KIKOSI cha tmu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kinatarajiwa kuondoka nchini
wiki ijayo kwenda Botswana kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na
mchezo dhidi ya Msumbiji kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania
tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Morocco.
Wachezaji wote wa Taifa Stars waliruhusiwa kurejea makwao baada ya
kuingia kambini juni 11 kwa ajili ya kujiandaa na safari hiyo na
watakutana tena kesho.
Stars inayofundishwa na Mholanzi, Mart Nooij itaondoka nchini Juni 27
kwenda Gaborone, ambako itaweka kambi ya mazoezi hadi Julai 7
itakaporejea nchini.
Taifa Stars itamenyana na Msumbiji ‘Mambas’ katika hatua ya mwisho ya
mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco baada ya kuitoa
Zimbabwe juzi kwa jumla ya mabao 3-2, ikianza kwa ushindi wa 1-0
nyumbani na kumaliza kwa sare ya 2-2 juzi mjini hapa.
Mechi yake kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya
Julai 19 na 20 mwaka huu, wakati mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji
kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu.
Stars pia inatarajiwa kuwa na mchezo wa kujipima nguvu na Uganda kabla ya kumenyana na Msumbiji.
No comments:
Post a Comment