http://4.bp.blogspot.com/_Z6ESZURCdgs/TKYOV33uDFI/AAAAAAAACYk/Q2PlYgl6LRQ/s1600/mlume.JPG
Mussa Mgosi baada ya pambano la Simba na Yanga alipokuwa Simba
MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa timu za Simba na Taifa Stars, Mussa Hassani Mgosi anayeichezea kwa sasa JKT Ruvu, amesema yupo tayari kutua katika timu yoyote itakayomhitaji kwa msimui ujao hata kama ni Simba au Yanga, mradi aridhishwe na masilahi atakayoafikiana na klabu husika.
Aidha mshambuliaji huyo amesema amefurahi mno kuweza kuisaidia JKT Ruvu kunusurika kushuka daraja, licha ya kukiri klabu huyo haikuwa na msimu msimu safari hii kwa namna ilivyoyumba na kupoteza makali iliyokuwa nayo kwa misimu kadhaa ya nyuma.
Akizungumza na MICHARAZO mapema leo, Mgosi aliyewahi kucheza soka la kulipwa katika klabu ya D Motema Pembe ya DR Congo, alisema kwa vile mkataba wake wa mwaka mmoja na JKT Ruvu unaisha baada ya msimu huu kumalizika yupo huru kutua klabu yoyote itakayokuwa ikimtaka.
Mgosi, alisema hatajali ni timu gani inayomtaka kwa msimu ujao, mradi wakubaliane kimasilahi kwa kuwa yeye ni mwanasoka na ajira yake inategemea mchezo huo hivyo atakuwa tayari kutua kokote.
Aliongeza, hata kama JKT Ruvu itakuwa ikimhitaji kusalia katika timu hiyo hatakuwa na pingamizi kwa vile ni moja ya timu anayoipenda na alishawahi kuichezea siku za nyuma kabla ya kurejea safari hii na kuitumikia kwa duru la pili na kushukuru kuisaidia kuiokoa isishule daraja.
"Niko tayari kutua kokote kwa msimu ujao, sitabagua timu hata kama ni Mbeya City, Ashanti Utd, Simba au Yanga muhimu masilahi yaniridhishe," alisema.
Mfungaji Bora huyo wa zamani wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na michuano maalum iliyofanyika China mwaka jana, alikiri ligi ya msimu huu ilikuwa ngumu na isiyotabirika japo anasikitika vibali kumkwamisha kuishiriki tangu duru la kwanza baada ya kurejea toka Kongo.