STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 26, 2013

RAIS KIKWETE ACHIMBA MKWARA MAJAMBAZI, WAHAMIAJI HARAMU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho ameamuru majambazi na wahamiaji haramu wote katika mikoa mitatu nchini kujisalimisha katika muda wa siku 14 kuanzia leo, Ijumaa, Julai 26, 2013 kabla ya kuanza kwa operesheni kubwa kuliko zote katika historia ya Tanzania nyenye lengo la kukomesha ujambazi katika mikoa hiyo na kukamata wahamiaji haramu.

Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu amesema kuwa leo ametoa amri kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama nchini kuanza maandalizii ya operesheni hiyo na hatimaye kuiendesha katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.

Majambazi wanateka magari, wanaua watu wetu, wanapora mali zao. Watanzania hawawezi kuendelea kuishi kwa hofu, woga na taabu katika nchi yao wenyewe. Tutawasaka majambazi misituni, tutawasaka majumbani, tutachimbua ardhini kutafuta hata silaha zilizofukiwa chini,” amesema Rais Kikwete.

Rais Kikwete ametoa amri hiyo mchana wa leo, Ijumaa, Julai 26, 2013 wakati alipohutubia wananchi wa mjini Biharamulo, Mkoani Kagera, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kagoma, Wilaya ya Muleba kwenda Lusahuga, Biharamulo.

Rais Kikwete ametoa amri hiyo kufuatia matukio ya mara kwa mara na yasiyokuwa na mwisho ya majambazi kuteka mabasi, kuua watu na kupora mali zadi katika mikoa hiyo, hali ambayo imesababisha malalamiko ya wakazi wa mikoa hiyo.

Rais Kikwete ameaambia wananchi: “Tumeamua kukomesha upuuzi huu katika mikoa ya Kagera, Kigoma Geita. Leo nimetoa maagizo kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama – Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Usalama wa Taifa kuandaa operesheni maalum, operesheni kubwa kuliko zote tokea tupate uhuru. Upuuzi huu hauwezi kuendelea.”

Ameongeza Rais Kikwete na kuwaambia wananchi: “Nawaamuru majambazi wote, wenye kumiliki silaha kinyume cha sheria na wahamiaji haramu wote wajisalimishe katika wiki mbili kuanzia leo. Wajisalimishe wao pamoja na silaha zao. Baada ya hapo, tunaanzisha operesheni ambayo haijapata kuonekana katika historia ya nchi yetu.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Sitanii, sina mzaha na hili. Nimechoka. Nalisema hili mchana, macho makavu. Nawaambia majambazi watafute kazi nyingine, kazi hii hailipi tena. Kwa wale majambazi na wahamiaji haramu kutoka nchi za jirani, waanze safari ya kurejea kwao.”

Rais Kikwete ameonya: “Na hata wale wanaoishi na kulea majambazi na wahamiaji haramu nao wajisalimishe. Na ole wao majambazi watakaojaribu kuwapiga risasi askari wetu. Watakiona cha mtema kuni.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

Uzinzi wamfikisha kiongozi CHADEMA kortini


RORYA,Tanzania
MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Rorya mkoani Mara ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Tai kupitia Chama hicho, Masirori Kyorang  amefikishwa Katika Mahakama ya Mwanzo Shirati kujibu mashitaka ya ugon Kwa mujibu wa kesi hiyo, Kyorang anadaiwa kushikwa ugoni na mke wa mlinzi wa Mbunge wa Jimbo la Rorya wakiwa gesti ya Triple Kabwana katika mji mdogo wa  Shirati, suiku wa kuamkia jana.

Akisomewa Mashitaka hayo  jana Julai 24, na Mwendesha Mashitaka wa Polisi mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Shirati Dock Nyatega , ambapo ilidaiwa kuwa mheshimiwa Masirori alikamatwa  mida ya saa 3 usiku, katika chumbani akiwa na mke wa mlinzi huyo wa Mbunge wa Jimbo la Rorya aliyejulikana kwa jina Pendo Omolo.

Mtuhumiwa Masirori alikana Mashitaka yake na kupata Dhamana hadi kesi yake itakapotajwa tena Julai  29 , ambapo Mke huyo Pendo amekwenda Nyumbanio kwao hadi Shauri hilo litakapoanza kusikilizwa na kubaini Ukweli wake baada ya Ushahidi kutolewa Mahakamani alisikika akisema Hakimu Nyatega .
 Habari hii imeandikwa na Samson Chacha, 0788312145, 0762219255

Arsenal njia nyeupe kumnasa Suarez ni baada ya Real kujiondoa kwenye mbio za kumwaniaKLABU ya Arsenal ipo katika nafasi nzuri ya kumnyakua mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez baada ya Real Madrid kujiondoa kwenye mbio za kumwania mchezaji huyo kutoka Uruguay.
Duru za michezo zilizonukuu chanzo kutoka ndani ya Santiago Bernabeu, zinasema kuwa bosi mpya wa Real Madrid, Carlo Ancelotti hana mpango wa kuongeza mshambuliaji mwingine baada ya kumuuza Gonzalo Higuain kwa Napoili ya Italia wiki hii.
Ancelotti anaamini kwamba silaha alizonazo katika safu yake ya mbele ikiongozwa na Cristiano Ronaldo na Karim Benzema inatosha kabisa kuua wapinzani wake.
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea pia anataka kuwapa nafasi makinda wanaoichezea timu ya taifa ya Hispania u21, Jese Rodriguez na Alvaro Morata ndiyo maana hana sababu ya kunyakua strika mwingine.
Chanzo hicho kilichonukuliwa na gazeti la michezo la Marca, kimesema " Tunaimani kubwa kwa Jese na Morata wataziba nafasi hiyo. Ni wazuri sana. Hatuna haja ya kusaini mshambuliaji mwingine mpya,"
Kwa maana hiyo ni kwamba njia ipo nyeupe wa Arsenal kumnyakua mchezaji huyo baada ya mbio za muda mrefu.

After Death ya kumuenzi Kanumba kutolewa hadharani Jumanne


FILAMU maalum kwa ajili ya kumuenzi marehemu Steven Kanumba iitwayo 'After Death' inatarajiwa kuachiwa rasmi mtaani kuanzia kesho.
Filamu hiyo iliyotungwa na Jacklyne Wolper na kuongozwa na Leah Richard 'Lamata' kama njia ya kuenzi kipaji na mchango wa marehemu Kanumba imeshirikisha wasanii kadhaa nyota waliowahi kufanya kazi na mkali huyo aliyefariki mwaka mmoja uliopita.
Akizungumza na MICHARAZO muda mfupi uliopita, Lamata alisema filamu hiyo iliyozinduliwa siku ya kumbukumbu ya kifo cha Kanumba Aprili 7 mwaka huu itaachiwa kesho Jumanne baada ya taratibu zote kukamilika kwa wasambazaji wao.
Alisema anaamini filamu hiyo itarejesha kumbukumbu za majonzi kwa mashabiki wa marehemu Kanumba, lakini pia watapata burudani baada ya kupita mwaka mmoja tangu wampoteze nyota huyo aliyekuwa akitamba kimataifa.
"Hayawi hayawi sasa yamekuwa, ile filamu ya kumuenzi marehemu Kanumba iliyochezwa na wakali karibu wote waliowahi kufanya kazi na mkali huyo iitwayo 'After Death' itaachiwa rasmi siku ya Jumanne ya Julai 30," alisema Lamata.
Lamata aliwataja baadhi ya wasanii waliocheza filamu hiyo ni pamoja na chipukizi walioibuliwa na Kanumba, Hanifa Daud 'Jenifer' na Othman Njaidi 'Patrick'.
Pia ndani yake wamo wakali kama Ruth Suka 'Mainda', Samsha Ford, Stanley Msungu, Patcho Mwamba, Ben Branco, Wolper, Irene Paul, Uncle D aliyeshabiana na marehemu Kanumba na wengineo.

Stars kushambulia mwanzo mwisho kesho, kaseja kukaa langoni Chuji, Bocco ndaniNa Boniface Wambura
MOJA ya mikakati ya Taifa Stars kwenye mechi ya kesho (Julai 27 mwaka huu) dhidi ya Uganda kuwania kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini ni kushambulia kwa muda mwingi wa mchezo.

Kocha Kim Poulsen amesema maandalizi ya Taifa Stars jijini Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo ambayo Uganda inaongoza kwa bao 1-0 yalikuwa mazuri, lakini mabao ni muhimu hivyo watashambulia bila kusahau kulinda lango lao.

“Unapocheza mechi za aina hii za nyumbani na ugenini, huku mwenyeji akiwa anaongoza mabao yana maana kubwa katika mechi. Mabao yanabadili mchezo na pia wachezaji kifikra,” amesema Kim akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Mt. Zion ambayo Stars imefikia.

Amesema katika mechi ya kwanza walitengeneza nafasi nyingi lakini hawakuzitumia, hivyo wamekuwa wakifanya mazoezi ya kushambulia, jinsi ya kutengeneza nafasi, na jinsi ya kumalizia.

“Hivyo tuko hapa (Kampala) kwa ajili ya kufunga, ni lazima tufunge ili tuweze kuendelea na mashindano. Lakini ngome yetu nayo ni lazima iwe makini ili kutoruhusu bao,” amesema Kim na kuongeza kuwa kikosi chake cha kwanza ni lazima kitakuwa mabadiliko kutoka na Mwinyi Kazimoto kuingia mitini na Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio Uholanzi.

Amesema angalau kutakuwa na mabadiliko kwa kuingiza sura mbili mpya katika kikosi cha kwanza, na kuongeza kuwa wachezaji wanafahamu umuhimu wa mechi hiyo kwani timu ikienda kwenye Fainali za CHAN itakuwa manufaa kwao binafsi.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefanya mazoezi ya mwisho leo jioni Uwanja wa Mandela ulioko Namboole ambao utatumika kwa ajili ya mechi hiyo kesho.

Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki na itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar wakiongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa mezani (fourth official). Kamishna wa mechi hiyo namba 38 ni Ismail Kamal kutoka Ethiopia.

Stars inatarajiwa kupangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Salum Abubakar, Frank Domayo, John Bocco, Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.

Hii ndiyo Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013-2014

http://1.bp.blogspot.com/-V9zsdzuy-tQ/Ue0Hn8wGHoI/AAAAAAAAVmg/BbN_62pW0d0/s1600/ratiba+vpl.JPG

Suarez ruksa kuteta na Arsenal, ila...!

http://i.telegraph.co.uk/multimedia/archive/02489/luis-suarez_2489623b.jpg
LONDON, Uingereza
LUIS Suarez ataruhusiwa kufanya mazungumzo na Arsenal baada ya klabu hiyo ya London kufikisha ofa ya paundi milioni 40 lakini Liverpool haiko tayari kumuuza mshambuliaji huyo hadi bei ya paundi milioni 50 itakapofikiwa.
Ofa iliyoweka rekodi ya Arsenal ya paundi milioni 40 jumlisha paundi moja ilikataliwa na Liverpool lakini Suarez sasa anataka kufanya mazungumzo na klabu hiyo ya London.
Ripoti nyingine zinasema mshambuliaji huyo amewaambia maafisa wa Liverpool kwamba anataka kujiunga na Arsenal na anajiandaa kuwasilisha barua ya kuomba kuondoka Anfield.
Ofa ya paundi milioni 40 inamaanisha kwamba kipengele cha kuvunjia mkataba wake kimefikiwa na hivyo ni lazima Liverpool imfahamishe kuhusu ofa hiyo na sasa yuko huru kuzungumza na Arsenal.
Arsenal wanajiandaa kumlipa Suarez mshahara wa paundi 150,000 (Sh. milioni 364) kwa wiki kwa mkataba wa miaka mitano.
Lakini Liverpool haiko tayari kumuuza hadi Arsenal watakapoongeza ofa yao.
Juzi Jumatano, Suarez aliichezea Liverpool kwa mara ya kwanza tangu tukio maarufu la kumng'ata mkononi beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic msimu uliopita, akiingia kutokea benchi katika dakika 18 za mwisho za mechi yao ya kirafiki waliyoshinda 2-0 dhidi ya Melbourne Victory kwenye Uwanja wa MCG.
Huku Liverpool ikiongoza kwa goli 1-0, Suarez alipika goli la pili la timu hiyo wakati alipomtengea mchezaji mpya Iago Aspas katika dakika za lala salama.
Baada ya mechi hiyo kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers alisema: "Hakuna kipya cha kueleza, yeye (Suarez) ni mchezaji wa Liverpool na ndani ya wiki chache zijazo tunahitaji kumrejeshea kasi yake."
Rodgers hata hivyo, alimkumbusha Suarez deni alilonalo kwa mashabiki wa Liverpool ambao walisimama upande wake kwa misimu miwili ambayo ametawaliwa na matukio ya utata.
"Sapoti aliyopata kutoka kwa mashabiki na watu wa mji wa Liverpool haipimiki," Rodgers aliongeza.
"Katika kipindi hicho alikosa mechi nyingi za timu kutokana na sababu mbalimbali. Watu walisimama upande wake kama mtoto wao na hakika walikuwa wakimtetea. Chochote kitakachotokea katika wiki zijazo jambo hilo litabaki akilini mwake kwa sababu ni mambo ambayo huwezi kuyasahau."
Liverpool sasa wamekataa ofa mbili kutoka Arsenal, ambao wamedhamiria kuimarisha safu yao ya ushambuliaji, wakati Real Madrid, ambao tayari wamemuuza Gonzalo Higuain kwa Napoli, bado pia wanamhitaji nyota huyo wa Uruguay licha ya kwamba hawajapeleka ofa yoyote.
Kufuatia ofa mpya ya Arsenal, mmiliki wa Liverpool, John Henry aliwakebehi katika ukurasa wake wa Twitter kwa kuandika: "Unadhani wanavuta/puliza nini kule Emirates?"
Haijawa wazi kama kama Henry anazungumzia majaribio ya Arsenal kutaka kumsajili Suarez au kiasi cha ofa wanazotuma.
Wakati Liverpool wanadhamiria kumbakisha Suarez, ambaye alifunga magoli 30 katika mechi 44 za klabu hiyo msimu uliopita, ugumu wao unatarajiwa kulegea kama kama ofa hiyo itazidi kuongezwa. Kama ofa ya Arsenal itakubaliwa, itakuwa ni zaidi ya mara mbili ya kiwango cha juu cha pesa walichotoa kumnunua mchezaji.
Arsenal, ambao ofa yao ya kwanza kwa Suarez ilikuwa ni paundi milioni 30, walilipa paundi milioni 17.5 kumnunua winga wa Sevilla, Jose Antonio Reyes mwaka 2004.
Suarez anataka kuondoka Anfield ili akacheze soka la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya licha ya kwamba alisaini kurefusha mkataba wake Liverpool mwaka jana tu.
Uvumi ulianza kukua kuhusu hatma ya Suarez tangu alipofungiwa mechi 10 mwishoni mwa Aprili kwa kumng'ata Ivanovic.
Mshambuliaji huyo amebakisha mechi sita za kutumikia katika kifungo chake na pia alifungiwa mwaka 2011 baada ya kukutwa na hatia ya kumfanyia vitendo vya kibaguzi beki wa Manchester United, Patrice Evra.
Suarez alijiunga na Liverpool akitokea Ajax Januari 2011 kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 22.7.
Wachezaji walionunuliwa na Arsenal kwa pesa nyingi zaidi ni Jose Antonio Reyes (paundi milioni 17.5 kutoka Sevilla), Santi Cazorla (paundi milioni 16, Malaga), Andrey Arshavin (paundi milioni 15, Zenit St Petersburg), Sylvain Wiltord (paundi milioni 13, Bordeaux) na Thierry Henry (paundi milioni 11, Juventus).

Simba, Coastal kuvaana Mkwakwani J2


TIMU ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam inatarajiwa kuvaana na 'ndugu' zao, Coastal Union ya Tanga katika pambano la kirafiki na kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Agosti 24 litakalochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani siku ya Jumapili.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema lengo la mechi hiyo ni pamoja na kuwaandaa wachezaji wao kabla ya kuanza kampeni ya kuwania kurejesha taji lao walilolipoteza kwa mahasimu wa jadi, Yanga.
Alisema mechi hiyo itatoa nafasi kwa mashabiki wa Simba waliopo jijini Tanga kuwafahamu wachezaji wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu mpya.
Alisema mara baada ya mechi hiyo wachezaji wa Simba watarejea jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi nyingine dhidi ya timu ya Kombaini ya Majeshi itakayopigwa Agosti 3 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Coastal itavaana na Simba ikiwa na kumbukumbu ya kuinyuka URA kwa bao 1-0, huku Simba ikiwa inauguza kipigo toka kwa Wakusanya ushuru hao wa Uganda waliowadungua mabao 2-1.

Tanzania yaanza vibaya michuano ya Wavu Uganda


Athuman Rupia (kulia) akiwa na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya wavu
TIMU ya taifa ya mchezo wa Wavu ya Wanaume ya Tanzania jana ilianza vibaya michuano ya Kanda ya Tano kuwania kufuzu fainali za kimataifa za mchezo huo FIVB World Cup 2014 zitakazofanyika Poland baada ya kutandikwa na Wakenya kwa seti 3-0.
Michuano hiyo ya Kanda ya Tano Afrika, inafanyika nchini Uganda kwenye uwanja wa MTN Sports uliopo Lugogo jijini Kampala ikishirikisha timu nne wakiwamo wenyeji Uganda.
Kwa mujibu wa mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, Athuman Rupia aliyezungumza na MICHARAZO kwa njia ya simu asubuhi hii kutoka Uganda, ni kwamba Tanzania ilishindwa kufuruka kwa Wakenya kutokana na hali ya uchovu waliokuwa nao baada ya kutua nchini humo majira ya asubuhi na jioni kushuka dimbani.
"Tumeanza vibaya michuano ya Kanda ya Tano kuwania Fainali za Kombe la Dunia baada ya kufungwa sti 3-0 na Wakenya, ila tunaamini uchovu umechangia kipigo chetu na tunajipanga kwa mechi zilizosalia dhidi ya Burundi na wenyeji Uganda," alisema Rupia anayeichezea pia timu ya Jeshi Stars.
Jumla ya timu za taifa za nchi nne tu kati ya sita zilizotarajiwa kushiriki michuano hiyo ndizo zinazochuana jiji Kampala baada ya  wakali kutoka Sudan na Rwanda kujioengua dakika za lala salama na kuziacha Kenya, Uganda, Tanzania na Burundi zikionyeshana kazi kuwania nafasi tatu za Kanda hiyo ya Tano.