasz Fabianski aliinyima mabao na kuibeba Swansea
Danny Welbeck
Danny Welbeck akifumua shuti ambalo hata hivyo halikuzaa bao katika kipindi cha kwanza.
Santi Cazorla
Mshambuliaji wa Arsenal Santi Cazorla akigangwa baada ya kuumizwa
Gylfi Sigurdsson
Gylfi Sigurdsson akishangilia bao lake la kuwasawazisha na wachezaji wenzake wa Swansea
Arsenal dejected
Wachezaji wa Arsenal wakiwa hoi baada ya bao lao kusawazishwa
BAADA ya kugawa dozi kwa wapizani wao mfululizo, Arsenal imejikuta ikiangukia pua baada ya kunyukwa mabao 2-1 ugenini na Swansea City.
Alexis Sanchez alifunga bao lake la sita katika mechi nne akimalizia kazi nzuri ya Danny Welback dakika chache baada ya kuanza kupindi cha pili, kabla ya nyota wa zamani wa Spurs, Gylfi Sigurdsson kusawazisha kwa mpira wa frii kiki dakika ya 75.
dakika tatu baadae mtokea benchi, Bafetimbi Gomis alifunga bao tamu la kichwa na kuwazima vijana wa Arsene Wenger ambao hicho ni kipigo chao cha pili msimu huu.

Mtibwa Sugar Hakunaga, Mbeya City hadi huruma

Wanaume!
http://3.bp.blogspot.com/-qZ4LPiEqNno/UCx3mruTiNI/AAAAAAAAM54/hThCPW5QOpM/s1600/Mecky+Mexime.jpg
Kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime
http://www.kabumbu.co.tz/wp-content/uploads/2014/09/mbeya-city.jpg
Waliofulia msimu huu, Mbeya City
WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikienda mapumziko, Mtibwa Sugar imethibitisha kuwa ndiyo timu bora mpaka sasa ikiwa kileleni mwa msimamo na pointi zake 15 baada ya mechi saba, kadhalika ikiruhusu mabao matatu tu huku timu nyingine 'urojo' kwa kuwa na kuta laini ziliruhusu magoli mengi.
Mtibwa inayonolea na kocha kijana mzawa, Mecky Mexime imezishinda hata timu kubwa zilizotamba kabla ligi haijaanza kwa usajili wa mamilioni ya fedha, huku washambuliaji wake wawili, Ame Ally Zungu na Ali Shomari wakifunga jumla ya mabao saba kuonyesha kombinesheni yao ilivyokuwa kali zaidi.
Magoli mengine ya Mtibwa yamefungwa na wakongwe Mussa hassan Mgosi mwenye mawili na Vincent Barnabas.
Mbeya City iliyosumbua msimu uliopita ikiicheza ligi hiyo kwa mara ya kwanza imejikita ndiyo nyonge zaidi msimu huu kwa kuburuza mkia ikiwa na pointi tano tu baada ya mechi saba ilizocheza kitu kilichowaacha mashabiki wa soka wa klabu hiyo kushindwa kuamini hali iliyowakuta.
Timu hiyo inayofundishwa na Juma Mwambusi Kocha Bora msimu uliopita imeshinda mara moja tu na kupoteza mechi nne na kuambulia sare michezo mitatu.
Ndanda iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutamba na Mbeya City wenyewe nao wameoonekana siyo lolote baada ya kushika nafasi ya pili toka mkiani ikiwa na pointi sita tu iliyotoakana na kushinda mechi mbili na nyingine zilizosalia imepoteza ikiwa ndiyo timu pekee pamoja na Mgambo ambazo hazijapata droo katika ligi ya msimu huu.
Kwenye mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu, Didier Kavumbagu aliyeanza kwa kasi 'amefungwa' spidi gavana kwani mpaka sasa amesaliwa na bao zake nne ambazo zimefikiwa na wachezaji aliokuwa amewaacha nyuma.
Kasi ya washambuliaji wa kizawa inatoa picha kwamba huenda safari hii Kiatu hicho kikatoka mikononi mwa wageni kama alivyoahidi Ali Shomari mwenye mabao mawili anayeichezea Mtibwa.
Ebu angalia msimamo na orodha ya wakali wa mabao mpaka sasa ligi ikienda mapumziko hadi Desemba 27.
MSIMAMO LIGI KUU TANZANIA BARA 2014-2015
                               P   W    D    L    F    A   GD  Pts
01. Mtibwa Sugar    07  04   03  00  10  03  07   15
02. Yanga               07  04   01  02  09  05  04   13
03.  Azam               07  04   01  02  08  04  04   13
04. Coastal Union    07  03   02  02  09  07  02   11
05. Kagera Sugar    07  02   04  01  06  04  02   10
06. JKT Ruvu          07  03   01  03   07  07  00  10
07. Simba               07  01   06  00   07  06  01  09
08. Polisi Moro        07  02   03  02   06  07   -1  09
09. Mgambo JKT     07  03   00  04   04  07   -3  09
10. Stand Utd         07  02   03  02   05   09  -4   09
11. Ruvu Shooting  07  02   01  04   04   07   -3  07
12. Prisons             07  01   03  03   06   07   -1   06
13. Ndanda Fc        07  02   00  05   08   12   -4   06
14. Mbeya City       07   01   02  04   02   06   -4   05

Wafungaji Bora:

4- Didier Kavumbagu(Azam), Rama Salim (Coastal), Danny Mrwanda (Polisi-Moro) Ame Ally (Mtibwa)
3- Ally Shomari (Mtibwa), Emmanuel Okwi (Simba), Rashid Mandawa (Kagera Sugar), Simon Msuva (Yanga)
2- Shaaban Kisiga (Simba), Nassor Kapama (Ndanda) Salum Kanoni (Kagera), Aggrey Morris (Azam), Najim Magulu, Samuel Kamuntu, Jabir Aziz (JKT Ruvu), Jerry Tegete (Yanga), Ibrahim Kihaka (Prisons), Mussa Mgosi (Mtibwa), Heri Mohammed (Stand Utd), Ally Nassorm Balimi Busungu (Mgambo)

Juventus yaiangamiza Parma 7-0 Italia

http://www2.pictures.zimbio.com/gi/Stephan+Lichtsteiner+Juventus+v+Parma+FC+Serie+wN6nAJVItT9l.jpgMABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Serie A, Juventus imeifanyia mauaji ya kutisha timu ya Parma kwa kuicharaza mabao 7-0 katika mfululizo wa ligi hiyo.
Juve wakiwa uwanja wa nyumbani walipata ushindi huo kupitia mabao yaliwekwa kimiani na Llorente, Carlos Tevez na Alvaro Morata waliofunga mawili kila mmoja na jingine la Stephan Lichtsteiner.
Llorente alianza kuandika bao dakika ya 23 kabla ya Lichtsteiner kuongeza la pili dakika ya 29 na Llorente kurudi tena dimbani kwa kufunga bao la tatu katia dakika ya 36.
Carlos Tevez alifunga mabao mawili ndani ya dakika nane katika dakika ya 50 na 58 kabla ya Álvaro Morata kumalizia kazi katika dakika ya  76 na 88.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Cagliari na Genoa zilitoshana nguvu kwa kufunga bao 1-1, huku Chievo Verona ikipata ushindi nyumbani dhidi ya Cesema kwa kuilaza mabaop 2-1, Empoli ikainyoa Lazio pia mabao 2-1 na Palermo ililazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Udinese.

Spurs yapigwa tena, Newcastle yatakata, Everton droo

Bojan
Stoke wakishangilia mabao yao dhidi ya Spurs
Ayoze Perez, Newcastle
Newcastle United iliyoitambia WBA nyumbani kwao
Leighton Baines
Everton wakifunga bao lao dhidi ya Sunderland
WAKATI Tottenham Hotspur ikiendelea kutoa takrima nyumbani kwake kwa kuruhusu kipigo kingine toka kwa Stoke City kwa kulazwa mabao 2-1, Newcastle United imeendelea na maajabu yake baada ya kupata ushindi ugenini dhidi ya West Bromwich Albion katika mfululizo wa Ligi Kuu ya England.
Newcastle ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wao kupitia kwa Ayoze Perez aliyefunga dakika ya 45 kabla ya Fabricio Coloccini aliyemaliza udhia katika dakika ya 62.
Spurs ambayo imekuwa ikifanya vyema kwenye Ligi Ndogo ya Ulaya, ilikumbana na kipigo kingine cha aibu nyumbani uwanja wa White Hartlane kutoka kwa Stoke City.
Wageni waliandika bao la kuongoza dakika ya 6 kupitia Bojan kabla ya Jonathan Walters kuongeza la p[ili dakika ya 33 na Spurs kupata la kufutia machozi kipindi cha pili katika dakika ya 77 kupitia Nacer Chadli, ksiha wenyeji kumpoteza beki wake Naughton kwa kucheza madhambi dhidi ya Victor Moses.
Katika pambano jingine la ligi Everton imejikuta iking'ang'aniwa ugenini na Sunderland kwa kulazimishwa sare ya 1-1.
Pambano linaloendelea sasa ni Arsenal ikiwa ugenini inaumana na Swansea City

Simba yaona mwezi, JKT Ruvu yaizima Ndanda x2

http://www.hivisasa.co.tz/wp-content/uploads/2014/09/OKWI-VS-GOR-MAHIA.jpg
HATIMAYE klabu ya Simba jioni ya leo imeodnoa 'gundu' baada ya kuichapa Ruvu Shooting kwa bao 1-0 katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa ni ushindi wa kwanza katika mechi 13 ilizocheza tangu msimu uliopita.
Bao pekee lililowapa faraja wana Simba liliwekwa kimiani na Mganda Emmanuel Okwi katika dakika ya 78 akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Ruvu Shooting aliyepangua kiki ya Elias Maguli.
Simba ambayo ilikuwa imetoka sare mechi sita zilizopita ilikuwa ikihitaji ushindi kwa hali yoyote ili kutuliza munkari ya mashabiki na wanachama wao sambamba na kuondoa dhana kwamba 'HAIWEZI KUSHINDA' mpaka uongozi ukutane na kundi na wanachama walipachikwa jina la UKAWA.
Kwa ushindi huo Simba imefikisha jumla ya pointi 9 na kuchuku toka nafasi ya 11 hadi nafasi ya saba wakati ligi ikienda mapumziko kwa wiki kadhaa.
Bao alililofunga leo Taifa limemfanya Okwi kufikisha jumla ya mabao matatu moja nyuma ya wachezaji waongooza kwenye orodha ya vinara wa mabao wa ligi hiyo, Danny Mrandwa wa Polisi-Moro, Ame Ally 'Zungu', Didier Kavumbagu wa Azam na Rama Salim wa Coastal Union.
Katika mechi nyingine iliyochezwa uwanja wa Chamazi, JKT Ruvu wameizima Ndanda Fc ya Mtwara kwa kuichapa mabao 2-0.
Vijana wa Fred Felix Minziro waliotoka kupokea kipigo cha bao 2-1 toka Polisi Moro walipata mabao yake kupitia kwa Samuel Kamuntu na Najim Magulu na kuifanya JKT kufikisha jumla ya pointi 10 na kukwea hadi nafasi ya sita.

Diafra Sanko, Big Sam wang'ara EPL Oktoba

WASHINDI wa tuzo za Ligi Kuu ya England Oktoba, wametajwa na mshambuliaji wa West Ham United, Diafra Sakho ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi huo.
Kocha wa West Ham United, Sam Allardyce pia ameshinda tuzo ya Kocha Bora wa Mwezi, akiwashinda kocha wa Hull City, Steve Bruce, Jose Mourinho wa Chelsea na Alan Pardew wa Newcastle United.
Sakho amekuwa katika kiwango kizuri The Hammers tangu ajiunge nayo kutoka Metz msimu huu na mwezi uliopita alifunga mabao matatu na kutoa pasi ya bao moja, West Ham ikizifunga QPR, Burnley na Manchester City.
Wengine walioingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo hiyo ni Sergio Aguero wa Man City, Leighton Baines wa Everton, Saido Berahino wa West Bromwich Albion, Alexis Sanchez wa Arsenal na Dusan Tadic wa Southampton.
Diafra Sakho amekuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu England Oktoba na kocha wake, Sam Allardyce nae amepewa nafasi hiyo kwa mwezi Octoba.

Ruvu Shooting kuvunja 'ndoa' ya Simba, Phiri? JKT, Ndanda Chamazi

http://1.bp.blogspot.com/-bdeY6ALCWMw/VDApTyxy8_I/AAAAAAAAppw/mBc2LYYxgvs/s1600/HMB_8444.JPG
Simba watashangilia kama hivi au itakuwa 'majanga'
Patrick Phiri, Kocha wa Simba akizungumza na wachezaji wake
Ruvu Shooting waliotamba kuigaragaza Simba leo Taifa. Wataweza?
http://3.bp.blogspot.com/-JOe_CaqBtZ8/VDDvhx2SD6I/AAAAAAAANfg/eTgmm4bMDPE/s1600/JKT%2BRUVU%2B2014.JPG
JKT Ruvu itavuna nini kwa Ndanda Fc leo Chamazi?
http://3.bp.blogspot.com/-NXJDcVCWLvU/VBRkZtkm6NI/AAAAAAAACrc/72CxWBdgpzg/s1600/20140913_160438.jpg
Ndanda Fc itaendeleza kipigo baada ya kuzidnuka kwa Azam?
WAKATI uongozi wa klabu yake ukikanusha taarifa za kuwa na mipango ya kumleta aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen, kocha  Patrick Phiri leo atakuwa katika kibarua kizit cha kulinda ajira yake wakati wake wa Simba watakaposhuka dimbani kuwakabili Ruvu Shooting katika mechi ya mwisho kati ya mbili alizopewa na uongozi.
Uongozi wa Simba ulitangaza kumpa kocha huyo wa kimataifa kutoka Zambia mechi mbili za mwisho kabla ya kumfuta kazi kama Simba haitaweza kupata ushindi. Mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Mtibwa ambayo iliisha kwa sare ya 1-1, ikiwa ni sare ya sita mfululizo kwa mabingwa hao wa zamani wa soka nchini.
Matokeo yoyote tofauti na ushindi kwa Simba leo itakuwa na maana kwamba Phiri atafungasha virago vyake kurudi kwao Zambia kwani atakuwa ameshindwa kutekeleza masharti ya mabosi wake ambao waliibuka katikati ya wiki kukanusha taarifa za kuwepo na mipango ya kumleta Kim Poulsen kuchukua nafasi ya Mzambia huyo.
Hata hivyo Phiri pamoja na vijana wake walionukuliwa wakidai kuwa wapo tayari kufutwa naye kazi kuliko kuona anaondolewa kwa sababu sare wanazopata ni sehemu ya matokeo ya mchezo, wameapa kufa na Ruvu ambayo baada ya ushindi mfululizo katika ligi hiyo ilijikuta wakizimwa na mabingwa wa zamani Coastal Union kwa kulazwa bao 1-0.
Phiri alisema hana hofu ya kutimuliwa kwani makosa yaliyowagharimu katika mechi zilizopita yamerekebishwa na leo wadau wa Msimbazi wajiandae kucheka kwa furaha ya ushindi kwa mara ya kwanza baada ya mechi 11 mfululizo.
Simba ambayo itaendelea kukosa huduma za nyota wake watatu, Shaaban Kisiga mwenye mabao mawili mpaka sasa katika orodha ya wafungaji msimu huu, Amri Kiemba na Haruna Chanongo wamesimamishwa muda usiojulikana kwa madai ya utovu wa nidhamu na kucheza chini ya kiwango.
Pia haitakuwa na kipa wao Hussein Sharrif 'Casillas' anayeuguza jehara la upasuaji wa ugoko aliofanyiwa Afrika Kusini hivi, lakini itakuwa na mkali wao kutoka Uganda, Emmanuel Okwi ambaye mpaka sasa amefunga mabao mawili.
Ruvu Shooting wenyewe kupitia Msemaji wao, Masau Bwire imekuwa ikisisitiza kuwa, Simba isitarajie mteremko na kuwa klabu ya kwanza kuwapa pointi tatu kwa sababu wamepania kuwapa kipigo ili kuurahisishia kazi uongozi juu ya azma yao ya kumtimua kocha Phiri.
"Hapa kwetu hata sare hawapati, maana tulisikia kundi la 'waasi' ndani ya klabu hiyo Ukawa kuwa Simba ingepata sare mfululizo mechi saba. Sisi ndiyo tutakaokuwa klabu ya kwanza kuwafunga Simba msimu huu. Tumepania na Simba isitarajie wepesi kwetu," alisema Bwire.
Bwire alisisitiza kipigo walichopewa na Coastal kimewazindua na kurekebisha kikosi chao ili kuendeleza wimbi la ushindi kama ilivyokuwa awali kwa kuzifunga Ndanda nyumbani kwao na baadaye Polisi Moro uwanja wa Mabatini.
Ruvu Shooting wana pointi 7 baada ya mechi sita wakishinda mbili, kutoka sare moja na kupoteza tatu wakiwa kwenye nafasi ya nane wakati wapinzani wa wakishika nafasi ya 10 wakiwa na pointi 6.
Katika mfululizo wa ligi hiyo leo pia kutakuwa na pambano jingine litakalozikutanisha timu za JKT Ruvu dhidi ya Ndanda, huku kila timu ikiwa katika hali tofauti, Ruvu ikiuguza kipigo cha Polisi-Moro na Ndanda ikichekelea kuitoa nishai Azam katika mechi zao zilizopita.

Marehemu Amigolas kuzikwa kesho makaburi ya Kisutu

Amigolas enzi za uhai wake
MWILI wa aliyekuwa kiongozi na mwanamuziki wa bendi ya Ruvu Stars aliyewahi kutamba na benchi za Bicco Stars, Chezimba Band na African Stars 'Twanga Pepeta', Khamis Kayumbu 'Amigolas' unatarajiwa kuzikwa kesho baada ya swala ya Alasir katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na MICHARAZO muda mfupi uliopita, mmoja wa viongozi na mwanamuziki aliyefanya kazi kwa muda mrefu na Amigolas, Rogert Hegga 'Catapillar' alisema kuwa, imethibitika kuwa mwili wa mwenzao utahifadhiwa kesho saa 10 jioni kwenye makaburi ya Kisutu.
Hegga alisema awali mama wa marehemu baada ya kuwasiliana na ndugu na jamaa waliopo mikoa ya Tabora na Kigoma, ilikuwa marehemu azikwe leo, lakini kutokana na rai ya watu wengi kutokana na umaarufu aliokuwa nao Amigolas, mwili huo sasa utazikwa kesho.
"Baada ya mama wa marehemu kuzungumza na ndugu na jamaa zake waliopo Tabora na Kigoma, imeamuliwa marehemu azikwe kesho (leo) Jumatatu baada ya swala ya Alasir," alisema Hegga.
Muasisi huyo wa Twanga Pepeta aliyewahi kutamba na wimbo wa 'Aminata', alifariki usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili alikolazwa kwa maradji ya Moyo.

Mtibwa Sugar yang'ang'aniwa na Kagera, kiporo chao chaisha 1-1

Kikosi cha Mtibwa kilicholazimishwa sare ya 1-1 na 'ndugu' zao wa Kagera Sugar
VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mtibwa Sugar imeshindwa kulinda ushindi wake iliyopata katika dakika 45 za kwanza zilizochezwa juzi baada ya jana Kagera Sugar kurudisha bao na kufanya matokeo kuwa bao 1-1.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, dakika 45 za pili zilipigwa jana asubuhi kwenye uwnaja wa Manungu Complex, Turiani na Kagera kupata ushindi wa bao 1-0.
Bao la Kagera liliwekwa kimiani na Rashid Mandawa katika dakika ya 56 na kuwa la kusawazisha ambalo Mtibwa Sugar ilipata katika dakika 45 za kwanza zilizochezwa juzi kwenye uwanja huo kabla ya pambano kuvunjwa kwa sababu ya mvua kubwa iliyonyesha.
Katika dakika 45 za kwanza bao la Mtibwa liliwekwa kimiani na Ame Ally 'Zungu' dakika mbili kabla ya mapumziko na kumfanya mshambuliaji huyo aliyesajiliwa akitokea Chuoni ya Zanzibar kufikisha bao la nne.
Idadi hiyo imemfanya kulingana na wachezaji Didier Kavumbagu wa Azam na Danny Mrwanda wa Polisi.
Matokeo hayo yameifanya Mtibwa kwenda mapumziko nikiwa bado kileleni ikiwa na pointi 15, ikifuatiwa na Yanga na Azam zenye pointi 13 kila moja na Coastal Union ikifuatiwa na pointi zake 11.

MSIMAMO WA LIGI ULIVYO SASA:

                               P   W   D    L   F    A   GD  Pts
01. Mtibwa Sugar    07  04  03  00  10   03  07  15
02. Azam                07  04  01  02   08  04  04  13
03. Yanga               07  04  01  02  09   05  04  13
04. Coastal Union   07  03  02   02  09   07  02 11
05. Kagera Sugar   07  02  04   01  06   04  02  10
06. Polisi Moro        07  02  03  02   06   07  -1  09
07. Mgambo JKT    07  03  00  04   04   07   -3  09
08. Stand Utd         07  02  03  02   05   09  -4  09
09. JKT Ruvu         06   02  01  03   05   07  -2  07
10. Ruvu Shooting 06  02  01  03   04   06  -2  07
11. Simba              06  00  06  00   06   06  00  06
12. Prisons            07  01  03  03   06   07   -1  06
13. Ndanda Fc       06  02  00  04   08  10   -2  06
14. Mbeya City       07  01  02  04   02   06  -4  05

Wafungaji:
4-
Didier Kavumbagu(Azam), Ame Ally (Mtibwa), Danny Mrwanda (Polisi-Moro)

Kiatu cha Dhahabu chawatenganisha Mastrika Mtibwa Sugar

http://3.bp.blogspot.com/-E0dqBrSc33w/UvJsnTqlICI/AAAAAAAAODQ/zBjwlonXZAA/s1600/ALLY+SHOMARI+MTIBWA+NA+ISSA+RASHID+SIMBA+PIX+NO+1.JPG
Ali Shomari (kushoto) akichuana na Baba Ubaya
Ame Ally 'Zungu' akiwajibika siku ya mechi yao na Simba
WASHAMBULIAJI wawili nyota wanayoibeba kwa sasa Mtibwa Sugar, Ally Shomari 'Shiboli' na Ame Ally 'Zungu' kila mmoja amekuwa na mtazamo wake kuhusiana na kasi yao ya kufunga mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara mmoja akiota Kiatu cha Dhahabu mwengine akikipotezea ila akitaka kuipa Mtibwa ubingwa wake wa tatu katika historia ya kandanda la Tanzania.
Wakali hao ambao kila mmoja amefunga mabao matatu (japo Zungu jana alifunga wakati wa pambano lao na Kagera Sugar ambalo lilitarajiwa kurudiwa leo asubuhi kumaliza dakika 45 za mwisho) waliiambia MICHARAZO kwa nyakati tofauti kwamba wanachekelea kuendelea kufunga mabao ili kuisaidia Mtibwa kutimiza ndoto iliyoweka mara ya mwisho miaka 14 iliyopita.
Ame Ally amesema yeye anafurahia kufunga mabao mengi zaidi akiwa hana ndoto ya kuja kunyakua Kiatu cha Dhahabu tofauti na Shomari alisema anakitamani mno kiatu hicho ambacho kimekuwa mikononi mwa wachezaji wa kigeni kwa misili miwili mfululizo iliyopita akianza Kipre Tchetche wa Azam kabla ya Amissi Tambwe wa Simba kumpokea msimu uliopita.
"Kila mchezaji ana malengo yake, mimi nafurahia kufunga mabao kwa sababu ya kutaka kuisaidia Mtibwa, nataka kuibebesha taji baada ya kunyakua mara ya mwisho ubingwa mwaka 2000, suala la tuzo ya Mfungaji Bora labda lije tu kwa bahati mbaya," alisema Ame aliyetua Mtibwa msimu huu akitokea Chuoni inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar.
Kwa upande wa Shomari anayeichezea Mtibwa kwa msimu wa pili sasa baada ya kunyakuliwa mwaka juzi akitokea Polisi-Moro wakati ikishuka daraja, alisema anakitamani Kiatu cha Dhahabu na amepania kuwa Mfungaji Bora sambamba na kuisaidia Mtibwa kuwa bingwa mpya wa Tanzania.
"Nakitamani mno Kiatu cha Dhahabu kwa msimu huu, nitapambana kuhakikisha nafunga mabao mengi ili kurejesha kiatu hicho mikononi mwa wazawa, ingawa natambua ushindani utakuwa mkubwa kuliko ilivyokuwa msimu uliopita, ambapo Tambwe alitwaa kiatu hicho kwa mabao 19 huku anayemfuata akiwa na mabao 13," alisema.
Nyota hao wawili ambao wanakamata nafasi ya pili kwa sasa ya wafumania nyavu nyuma ya Didier Kavumbagu wa Azam mwenye mabao manne kwa ujumla wao wameifungia Mtibwa mabao sita, huku mengine yakiwekwa kimiani na Mussa Mgosi mwenye mabao mawili na Vincent Barnabas aliye na bao moja kati ya mabao 9 ya mabingwa hao wa zamani wa Tanzania waliopo kileleni kwa sasa.

Pacquiao kutua nchini mwakani, Mtanzania kusindikiza pigano lake Macao

http://fightnights.com/uploads/manny-pacquiao.jpg
Manny Pacquiao
BINGWA wa Dunia wa WBO uzani wa Welter, Manny Pacquiao anatarajiwa kutua nchini Februari mwakani kuja kushuhudia pambano la kimataifa la Ngumi za Kulipwa kama mgeni rasmi.
Aidha mmoja kati ya mabondia watatu wa uzani wa Feather (kilo 57) Cosmas Cheka, Sadiki Momba au Mohammed Matumla 'Snake Boy Jr' anatarajiwa kuteuliwa kwenda kupigana pambano la utangulizi wakati Pacquiao atakapokuwa akitetea taji lake dhidi ya Chris Algieri siku ya Novemba 22.
Pambano hilo la Pacquiao na Algieri litafanyika kwenye ukumbi wa Cotai Arena, Venetian Resort mjini Macoa nchini China.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania, PST, Anthony Rutta aliliambia MICHARAZO kuwa walikuwa wakifanya mazungumzo na meneja wa bingwa huyo wa dunia na mwanasiasa nchini Ufilipino aje nchini mwakani.
Rutta alisema PST kupitia Bingwa wa zamani wa dunia wa uzito wa juu wa WBF,  Francois Botha aliyekuja nchini wakati wa pambano la Francis Cheka dhidi ya Mmarekani, Phil Williams wanafanya mazungumzo ili bondia huyo kuja nchini.
"PST inafanya mpango wa kumleta Manny Pacquiao nchini Februari kuja kuwa mgeni rasmi wa pambano la kimataifa kati ya bondia wa Tanzania mpinzani wa kigeni toka Ulaya," alisema Rutta.
Alisema mipango hiyo inakuja wakati PST imepata ofa ya kumpeleka bondia mmoja kucheza pambano la utangulizi wakati Pacquiao akitetea taji lake na Algieri wiki mbili zajazo.
"Tumepewa ofa kupitia Botha kutuma bondia mmoja kucheza pambano la utangulizi wakati Mfilipino huyo akitetea taji lake na hii itakuwa mara ya kwanza kwa bondia wa Tanzania kushindikiza pambano kubwa kama hilo," alisema.
Alisema kwa sasa wanafanya mchakato wa kuteua bondia mmoja kati ya watatu wenye sifa na kilo ziliotakiwa kati ya Momba, Matumla na Cheka mdogo.
"Mmoja kati ya mabondia hao atateuliwa kwenda Macao kupigana, hii ni fursa ya kipekee kwa mabondia wa Tanzania," alisema Rutta.

HUYU NDIYE KHAMISI KAYUMBU 'AMIGOLAS' NYOTA ILIYOZIMIKA!

http://api.ning.com/files/bxro-84u7tLTBDW*nWcDoDyvNYEN440Q-1k-yefa1CDbcO9VA7*n8Q*KCtSLmpJwtvHZpC9ml6ZohUFZxoZDGatCYgbNkixq/Amigolas_1001.jpg?width=550
TASNIA ya Sanaa nchini imeendelea kupata machungu baada ya mmoja wa wanamuziki mahiri nchini, Khamis Kayumbu maarufu kama 'Amigolas' kufariki usiku wa kuamkia leo baada ya kuugua ugonjwa wa Moyo uliomfanya alazwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa siku kadhaa.
Mwanamuziki huyo aliyekuwa mkali wa utunzi na uimbaji aliyewahi kuziimbia bendi ya Bicco Stars, Chezima, African Stars kabla ya kutua Ruvu Stars aliyokuwa na mauti akiwa ndiye kiongozi wake.
MICHARAZO ina bahati ilifanya mahojiano maalum na mwanamuziki huyo katikati ya mwaka huu ambapo aliweka bayana mahali alipotoka, alipo na mipango yake ya baadaye, ingawa ndoto hazijatimia baada ya mauti kumkumba akiwa katika harakati za kuingia studio kurekodi nyimbo tatu za mwisho za bendi yake.
http://3.bp.blogspot.com/-ArtG68vJtOE/UgiyuMNJCII/AAAAAAAAR1k/qJLAfAsfOl4/s640/amigo.jpg
Ebu chungulia mahojiano hayo yaliyozaa makala iliyotoka kwenye gazeti la NIPASHE sambamba na kwenye blogu hii;

NYOTA wa muziki wa dansi nchini aliyewahi kutamba na bendi kadhaa ikiwamo African Stars 'Twanga Pepeta', Khamis Kayumbu 'Amigolas' amesema katu hatausahau mwaka 1995 maisha mwake.
Unajua kwanini?
Amigolas anasema mwaka huo ndiyo alipohamia rasmi katika bendi ya African Stars na kudumu nayo hadi mwaka 2013 ikiwa ni zaidi ya miaka 10 kabla ya kutua Ruvu Stars aliyepo kwa sasa kama kiongozi.
Anasema pia ni mwaka ambao alikaribia kwenda Ahera baada ya kuvamiwa na majambazi nyumbani kwake na kucharagwa mapanga mwilini mzima na wakora hao kabla ya kuokolewa na majirani zake.
"Itanichukua muda mrefu kuusahau mwaka huu, nilikuwa nife kama siyo majirani kuwahi kutoka baada ya mayowe tuliyopita, ila wakora hao waliofahamika kama Komando Yosso walinijeruhi," anasema.
Mtunzi na muimbaji huyo aliyewahi kuzipigia bendi za Bicco Stars na Chezimba Band, anasema anashukuru majirani hao walisaidia kuwafanya majambazi hayo kushindwa kumpora mali yoyote.
"Hawakufanikiwa kupora chochote zaidi ya kutujeruhi mimi na familia yangu, ilikuwa balaa na pengine ningekuwa marehemu kwa sasa kama siyo majirani kutoka mapema na kutuokoa," anasema.
Mwanamuziki huyo aliyevutiwa kisanii na gwiji, Hassan Rehani Bitchuka anasema anashukuru matibabu aliyopata yalimsaidia kumrejeshea uhai wake na kudunda mpaka leo akimshukuru Mungu.
Amigolas anashukuru muziki kumsaidia kwa mambo mengi ikiwamo kupata umaarufu na kutembelea mataifa mbalimbali duniani anasema kila akikumbuka tukio hilo usisimkwa kwa asivyoponea chupuchupu.
 http://2.bp.blogspot.com/_a_xKoIDsA80/TVF7EKD6LFI/AAAAAAAALBU/AtIO0-ITIwo/s1600/ASHA.JPG
AMINATA
Amigolas anayependa kula wali na ugali kwa dagaa, kisamvu, samaki au kuku anasema licha ya kutojikita sana kwenye utunzi amewahi kutunga nyimbo chache zilizomjengea jina kubwa kwa mashabiki.
Moja wa nyimbo hizo ni 'Aminata' alioutunga Twanga Pepeta ambao unaendelea kutamba mpaka sasa, nyingine zikiwa ni 'Kila Mja Ana Kilio Chake' na sasa anajiandaa kuibuka na 'Kioo' akiwa na Ruvu.
"Nashukuru moja ya nyimbo zangu, Aminata mpaka sasa unatamba na kusumbua kuanzia redioni hadi videoni," anasema.
Shabiki huyo wa klabu ya Simba na Chelsea ya England anasema muziki wa Tanzania umepiga hatua kubwa, lakini bado hakuna umoja, upendo na mshikamano baina ya wanamuziki na wamiliki wa bendi.
"Pia watangazaji na hata Wizara inayohusisha na sanaa na Utamaduni na Michezo imeupa kisogo sana muziki wa dansi, kitu ambacho kinakatisha tamaa," anasema.

http://www.bongo5.com/wp-content/uploads/2012/03/twanga1.jpg
MARUFUKU
Amigolas mwenye mke na watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume anasema anashukuru wanae kutokuwa na mzuka wa muziki na hatamani wanae kujiingiza kwenye fani hiyo.
"Sitaki hata kidogo wanangu wawe wanamuziki na ninashukuru hakuna hata mmoja mwenye mzuka na fani hii," anasema.
Mkali huyo anayejishughulisha na biashara zinazosimamiwa na mkewe, baada ya kutambulishwa na Bicco Stars aliokaa nao tangu 1991-94, alihamia Chezimba kabla ya 1995 kutua African Stars.
"Nimekaa Twanga Pepeta nikishiriki karibu albamu zote na mwaka jana nikaona ngoja nibadilishe upepo na nina matumaini makubwa ya kupiga hatua kimafanikio na kimuziki nikiwa na Ruvu Stars," anasema.
Mwanamuziki huyo anawashukuru mama yake mzazi, Asha Suleiman, familia yake yaani mke na wanawe pamoja na rafiki zake hasa Marcus toka Uswisi anayedai amekuwa akimsapoti kwa muda mrefu.

Senzo Meyiwa kuweka rekodi Tuzo wa Mwanasoka Bora Afrika 2014?


http://www.chronicle.co.zw/wp-content/uploads/2014/10/senzo-meyiwa-1.jpg
Senzo Meyiwa enzi za uhai wake
http://en.africatopsports.com/wp-content/uploads/2013/02/665605-yaya-toure.jpg
Yaya Toure kutetea tena tuzo yake ya Mwanasoka Bora Afrika
ALIYEKUWA kipa na nahodha wa timu za Orlando Pirates na Bafana Bafana (timu ya taifa ya Afrika Kusini) Senzo Meyiwa aliyeuwawa kwa risasi na majambazi ameteuliwa kuwania tuzo za Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika 2014.
Jina la kipa huyo aliyekuwa na miaka 27 ni miongoni mwa orodha ya wanasoka walioteuliwa na Shirikisho la Soka Brani Afrika, CAF iliyotangazwa kwa ajili ya tuzo za Mwanasoka Bora Afrika na wale wanaocheza nyumbani kwa mwaka 2014.
Iwapo ataibuka kidedea ataweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza Marehemu kushinda tuzo hiyo.
Katika orodha ya Mwanasoka Bora Afrika, mtetezi Yaya Toure ameteuliwa tena kuwania tuzo hiyo akichuana na wakali kama  Emmanuel Adebayor wa Togo, Ahmed Musa wa Nigeria na Kwado Asamoah wa Ghana, huku Mbwana Samatta aliyekuwa kwenye orodha ya mwaka jana akipigwa chini safari hii.
Jumla ya wachezaji 25 wameingia kwenye kinyang'anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika, wakati wengine 20 watawania tuzo ya Mchezaji anayecheza Afrika.
Washindi wa vipengele hivyo viwili watapatikana baada ya kura zitakazopigwa na Makocha Wakuu na Wakurugenzi wa Ufundi wa vyama vya soka na Mashirikisho wanachama wa CAF.
Sherehe za tuzo zitafanyika Alhamisi ya Januari 8, mwakani mjini Lagos, Nigeria. Yaya Toure ndiye anashikilia tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika, wakati Mohamed Aboutreika wa Misri anashikilia tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika ambaye hata hivtyo safari hii hayupo.

Orodha kamili ya Wanasoka walioteuliwa kuwania tuzo hizo mwaka huu ni kama ifuatavyo;

TUZO YA MWANASOKA BORA AFRIKA1.    Ahmed Musa       (Nigeria, CSKA Moscow)
2.    Asamoah Gyan    (Ghana, Al Ain)
3.    Dame N’doye       (Senegal, Lokomotiv Moscow)
4.    Emmanuel Adebayor (Togo, Tottenham)
5.    Eric Maxim Choupo-Moting  (Cameroon, Schalke)
6.    Fakhreddine Ben Youssef     (Tunisia, CS Sfaxien)
7.    Ferdjani Sassi                   (Tunisia, CS Sfaxien)
8.    Yao  Gervais ‘Gervinho’ (Ivory Coast, Roma)
9.    Islam Slimani             (Algeria, Sporting Lisbon)
10. Kwadwo Asamoah     (Ghana, Juventus)
11. Mehdi Benatia           (Morocco, Bayern Munich)
12. Mohamed El Neny     (Misri, Basel)
13. Pierre-Emerick Aubameyang(Gabon,B. Dortmund)
14. Raïs M'Bolhi             (Algeria, Philadelphia Union)
15. Sadio Mané               (Senegal, Southampton)
16. Seydou Kieta             (Mali, As Roma)
17. Sofiane Feghouli       (Algeria, Valencia)
18. Stephane Mbia         (Cameroon,  Sevilla)
19. Thulani Serero           (Afrika Kusini, Ajax)
20. Vincent Aboubakar     (Cameroon, Porto)
21. Vincent Enyeama       (Nigeria, Lille)
22. Wilfried Bony             (Ivory Coast, Swansea)
23. Yacine Brahimi         (Algeria, Porto)
24. Yannick Bolasie         (DRC, Crystal Palace)
25. Yaya Toure               (Ivory Coast, Man City)

TUZO YA MWANASOKA BORA ANAYECHEZA AFRIKA
1.    Amr Gamal               (Misri, Al Ahly)
2.    Abdelrahman Fetori   (Libya, Ahly Benghazi)
3.    Bernard Parker         (Afrika Kusini, Kaizer Chiefs)
4.    Bongani Ndulula         (Afrika Kusini, Amazulu)
5.    Akram Djahnit           (Algeria, ES Setif)
6.    Ejike Uzoenyi             (Nigeria, Enugu Rangers)
7.    El Hedi Belamieri       (Algeria, ES Setif)
8.    Fakhereddine Ben Youssef   (Tunisia, CS Sfaxien)
9.    Ferdjani Sassi                    (Tunisia, CS Sfaxien)
10. Firmin Mubel Ndombe          (DRC, AS Vita)
11. Geoffrey Massa         (Uganda, Pretoria University)
12. Jean Kasusula                     (DRC, TP Mazembe)
13. Kader Bidimbou                  (Kongo, AC Leopards)
14. Lema Mabidi                       (DRC, As Vita)
15. Mudathir Al Taieb                (Sudan, Al Hilal)
16. Roger Assalé               (Ivory Coast, Sewe Sport)
17. Senzo Meyiwa (Afrika Kusini, Orlando Pirates)
18. Solomon Asante                 (Ghana, TP Mazembe)
19. Souleymane Moussa      (Cameroon, Coton Sport)
20. Yunus Sentamu                  (Uganda, AS Vita)

Breaking News! Mwanamuziki Khamis Amigolas afariki dunia

http://api.ning.com/files/dyEc5o4i5R40CVU*duc5GvfEdRdfsq*YNDQExCkCTTWwBhKlKRvwR7nmiRAkRIilv-ILlXQzgl*2lrXVs1ybGjHfMVry78iT/amigo2.jpg?width=450
Amigolas enzi za uhai wake
MWANAMUZIKI nyota wa zamani wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Khamis Kayumbu 'Amigolas'  amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Muimbaji huyo aliyekuwa bendi ya Ruvu Star, amekumbwa na mauti hayo baada ya kulazwa hospitalini hapo kwa tatizo la Moyo kwa siku kadhaa.
Muasisi huyo wa Twanga Pepeta na anayekumbukwa na utunzi mahiri wa wimbo wa Aminata, alilazwa hospitalini hapo wiki mbili zilizopita na alikuwa katika maandalizi ya kufanyiwa upasuaji juu ya tatizo lake.
Mpaka anafariki mkali huyo ndiye aliyekuwa kiongozi wa bendi ya Ruvu Star ambayo inatamba na nyimbo zake tatu za awali na walikuwa wakijiandaa kumalizia nyingine mbili kabla ya kzuindua albamu yao ya kwanza.
Kabla ya kuzipigia Twanga Pepeta na Ruvu Stars, marehemu Amigolas enzi za uhai wake alifanya kazi na bendi za Bicco Stars chini ya Kinguti System.
Msiba uko nyumbani kwa mama mzazi wa marehemu Mburahati jijini Dar es Salaam jirani kabisa na Shule ya Msingi Mianzini, na kwamba taratibu za mazishi zinasubiri ndugu na jamaa kutoka Tabora na Kigoma.