STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, September 24, 2012

Vincent Barnabas akiri ligi ngumu msimu huu

Vincent Barnabas (kushoto) akiwa dimbani na timu ya taifa , Taifa Stars

WINGA machachari wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar, Vincent Barnabas amesema matokeo ya mechi za awali za Ligi Kuu Tanzania Bara zimeonyesha jinsi gani msimu huu utakuwa na ligi ngumu isiyotabirika kirahisi.
Aidha nyota huyo aliyewahi kutamba na timu za Kagera Sugar, Yanga na African Lyon, ameitabiria klabu yake ya Mtibwa Sugar kufanya vema tofauti na msimu uliopita ilipomaliza ikiwa nafasi ya nne.
Akizungumza na MICHARAZO, Barnabas, alisema kwa mechi za raundi tatu zilizokwisha kucheza mpaka sasa inaonyesha wazi ligi ya msimu huu sio nyepesi kama watu walivyokuwa wakiifikiria.
Nyota huyo alisema kutokana na mwenendo wa ligi hiyo, ni vigumu kutabiri mapema nani anayeweza kuwa bingwa kwa vile ligi bado haijatulia.
"Sio siri msimu huu ligi imeanza kuonyesha ni ngumu kwa aina ya matokeo yaliyopatikana, naamini ugumu huu umetokana na klabu zote kujipanga vema na kusaidia kuongeza ushindani," alisema.
Juu ya Mtibwa ambayo ilianza kwa sare dhidi ya Polisi Moro kabla ya kuilaza Yanga mabao 3-0 na kuzimwa na Azam mwishoni mwa wiki kwa bao 1-0, winga huyo alisema anaamini itafanya vema msimu huu tofauti na ligi iliyopita.
"Kwa namna tulivyo, naamini tutafanya vema, licha ya ugumu unaoonekana kwenye ligi ya msimu huu, wachezaji tumejipanga kuipigania timu ili imalize msimu tukiwa katika nafasi bora zaidi ya msimu uliopita," alisema Barnabas.
Kwa matokeo ya mwishoni mwa wiki, Mtibwa imejikuta ikiachwa nafasi ya sita ya msimamo ikiwa na pointi nne sawa na ndugu zao za Kagera Sugar na Yanga iliyozinduka kwa kuilaza JKT Ruvu mabao 4-1, ikizizidi uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Mwisho

Mashali, Sebyala kumkumuka Mwl Nyerere kwa masumbwi Dar

Med Sebyala wa Uganda akiwa na taji lake la ubingwa wa Uganda
Thomas Mashali wa Tanzania akiwa na ubingwa wake wa TPBO


BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Thomas Mashali anatarajia kuzidunda na Mganda Med Sebyala katika pambano la kuwania taji la Afrika Mashariki siku ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Pambano hilo la uzati wa kati la raundi 10 limepangwa kufanyika Oktoba 14 kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese Dar es Salaam.
Mratibu wa pambano hilo litakalosimamiwa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBO, Regina Gwae alisema tayari wameshamalizana na mabondia hao kwa ajili ya pambano hilo la kimataifa.
Regina, alisema pambano hilo ni fursa nzuri kwa Mashali anayeshikilia ubingwa wa Taifa wa TPBO kujitangaza kimataifa iwapo atafanikiwa kumnyuka Sebyala.
“Huwezi kwenda nje kama ndani hufanyi vizuri na huwezi kwenda Ulaya, iwapo unashindwa kutamba  Afrika Mashariki, hivyo tumeona tumpe Mashali mchezo huu ili akifanya vyema aweze kuvuka mipaka ya sasa, "alisema Regina.
Regina alisema ana matumaini mpambano huo utakuwa mzuri na utakaovutia kutokana na ukweli mabondia wote wawili wana sifa zinazofanana waking'ara ndani ya nchi zao.
Alisema Sebyala ni mmoja wa bondia wazuri waliowasumbua baadhi ya nyota wa ngumi nchini kama Rashid Matumla na Francis Cheka aliowahi kuja kucheza nao hapa nchi  katika mechi za zisizo za ubingwa.
Mratibu huto aliwaomba wafadhili wajitokeze kwa ajili ya kudhamini mchezo huo unatarajiwa kuwa na mapambano ya utangulizi.

Mwisho

Maugo kuwania ubingwa wa WBF Arusha

Bondia Mada Maugo

BONDIA nyota wa ngumi za kulipwa nchini, Mada Maugo anatarajiwa kupanda ulingoni mjini Arusha kuzichapa na Mustapha Katende kutoka Uganda katika pambano la kuwania ubingwa wa Mabara wa WBF.
Pambano hilo la uzani wa Super Middle la raundi 12 litafanyika Oktoba 28 kwenye ukumbi wa Triple A, jijini humo na kusindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi pamoja na burudani ya muziki wa kizazi kipya.
Akizungumza na MICHARAZO leo asubuhi, Maugo alisema awali pambano hilo litakalosimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania, PST, lilikuwa limkutanishe na bondia toka Iran, Gavad Zohrenvard.
Maugo alisema hata hivyo bondia huyo wa Iran amepatwa na dharura na hivyo kupangiwa Mganda ili kuonyeshana nae kazi siku ya pambano hilo.
"Natarajia kupanda ulingoni Oktoba 28 kwenye ukumbi wa Triple A mjini Arusha kuzichapa na Mganda, Mustapha Katende, ambapo pia tutasindikizwa na michezo mbalimbali ya utangulizi," alisema.
Alitaja baadhi ya mabondia watakaowasindikiza siku hiyo ni Robert Mrosso wa Arusha atakayepigana na Selemani Said 'Tall' wa Dar na Abbas Ally wa Arusha dhidi ya Joseph Marwa wa Zanzibar.
Bondia huyo aliyepanda mara ya mwisho ulingoni April mwaka huu kuwania ubingwa wa IBF-Mabara dhidi ya Francis Cheka na kupigwa, alisema amejiandaa vya kutosha kuweza kunyakua taji hilo la WBF dhidi ya Mganda.
"Naendelea kujifua kwa ajili ya kuhakikisha natwaa taji hilo, sambamba na kusaidia kutoa hamasa kwa vijana wenye vipaji vya ngumi mkoani Arusha," alisema Maugo.

Mwisho

WAZIRI MAKALLA MGENI RASMI PAMBANO LA CHEKA< NYILAWILA

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Amos Makalla atakayekuwa mgeni rasmi katika pambano la ngumi la kuwania ubingwa wa UBO Mabara kati ya Francis Cheka na Karama Nyilawila


NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni Vijana na Michezo, Amos Makalla anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa pambano la kimataifa la kuwania ubingwa wa Mabara wa UBO kati ya mabondia Francis Cheka na Karama Nyilawila.
Pambano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam Septemba 29, na waratibu wa mchezo huo, kampuni ya Afrika Kabisa Entertainment wamesema Waziri Makalla ndiye atakayemvisha taji mshindi.
Promota Robert Ekerege, aliiambia MICHARAZO kwamba tayari amehakikishiwa na Waziri Makalla kuwa mgeni rasmi katika pambano hilo la Super Middle la raundi 12 amblo litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
"Mgeni rasmi katika pambano letu kati ya Cheka na Nyilawila atakuwa Naibu Waziri wa Michezo, Amos Makalla, na kila kitu kimekamilika katika maandalizi ya pambano hilo," alisema Ekerege.
Ekerege alisema mbali na Waziri Makalla, pia siku ya pambano hilo litahudhuriwa na Mlezi wa mchezo wa ngumi nchini, Suleiman Kova ambaye ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa, katika kunogesha pambano hilo mabondia kadhaa karibu 10 watapanda ulingoni kuwasindikiza akina Cheka kwa kucheza michezo ya raundi sita kila moja na wa watasindikiza na burudani toka Mashujaa Band.
"Mashujaa Band ndio watakaosindikiza michezo hiyo yote ambayo itakuwa na ulinzi wa kutosha ili kudhibiti vitendo vyote vya kihuni ambavyo vinaweza kutuharibia," alisema Ekerege.

Mwisho

VAN PERSIE AIZAMISHA LIVERPOOL, ARSENAL WAISHIKA MANCHESTER CITY, DEMBA BA HASHIKIKI...MILAN, INTER HOI!


LONDON, England
PENATI ya Robin van Persie kuelekea mwishoni mwa mechi iliipa Manchester United iliyocheza chini ya kiwango ushindi wa ugenini wa 2-1 dhidi ya wachezaji 10 wa Liverpool katika mechi yao iliyojaa hisia ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Anfield huku mabingwa watetezi, Manchester City wakishikiliwa kwa sare ya nyumbani ya 1-1 dhidi ya Arsenal leo.
Mholanzi Van Persie aliwahakikishia ushindi Man U wakati alipopiga penati ya shuti kali iliyomshinda kipa Pepe Reina kufuatia Glen Johnson kumuangusha Antonio Valencia.
Licha ya kucheza chini ya kiwango, Man U walipanda hadi katika nafasi ya pili katika msimamowa ligi wakiwa na pointi 12, wakizidiwa kwa pointi moja tu na vinara Chelsea.
Man City walipata sare ya tatu katika mechi zao tano za mwanzo wa msimu baada ya  Laurent Koscielny kuisawazishia Arsenal kwa bao la 'usiku' kufuatia goli la utangulizi la Joleon Lescott kuwapa wenyeji uongozi hadi mapumziko. Timu zote mbili hazijafungwa na kufikisha pointi tisa.
Tottenham Hotspur wamefikisha pointi nane baada ya Jermain Defoe kuwafungia bao la ushindi wa 2-1 dhidi ya Queens Park Rangers, ukiwa ni ushindi wa kwanza wa nyumbani wa Tottenham chini ya kocha Andre Villas-Boas.
Demba Ba alifunga bao pekee lililowapa Newcastle United ushindi wa 1-0 dhidi ya Norwich City inayonolewa na kocha wao wa zamani, Chris Hughton.
Hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Anfield tangu kutolewa kwa taarifa ya  Hillsborough iliyowasafisha mashabiki wa Liverpool ambao awali walikuwa wakilaumiwa kwa kusababisha vifo vya mashabiki 96 kwenye mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la FA mwaka 1989.
Balaa kwa Liverpool lilianza katika dakika ya 39 wakati mchezaji wao Jonjo Shelvey alipotolewa nje kwa kadi nyekundu.
Hata hivyo, Liverpool walipata bao walilostahili baada ya kuanza kipindi cha pili kupitia shuti la Steven Gerrard, lakini Man U wakasawazisha dakika sita baadaye kupitia shuti la "upinde" la beki Rafael.
Bao la 'usiku' la Van Persie, ambalo ni la tano kwake msimu huu, limemuacha kocha Brendan Rodgers akikosa ushindi baada ya mechi tano za mwanzo wa msimu, ikiwa ni rekodi "mbovu" kabisa katika historia ya klabu hiyo kwenye Ligi Kuu ya England.

Yanga kupokwa ushindi dhidi ya JKT Ruvu?

Kikosi cha timu ya Yanga

LICHA ya kuchekelea ushindi wa mabao 4-1 iliyopata dhidi ya JKT Ruvu, mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga huenda wakapokwa ushindi wao huo iliyopata juzi kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar iwapo itabainika wakikiuka kanuni za ligi juu ya idadi ya wachezaji wa kigeni kucheza mechi moja.
Yanga katika mechi yao na JKT iliwachezesha wachezaji wake wote watano wa kigeni, kitu kinachoelezwa ni kinyume na kanuni inayoruhusu klabu kuwatumia wachezaji wasiozidi watatu kucheza mechi moja ya ligi.
Katika pambano hilo la juzi Yanga iliwachezesha mapro wake wote akiwamo kipa Yew Berko, beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima, mshambuliaji Didier Kavumbagu na winga Hamis Kiiza.
Micharazo, imedokezwa kwamba uongozi wa Simba tayari unajiandaa kuwasilisha barua ya kupinga kitendo kilichofanywa na watani zao za kuwatumia wachezaji wake hao wa kigeni katika mechi moja, ingawa tunaendelea kufuatilia kuona kama Yanga ilikiuka kanuni ya ligi kuhusu wachezaji au la...
Kama itakuwa imekiuka kuna uwezekano Yanga wakajikuta wakipokwa ushindi huo na kuzidi kuwasononesha baada ya kutoka kwenye machungu ya kushindwa kufurukuta katika mechi zao za awali ambapo ililazimishwa suluhu na Prisons Mbeya kabla ya kulala mabao 3-0 kwa Mtibwa Sugar.


Simba yazidi kupaa Ligi Kuu Tanzania Bara

Amri Kiemba wa Simba ajijaribu kumtoka beki wa Ruvu katika pambano lao la jana
 
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba, wameendeleza wimbi la ushindi wa asilimia 100, baada ya kuibuika na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, pambano lililochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 30, likiwekwa nyavuni na nyota wa kimataifa wa Zambia, Sunzu kwa kichwa maridadi akimalizia krosi iliyopigwa baada ya kazi nzuri ya kuwachambua mabeki iliyofanya na Said Nassor ‘Cholo’ aliyepanda kusaidia mashambulizi.

Dakika 38, Kiemba akawachachafya wachezaji wa Ruvu, kabla ya krosi yake kukosa mmaliziaji na kuishia mikononi mwa Benjamin Haule.

Simba iliendelea kushambulia ambapo katika dakika ya 44, beki Mau Bofu wa Ruvu alimwangusha Sunzu ndani ya 18 na mwamuzi Swai kuamuru ipigwe penati. Akuffor akabeba jukumu la kupiga tuta hilo, ambalo mlinda mlango Haule alipangua na kuwa kona tasa.

Hadi mapumziko, Simba ilitoka ikiongoza kwa bao hilo, huku mashabiki waliohudhuria mechi hiyo wakishuhudia maamuzi tata ya mwamuzi Swai, aliyeonekana dhahiri kutowajali vibendera wake Samwel Mpenzu na Godfrey Kihwili wote wa Arusha pindi wanapoashiria madhambi.

Kipindi cha pili kilianza kwa Ruvu kushambulia lango la Wekundu na kama si umakini mdogo miongoni mwa washambuliaji wake Paul Ndauka, Hussein Said na Hassan Dilunga aliyekuwa akipenya kirahisi safu ya ulinzi, wangeweza kupata mabao.

Sunzu akafanya shambuliazi kali dakika ya 55 lililotokana na jitihada binafsi akiwalima chenga mabeki, kabla ya Ruvu nao kurudi langoni mwa Simba na Dilunga (Hassani) nusura aipatie bao timu yake, kabla ya mawasiliano madogo na Abdulrahman Mussa kumgharimu.

Ruvu ikapata bao la kusawazisha mnamo dakika ya 78, lililowekwa nyavuni na mtokea benchi Seif Rashid, akitumia makosa ya beki Juma Nyoso wa Simba, aliyeshindwa kuondoa hatari langoni akiwa peke yake na kuukanyaga mpira huo na kuteleza, ambapo Seif aliunasa na kumchambua Juma Kaseja.

Daniel Akuffor akimtoka beki wa Ruvu Shooting


Wakati wengi wakimiani matokeo ya pambano hilo yangebaki kuwa ni sare ya bao 1-1, mtokea benchi wa Simba, Christopher Edward aliyeingia kuchukua nafasi ya Akuffor, akaipatia timu yake bao la pili dakika ya 87 kwa shuti na kuamsha mamia ya mashabiki wake jukwaani.