STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, June 17, 2014

Thomas Muller awafunika wakali wengine Brazil

WAKATI Climt  Dempsey wa Marekani akiweka rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi mpaka sasa kwenye Kombe la Dunia likikamata nafasi ya tano tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 1930, Mjerumani Thomas Muller amewafunika wakali wengine kwa kuongoza orodha ya ufungaji mpaka sasa.
Muller anaongoza msimamo akiwa na mabao matatu aliyioyapata jana wakati wakiiangamiza Ureno kwa mabao 4-0 na kuwazidi Robin Van Persie, Karim Benzema na Arjen Robben, Neymar waliokuwa wakiongoza na mabao mawili kila mmoja wakati raundi ya kwanza ikitarajiwa kumalizka leo kabla ya timu nyingine kuanza ngwe ya pili ya makundi.
Muller alifunga mabao hayo katika pambano la kundi la kifoi ambalo lilishuhudia Mmarekani Clint Dempsey akifunga bao la mapema zaidi katika michuano ya mwaka huu ya nchini Brazili katika sekunde ya 29 tu na kukamata nafasi ya tano katika goli la mapema lililowahi kufungwa kwa muda wote wa michuano hiyo ya Kombe la Dunia.
Bao la Mmarekani huyo limepitwa na yale ya Hakan Sukur linaloongoza likiwa lifungwa Sekunde ya 11 katika michuano ya mwaka 2002, Vaclav Masek aliyefungwa sekunde ya 16 kwenye michuano ya mwaka 1962, Ernst Lehner la sekunde ya 25 kwenye michuano ya mwaka 1934 na lile la Brayan Robson la sekunde ya 27 michuano ya mwaka 1982.
Orodha ya mabao ya mapema katika Kombe la Dunia ni kama ifuatavyo;
Hakan Sukur (2002) Sekunde 11
Vaclav Masek (1962) Sekunde 16
Ernst Lehner (1934) Sekunde 25
Brayan Robson (1982) Sekunde 27
Clint Dempsey (2014) Sekunde 29
Bernard Lacombe (1978) Sekunde 30
Emile Veinante (1938) Sekunde 35
Arne Nyberg (1938) Sekunde 35
Florian Albert (1962) Sekunde 50
Adalbert Desu (1930) Sekunde 50

Chini ni Orodha ya wafungaji wanaoongoza kwa sasa katika michuano ya Brazil;
3- Thomas Müller (Germany)
2- Karim Benzema (France)
    Neymar (Brazil)
    Arjen Robben (Netherlands)
    Robin van Persie (Netherlands)
1- Lionel Messi (Argentina)
    Xabi Alonso (Spain)   
    P. Armero (Colombia)
    Mario Balotelli (Italy)       
    J. Beausejour (Chile)
   Winfried  Bony (Côte d'Ivoire)
   Gervinho (Cote d'Ivoire)
   T. Cahill (Australia)
   J. Campbell (Costa Rica)
   Edinson Cavani (Uruguay)
   S. de Vrij (Netherlands)
   Andre Ayew (Ghana)
   Clint Dempsey (USA)
   John Brooks (USA)
  Mats Hummels (Germany)

Shaaban Kisiga aibeba Morning Star

Na Adam Fungamwango
KIUNGO mchezeshaji wa Mtibwa Sugar Shaabani Kisiga, juzi aliipeleka robo fainali ya Wadau Cup timu yake ya Morning Star ya Kiwalani alipofunga bao moja na kutengeneza lingine, ilipoifunga Mwananyamala Veterani mabao 2-0.
Mechi hiyo kali ilifanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Mwananyamala ambako michuano hiyo inafanyika.
Kisiga ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Simba na SC Villa ya Uganda, alifunga bao kwenye dakika ya 75 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Zokora Nyambiso.
Bao hilo liliamsha mayowe kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya kulisubiri kwa muda mrefu, kwani timu yao ilihitaji ushindi tu ili iweze kusonga mbele.
Mshambuliaji wa Ruvu Shooting Paul Ndauka aliikosesha bao Morning Star katika dakika ya 80 baada ya kupiga shuti lililopaa akibaki yeye na kipa Hamza Zongera wa Mwananyamala Veterani.
Kisiga akiwa katikati ya uwanja alitoa pasi ndefu kwa Nyeje Mussa ambaye hakufanya makosa na kuukwamisha mpira wavuni kwenye dakika ya 88, akiihakikishia timu yake ushindi.
Mbali na Morning Star, timu nyingine zilizofanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ni Mbogamboga FC, Sharobaro FC na African People zote za Mwananyamala, Kijitonyama Chipukizi, Generation ya Kinondoni.

Ruvu Star kusambaza Spirit videoni

Rogert Hegga
BENDI ya Ruvu Star imekamilisha kurekodi video zao mbili za nyimbo za 'Spirit' na 'Jua Kali' na wanatarjiwa kuanza kusambaza wiki hii ili kuwapa burudani mashabiki wa muziki wa dansi nchini.
Nyimbo hizo zilizorekodiwa video hizo ni kati ya tatu zinazoendelea kutamba kwenye vituo vya redio, wimbo mwingine ukifahamika kwa jina la 'Network Love' ambao video yake imewekwa kiporo kwa sasa.
Akizungumza na MICHARAZO mmoja wa viongozi wa Ruvu, Roger Hegga alisema nyimbo hizo zitasambazwa kuanzia kesho kabla ya bendi yao kuingia tena studio kumaliza kurekodi nyimbo tatu za mwisho za kukamilisha albamu yao ya kwanza.
Hegga alisema walipanga kuingia studio wiki hii, lakini wamesitisha zoezi hilo kupisha maandalizi ya onyesho maalum la 'Usiku wa Mwana Dar es Salaam' litakalofanyika siku ya Jumamosi, jijini Dar.
"Baadhi ya wanamuziki wa Ruvu ni wale walioshiriki albamu ya Mwana Dar es Salaam ya African Stars 'Twanga Pepeta'. hivyo kwa sasa wanamuziki hao tupo katika mazoezi ya onyesho hilo," alisema.
Alisema baada ya onyesho hilo la 'Usiku wa Mwana Dar es Salaam' wanamuziki wa Ruvu watarejea kwenye bendi yao na kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuingia studio kurekodi nyimbo hizo.
Hegga, mtunzi na muimbaji nyota nchini alizitaja nyimbo hizo za mwisho za kukamilisha albamu yao ni 'Koo' uliotungwa na Khamis Kanyumbu 'Amigolas', 'Chewa Original'-Suleiman Muhumba na 'Facebook' cha mpapasa kinanda Victor Mkambi.

Taifa Stars kuinolea makali Mamba nchini Botswana

KIKOSI cha tmu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kinatarajiwa kuondoka nchini wiki ijayo kwenda Botswana kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na mchezo dhidi ya Msumbiji kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Morocco.
Wachezaji wote wa Taifa Stars waliruhusiwa kurejea makwao baada ya kuingia kambini juni 11 kwa ajili ya kujiandaa na safari hiyo na watakutana tena kesho.
Stars inayofundishwa na Mholanzi, Mart Nooij itaondoka nchini Juni 27 kwenda Gaborone, ambako itaweka kambi ya mazoezi hadi Julai 7 itakaporejea nchini.
Taifa Stars itamenyana na Msumbiji ‘Mambas’ katika hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco baada ya kuitoa Zimbabwe juzi kwa jumla ya mabao 3-2, ikianza kwa ushindi wa 1-0  nyumbani na kumaliza kwa sare ya 2-2 juzi mjini hapa.
Mechi yake kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Julai 19 na 20 mwaka huu, wakati mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu.
Stars pia inatarajiwa kuwa na mchezo wa kujipima nguvu na Uganda kabla ya kumenyana na Msumbiji.

Dk Ndumbaro amdindia Malinzi, 'amchinja' tena Wambura

Dk Ndumbaro
KAMATI  ya Uchaguzi ya Simba imemuondoa kwa mara nyingine Michael Wambura kutokana na kufanya kampeni kabla ya wakati huku akiwa ameonywa.
Pia imesisitiza uchaguzi utafanyika Juni 29 kama ilivyopangwa kwa kuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliyetangaza kuusimamisha, hana mamlaka hayo kikatiba.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, mwanasheria na wakili maarufu nchini, Dokta Damas Daniel Ndumbaro 'DDN' ndiye amefunga na kusema hayo.
Ndumbaro amemwaga ripoti kamili ambayo inachambua mambo yote huku ikionyesha kiasi gani Malinzi hana haki ya kusitisha uchaguzi huo kama alivyotangaza jana.
IFUATAYO NDIYO RIPOTI KAMILI YA DAKTARI HUYO WA SHERIA NCHINI:
Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, ilifanya mkutano wake kawaida tarehe 15 Juni 2014 kujadili mambo mbalimbali ambayo yanayohusu uchaguzi mkuu wa Simba Sports Club ambao umepangwa kufanyika tarehe tarehe 29 Juni 2014. Kamati ya Uchaguzi ya Simba sports Club inapenda kuujulisha umma, hususan wapenzi wa Simba Sports Club mambo yafuatayo:

1. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, kwa mujibu wa Ibara ya 10(6) ya Kanuni za uchaguzi za TFF toleo la mwaka 2013, ndiyo chombo pekee chenye mamlaka ya kutangaza, kubadilisha, kusimamisha au kufuta tarehe ya Uchaguzi ya Simba Sports Club. Kwakuwa Kamati haijafanya hivyo, wala hakuna mdau yoyote aliyeleta hoja ya kusimamisha uchaguzi, tunawajulisha kuwa uchaguzi wa Simba Sports Club upo pale pale kama ambayo Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilivyopanga. Maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vema na Uchaguzi utafanyika tarehe 29 Juni 2014 kama ilivyopangwa hapo awali.
2. Kamati imesikia kupitia vyombo vya habari kuwa TFF imesimamisha uchaguzi wa Simba Sports Club mpaka hapo Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club itakapoteua Kamati ya Maadili. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club inapenda kusema yafuatayo:
i. Mamlaka ya kusimamisha uchaguzi ni kazi ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kwa mujibu wa ibara 10 (6) ya Kanuni za Uchaguzi, 2013
ii. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilipoanza mchakato wa uchaguzi ilitoa tamko kuwa: “kwasababu Simba Sports Club haina kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Rufaa ya uchaguzi, wala Kamati za Maadili kwa mujibu wa ibara za 16 (e) na (f) ya Katiba ya Simba Mwaka 2014, vyombo husika vya TFF vitatumika”. Kulikuwa hakuna pingamizi toka kwa mtu yoyote juu ya kauli hiyo, ikiwemo TFF.
iii. Tarehe 26 Mei 2013, Rais wa TFF aliialika Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club katika chakula cha mchana. Katika mkutano huo, kauli ya aya (ii) hapo juu ilirejewa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilikabidhi rasmi mchakato mzima wa uchaguzi na kutoa ufafanuzi kuwa kamati husika za TFF zitahusika, jambo ambalo halikupingwa na TFF.
iv. TFF iliruhusu Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF kusikiliza Rufaa za uchaguzi za Simba, hivyo basi haiwezi kuzuia Kamati zake nyingine kusikiliza Masuala ya kimaadili. “Estopel” inawazuia TFF kufanya hivyo sasa.
v. Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club, isipokuwa watatu tu, ni wagombea katika uchaguzi huu. Na hao watoto tayari wapo kwenye Kambi za Kampeni za uchaguzi hii ambazo zipo bayana kabisa. Kuiagiza Kamati ya Utendaji ya Simba iunde Kamati ya Maadili kusikiliza kesi za maadili dhidi yao wenyewe ni kukiuka msingi wa haki ya asili (natural justice). Ni dhahiri kuwa haki haiwezi kutendeka kwa wajumbe wa kamati ya utendaji ya Simba Sports Sports Club, ambao ni watuhumiwa katika masuala ya maadili, wachague majaji wa kuwahukumu. Hapo haki haitatendeka.
Ifahamike kuwa, baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club kuteua Kamati ya uchaguzi ya Simba Sports Club, Kamati hiyo haina mamlaka tena ya kujadili, kuingilia au kuteua chombo kingine kufanya shughuli zinazohusu uchaguzi ukizingatia kuwa wajumbe wake ni wagombea.
vi. Katika Uchaguzi Mkuu wa TFF wa Mwaka 2013, ambao ulimuingiza Jamal Malinzi Madarakani, FIFA walikuja, wakongea na pande zote na hatimaye, walisema kuwa; “tunapendekeza kuwa uchaguzi mkuu usimame ili kuunda kamati mbalimbali”. Mapendekezo hayo yalipokelewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Bw. Deo Lyato, na hatimaye ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF ndio iliyotangaza kusimamisha Uchaguzi na sio Sepp Blatter.
vii. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ni Kamati huru ambayo haipaswi kuingiliwa na Chombo chochote kile. Ili kulinda uhuru huo, tunalazimika kukanusha matamshi ya TFF kuhusu kusitisha Uchaguzi Mkuu wa Simba Sports Club. 
3. Malalamiko ya Kimaadili Kupelekwa FIFA.
Kwa mujibu wa Ibara ya 11 (9) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, 2013, inatoa mamlaka kwa Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kupeleka masuala ya maadili katika kamati ya maadili ya TFF. Tarehe 9 Juni 2014, Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilipeleka Masuala ya Maadili katika Kamati ya Maadili ya TFF. Kwakuwa TFF imekataa kusikiliza masuala ya maadili ambayo yanakiuka Kanuni za maadili, Katiba za Simba, TFF na FIFA, Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, itapeleka Masuala ya Maadili FIFA ili haki itendeke.
4. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilijadili kuhusu vitendo vya wagombea kupiga kampeni kabla ya muda wa kampeni ulioruhusiwa. Kwa mujibu wa Mchakato wa Uchaguzi ya Simba Sports Club, muda wa kampeni unaanza tarehe 24 -28 Juni 2014. Hapo awali kamati ilibaini kuwa wagombea wawili wa nafasi ya urais; Michael Richard Wambura na Evans Aveva walifanya vitendo vya kampeni siku ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea. Tarehe 25 Mei 2014, Kamati iliwapa ONYO KALI la maandishi wagombea hao na kuwataarifu kuwa hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kuondolewa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi. 
Baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kumuondoa Bw. Michael Richard Wambura katika kinyang’anyiro cha uchaguzi Mkuu wa SImba Sports Club, Bw. Wambura aliitisha Mkutano na waandishi wa habari, aliitukana Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, na kutoa matamshi ambayo ni Kampeni.
Baadaya ya Kamati ya Rufaa ya uchaguzi ya TFF kumrejesha Bw. Wambura katika Kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Simba, Bw. Wambura aliitisha tena mkutano wa waandishi wa habari, aliisifu kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF, kwa mara kwanza aliisifu Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club na kutoa matamshi ambayo ni wazi kuwa ni kampeni. Baadhi ya Matamshi aliyoyatoa kupitia vyombo vya habari ni kama ifuatavyo:
i. “Simba Sports Club inahitaji zaidi wadhamini na sio wafadhili”
ii. “Wafadhili kazi yao in kutoa fedha mfuko wa kushoto na kuepeleka mfuko wa kulia”
iii. “Simba ilikuwa na viwanja vitatu lakini kimoja kimeuzwa na wajanja na vimebaki viwili tu”
Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilitafakari matamshi hayo, na kubaini kuwa hiyo ni kampeni ya waziwazi wakati muda wa kampeni bado haujaanza.
Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ililipa jambo ili uzito wa kipekee kwasababu Mkosaji amekuwa na tabia ya kurudia kosa hilo hata baada ya kupewe onyo la maandishi.
HIVYO BASI: Kwa mujibu wa mamlaka ya kikanuni, hususan Ibara za: 6 (1) (a) – (g); 6 (1) (L) na 14(3) za Kanuni za uchaguzi za TFF – 2013, Bw. Michael Richard Wambura anaondolewa Katika Kinyang’anyiro cha Uchaguzi wa Simba Sports Club, 2013, kwa kosa la kurudia kufanya kampeni kabla ya muda wa kampeni ambao umepengwa."

Ratiba ya Kombe la Dunia ipo hivi

  
LEO Juni 17, 2014
16. Ubelgiji     v    Algeria        Saa 1:00 Usiku  
17. Brazil    v    Mexico        Saa 4:00 Usiku  
18. Urusi    v    Korea        Saa 6:59 Usiku      

KESHO Juni 18, 2014
20.Australia    v Uholanzi        Saa 1:00 Usiku
19. Hispania v    Chile            Saa 4:00 Usiku
18. Cameroon    v    Croatia        Saa 6:59 Usiku      

Alhamisi Juni 19, 2014

21.Colombia    v    Ivory Coast     Saa 1:00 Usiku  
23.Uruguay    v    England     Saa 4:00 Usiku
22.Japan    v    Ugiriki         Saa 6:59 Usiku    

Riyana, Slim wapiga mzigo Zenji


STAA wa filamu nchini, Riyama Ally na Slim Omary 'Kiwi' wapo Zanzibar kwa ajili ya kutengeneza filamu iitwayo 'Dhana' wakishirikiana na wasanii wa visiwani humo.
Akizungumza na MICHARAZO juzi, Kiwi alisema sehemu kubwa ya filamu hiyo imekamilika na walikuwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam kuendelea na majukumu yao mengine.
Kiwi alisema mbali na yeye na Riyama filamu hiyo imechezwa pia na msanii maarufu visiwani humo aitwaye Eddy na wakali wengine za Zanzibar na ni 'bonge' la mseto.
"Tupo visiwani kumaliza kushiriki filamu mpya iliyozalishwa visiwani humu iitwayo 'Dhana' ni bonge la filamu kwani kisa chake kina mafunzo makubwa kwa jamii," alisema.
Kiwi alisema simulizi ya filamu hiyo linamhusu mtu mmoja ambaye anamjengea dhana mbaya mkewe kumfanyia usaliti na kuamua kulipa kisasi ambacho kinakuwa majutoa kwake.
"Hii siyo ya kuikosa kwa sababu mikasa kama hii imekuwa ikizikumba nyumba nyingi na watu kuwekeana kinyongo kwa dhana tu, bila ya uhakika wa jambo analodhania," alisema.
Msanii huyo anayetamba

Ghana yafa kiume, Nigeria yabanwa na Iran, Ujerumani dah!

Ronaldo alijitahidi mbele ya Ujeruman, lakini jahazi lao lilizama mara 4
Vita ya Nigeria na Iran ilikuwa hivi
Dempsey akishangilia bao lake dhidi ya Ghana
WAKATI Ujerumani ikitoa onyo katika Fainali za Kombe la Dunia kwa kuigagadua Ureno kwa mabao 4-0 timu za Afrika zimeendelea kuchechemea.
Ghana ilijikuta ikifa kiume mbele ya Marekani kwa kucharazwa mabao 2-1, huku wawakilishi Nigeria wakibanwa mbavu na Iran katika mchezo mwingine.
Ujeruman waliopo kundi G waliitoa nishai Ureno ikiwa na nyota wa dunia, Cristiano Ronaldo kwa kuilaza mabao 4-0 huku beki wake 'mapepe' Pepe alilimwa kadi nyekundu.
Mabao ya Thomas Muller aliyefunga 'hat trick' na jingine la Mats Hummels yalitosha kuiangamiza Ureno katika pambano la kwanza la timu hizo lililochezwa saa 1 usiku.
Baadaye saa nne Nigeria ikisakata kandanda murua ilishindwa kupata ushindi mbele ya Iran iliyotumia muda mrefu kupaki basi na kushambulia kwa pamoja.
Manane ya usiku Ghana walikuwa dimbani kukamilisha ratriba ya mechi za kwanza za kundi G kwa kuvana na Marekani na kujikuta wakilazwa mabao 2-1.
Bao la mapema la Clint Dempsey kwenye sekundi ya 31 na jingine la dakika ya 86 kupitia kwa John Brooks yalitosha kuzima ndoto za Ghana kuambulia sare.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Fulham, aliifungia Marekani inayonolewa na kocha Jurgen Klinsmann alifunga bao hilo dakika nne baada ya Ghana kuchomoa bao kupitia kwa Andre Ayew.
Michuano hiyo itaendelea tena leo kwa michezo mitatu, Algeria wataumana na Ubelgiji, huku Brazil wenyeji wa michuano hiyo watacheza mchezo wao wa pili dhidi ya Mexico na Urusi kupepetana na Korea.

Kalidjo Kitokololo atua Mashujaa Band, uongozi watamba

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bendi ya Mashujaa Bw. Maximillian Luhanga akizungumza katika mkutano huo wakati alipomtambulisha rapa Kitokololo kushoto kutoka bendi ya FM Academia kulia ni King Dodoo mshauri wa bendi hiyo.
Kitkololo akitangaza rasmi kujiunga na bendi ya Mashujaa leo kulia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano Bw. Maximillian Luhanga.
BENDI ya Mashujaa imemchukua rapa, Kalidjo Kitokololo ‘Kuku’ kutoka bendi ya FM Academia na kusaini naye Mkataba wa miaka miwili.
Akizungumza kwenye ukumbi wa Milenium Business Park leo , Kijitonyama, Dar es Salaam Mkurugenzi wa Mawasiliano wa bendi hiyo, Maximillian Luhanga amesema kupatikana kwa Chitokololo ni furaha kubwa kwao. 
“Kalidjo anakuwa rapa wa tatu katika bendi ya Mashujaa , baada ya Saulo John maaurufu Ferguson na Sauti ya Radi, ambao wote ni wakali, kwa marapa hao wote tunaamini bendi yetu itakuwa inatisha sana,” amesema Luhanga. 
Maxmilian Luhanga amesema Kitokololo anaanza kazi mara moja baada ya kusaini mkataba mpya.
Kwa upande wake, Kitokololo mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) amesema amekuja Tanzania kutafuta maisha na Mashujaa imempa ofa nzuri ndiyo maana amejiunga na bendi hiyo.
Amesema ameondoka vizuri FM Academia akiwa amewaaga vizuri wenzake ambao wameridhia kuondoka kwake.
Kitokololo amesema kwamba amejiunga na Mashujaa akimfuata King Dodo ambaye kimuziki ni baba yake , King Dodoo ndiye aliyemleta nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2004.
Mashujaa itamtambulisha rasmi mwanamuziki huyo katika onyesho maalum litakalofanyika ukumbi wa Letasi Lounge Ijumaa wiki hii. Mashujaa pia wanatarajiwa kuwa na ratiba ndefu mara baada ya mfungo mtukufu wa ramadhani ambapo Maximillian Luhanga amewaambia mashabiki wa bendi hiyo nchini kote kukaa mkao wa kula, Kwakuwa bendi hiyo itakuwa na ziara karibu mikoa yote ya Tanzania ili kutoa burudani kwa mashabiki wao.