STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, May 19, 2012

Doyi Moke awataka Yanga watulie

KIPA nyota wa zamani wa klabu za Majimaji-Songea, Simba na Yanga, Doyi Moke, amewasihi wanachama wa timu ya Yanga kumaliza matatizo yao kwa kukaa mezani na kuzungumza. Aidha, kipa huyo raia wa JK Congo na aliyewahi kuzidakia pia timu za Rayon Sport ya Rwanda na Vital'O ya Burundi, alisema wanayanga wanapaswa kukumbuka kuwa mbele yao kuna kibarua cha kutetea taji la Kombe la Kagame la klabu bingwa za Afrika Mashariki na Kati hivyo watulizane mapema. Akizungumza kwenye mahojiano maalum, mkali huyo ambaye kwa sasa ni mfanya biashara madini alisema Yanga watajuta mbeleni wasipokaa mezani. "Nadhani hali inayoendelea Yanga haileti ishara njema, pande zinazotofautiana zikae chini na kuzungumza, kuendelea kulumbana bila kupata muafaka ni kuiweka pabaya timu yao wakati wanakabiliwa na michuano ya Kombe la Kagame linaloanza Juni," alisema. Alisema hadhani kama kuendelea kujadili kipigo cha mabao 5-0 walichopewa na watani zao Simba au kupokonywa taji la ligi kuu itaisaidia klabu hiyo wakati matokeo hayo hayawezi kubadilika. Baadhi ya wanachama wa Yanga wamekuwa wakishinikiza mwenyekiti Lloyd Nchunga ajiuzulu mara moja, na katika kuhakikisha hilo wameitisha mkutano mkuu kesho klabuni huku mwenyekiti akiwa ametaja Julai 15 kuwa siku ya mkutano mkuu rasmi wa mwaka.
Doye Moke enzi akicheza soka nchini Tanzania

Mashujaa, Mashauzi kung'arisha Miss Tabata

BENDI zinazotamba nchini kwa sasa Mashujaa na Mashauzi Classic zitatumbuiza kwenye kinyang'anyiro cha kumtafuta mrembo wa Tabata kitakachofanyika Juni Mosi katika ukumbi wa Da West Park, Tabata. Mratibu wa shindano hilo, Godfrey Kalinga alisema wameamua kuweka burudani yenye ladha tofauti ili kukidhi kiu ya watu mbalimbali watakaohudhuria shindano hilo. Kalinga alisema siku hiyo pia itatumika kusherehekea miaka 10 tangu kuasisiwa kwa shindano la Miss Tabata. "Shindano la mwaka huu litakuwa ni la aina yake kwa sababu utakuwa ni mwaka wetu wa 10 tangua kuanza kuandaa Miss Tabata... ndio maana tunaleta burudani nyingi," alisema mratibu huyo wa Bob Entertainment na Keen Arts. Alisema warembo waliyowahi kushinda mataji mbalimbali ya shindano hilo, pia wamealikwa kusherehekea miaka 10 ya Miss Tabata. Shindano hili limedhaminiwa na Dodoma Wine, Redds, Integrated Communications, Fredito Entertainment, Multichoice Tanzania, Screen Masters, Kitwe General Traders, Step In Electronics, Brake Point, Atriums Hotel na Lady Pepeta. Warembo 10 wa kwanza watafuzu kushiriki Miss Ilala na baadaye Miss Tanzania. Mrembo anayeshikilia taji la Tabata kwa sasa ni Faiza Ally. Warembo wa Tabata wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano ya Miss Tanzania ambapo 2010 Consolata Lukosi alishinda nafasi ya tatu kabla ya kutangazwa kuwa balozi wa kinywaji cha Redds.
Visura watakaochuana kinyang'anyiro cha Miss Tabata 2012

'Ticotico' wa Simba aanzisha klabu binafsi ya soka, kuteta leo

ALIYEWAHI kuwa Katibu wa Kamati ya Fedha ya klabu ya Simba, Onesmo Waziri 'Ticotico' ameanzisha klabu ya soka iitwayo 'Golden Bush Fc', ambayo imeshasajiliwa rasmi tayari kwa ajili ya ushiriki wa michuano mbalimbali. Akizungumza na MICHARAZO, Ticotico, mmoja wa 'membaz' wa zamani wa Friends of Simba, alisema klabu yake imesajiliwa ndani ya wilaya ya Kinondoni na itakuwa na makao makuu yake eneo la Mabibo, Dar es Salaam. Alisema mpaka sasa timu hiyo imeanza kukusanya wachezaji chini ya kocha wa muda, nyota wa zamani wa timu ya Yanga, Waziri Mahadh 'Mandieta'. Ticotico, alisema katika kuhakikisha klabu yake inajiendesha kisasa ikiwa na ufadhili wa kutosha wameitisha mkutano na wadau wa soka wilayani Kinondoni, ili kujadili na kutoa mawazo yao. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika leo Jumamosi mchana, kwenye majengo ya ofisi ya TANLAP, Kinondoni Biafra. Ticotico aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Red Coast iliyotamba Ligi ya TFF-Kanda, alisema lengo la kuanzisha klabu hiyo ni kuendeleza soka nchini sambamba na kuwasaidia vijana wenye vipaji vya mchezo huo. "Katika kuendeleza soka nchini nimeamua kuanzisha klabu itakayoitwa Golden Bush, ambayo imeshasajiliwa na Jumamosi tunatarajia kufanya mkutano au tuseme kongamano la wadau wa soka kupata mawazo namna ya kuifanya iwe klabu ya kipekee Kinondoni," alisema. Mwisho

KWAHERI JEMBE MAFISANGO TUTAKUKUMBUKA DAIMA

MAISHA UPITA, LAKINI MEMA NA MAZURI YA MTU HAYASAHAULIKI. TUTAKUKUMBUKA DAIMA PATRICK MUTESA MAFISANGO KWA UHAMIRI WAKO DIMBANI. KAPUMZIKE KWA AMANI BABA!

Jezi ya Mafisango yataifishwa SIMBA, Wengi wamlilia!

KLABU ya soka ya Simba imeamua 'kuitaifisha' jezi namba 30, aliyokuwa akiitumia kiungo wao wa kimataifa kutoka Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Patrick Mutesa Mafisango kama njia ya kumuenzi. Uongozi wa Simba umesema kuanzia sasa hautaitumia tena jezi hiyo kama heshima ya mchezaji huyo aliyefariki usiku wa kuamkia juzi, jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Simba, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia waombolezaji waliofika kuuaga mwili wa marehemu Mafisango kwenye viwanja vya TCC-Chang’ombe, Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl JK Nyerere, ili kusafirishwa leo kwenda kwao Kongo kwa ajili ya mazishi yanayofanyika kesho Jumapili. Heshima, aliyopewa Mafisango inafanana ya ile ya kiungo wa zamani wa kimataifa wa Cameroon, Marc Vivien Foe na klabu yake, Manchester City ya England alipofariki Juni, 2003, ambapo jezi yake namba 23 ilitunzwa moja kwa moja. Kiungo huyo aliyekuwa ameitwa saa chache kujiunga na timu yake ya taifa ya Rwanda 'Amavubi' kwa kipindi alichoichezea Simba alijijengea jina kwa umahiri aliokuwa nao dimbani, kiasi cha kusamehewa hata alipofanya utovu wa nidhamu hivi karibuni kambi ya timu hiyo. Rage alisema msiba huu ni mkubwa kwa Simba kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa ni muhimili mkubwa kwa timu hiyo akiwashauri wachezaji na kuwa nao karibu ndani na nje ya uwanja. “Mafisango alikuwa na mchango mkubwa kwa Simba na mara ya mwisho klabu kukumbumbwa na msiba mzito namna hii ilikuwa ni mwaka 1978 ambapo Simba ilimpoteza mchezaji wake mahiri Hussein Tidwa na ukweli ni kwamba wachezaji hawa tutawaenzi miaka yote na ndio sababu ya kutotumia tena jezi namba 30 kwa kuvaliwa na mchezaji yoyote,” alisema Rage. Rage alisema licha ya umahiri wa Mafisango Dimbani pia alikuwa mchezaji ambaye alitoa mchango mkubwa na hasa wachezaji wawapo nje ya nchi kutokana na umahiri wake wa kujua lugha mbalimbali ambapo alikuwa akiwasaidia wachezaji wenzake. “Ni pengo kubwa kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa akijua lugha nyingi ikiwemo Kiswahili, Kingereza na Kifaransa na kuwasaidia wachezaji walipokuwa nje ya nchi tutamkubuka sana Mafisango,” aliongeza. Kutokana na machungu ya msiba huo Rage alishindwa kumaliza kusoma risala fupi ya marehemu mara baada ya kuishiwa nguvu na kumwaga machozi na kupelekea Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Godfrey Nyange ‘Kaburu’ kumsaidia kusoma risala hiyo. “Mfisango ni mchezaji ambaye alikuwa akijituma nje na ndani ya uwanja na kabla ya kutua Simba Marehemu aliwahi kucheza soka katika timu mbalimbali ikiwemo Tp Mazembe ya DRC, APR ya Rwanda , Azam na Simba za Tanzania na pia alikuwa Nahodha wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ alisema Kaburu. Wakati wa kutoa heshima za mwisho katika uwanja wa Sigara maelfu ya watu walijitokeza uwanjani hapo wakiongozwa na mchungaji Tito Kihame ambaye aliongoza ibada ya kuuga mwili wa marehemu, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara na viongozi mbalimbali wa serikali na viongozi kutoka klabu mbalimbali za hapa nchini. Mukangara aliwataka wachezaji wa Tanzania kujituma na kuwa na moyo kama ambao alikuwa nao Marehemu Mafisango kwa kujituma na kuwa na jitihada za zaidi nje na ndani ya uwanja kama ambavyo marehemu alivyokuwa akifanya. “Kifo chake ni pigo kubwa kwa Simba na Watanzania kwa ujumla na tunamshukuru kwa kuvuka mipaka na kuona umuhimu wa kuja na kucheza Tanzania na pia wachezaji wa Simba wasikate tamaa cha muhimu waendeleze kile ambacho alikiacha marehemu,” alisema Mukangara. “Ukweli ni kwamba katika familia ya soka hapa nchini tumepoteza mtu muhimu sana na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani,” alisema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF Angetile Osiah. “Sisi Simba ni watani zetu na tunakuwa pamoja katika shida na hivyo basi mimi kama kiongozi wa Yanga nimeiwakilisha klabu nzima na tutaendelea kuwa bega kwa bega na watani zetu katika kipindi hiki kigumu ila mchezaji Mafisango alikuwa ni mchezaji hodari uwanjani hivyo basi anastaili kuigwa na wachezaji wengine,” alisema Selestine Mwesigwa katibu Mkuu wa Yanga. Nao wachezaji mbalimbali kutoka timu ya Taifa Taifa Stars walijitokeza na kubeba jeneza la mchezaji mwenzao na kuliingiza katika viwanja vya Sigara wachezaji hao Juma Kaseja, Jonh Bocco, Mwinyi Kazimoto, Shabani Nditi, Amiry Maftah, Nurdin Bakari, Agrey Moris na Juma Nyoso. Profesa Philemon Sarungi akimsaidia Rage Mara baada ya nyota hao kuufikisha mwili wa marehemu katika sehemu husika ambayo ilipangwa Kazimoto na Kaseja iliwalazimu watu wa ziada kujitokeza na kuwapa sapoti mara baada ya kushindwa kutembea na kuwapeleka katika eneo husika ambalo walikuwa wamepangiwa kukaa. Naye Msemaji wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema msafara wa leo kwenda Kongo kuusafirisha mwili wa Mafisango, Haruna Moshi 'Boban' atawakilisha wachezaji wa klabu hiyo huku kwa uongozi atakuwa Mjumbe wao wa kamati ya utendaji Joseph 'Mzee Kinesi' Itang’are. Kamwaga alisema mwili huo ungeondoka asubuhi ya leo ukiambatana na mtoto wa marehemu Crespo Tabu Mutesa, mwenye umri wa miaka mitano na mchezaji wa Yanga Haruna Niyonzima ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda.