STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, May 19, 2012

Jezi ya Mafisango yataifishwa SIMBA, Wengi wamlilia!

KLABU ya soka ya Simba imeamua 'kuitaifisha' jezi namba 30, aliyokuwa akiitumia kiungo wao wa kimataifa kutoka Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Patrick Mutesa Mafisango kama njia ya kumuenzi. Uongozi wa Simba umesema kuanzia sasa hautaitumia tena jezi hiyo kama heshima ya mchezaji huyo aliyefariki usiku wa kuamkia juzi, jijini Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Simba, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia waombolezaji waliofika kuuaga mwili wa marehemu Mafisango kwenye viwanja vya TCC-Chang’ombe, Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl JK Nyerere, ili kusafirishwa leo kwenda kwao Kongo kwa ajili ya mazishi yanayofanyika kesho Jumapili. Heshima, aliyopewa Mafisango inafanana ya ile ya kiungo wa zamani wa kimataifa wa Cameroon, Marc Vivien Foe na klabu yake, Manchester City ya England alipofariki Juni, 2003, ambapo jezi yake namba 23 ilitunzwa moja kwa moja. Kiungo huyo aliyekuwa ameitwa saa chache kujiunga na timu yake ya taifa ya Rwanda 'Amavubi' kwa kipindi alichoichezea Simba alijijengea jina kwa umahiri aliokuwa nao dimbani, kiasi cha kusamehewa hata alipofanya utovu wa nidhamu hivi karibuni kambi ya timu hiyo. Rage alisema msiba huu ni mkubwa kwa Simba kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa ni muhimili mkubwa kwa timu hiyo akiwashauri wachezaji na kuwa nao karibu ndani na nje ya uwanja. “Mafisango alikuwa na mchango mkubwa kwa Simba na mara ya mwisho klabu kukumbumbwa na msiba mzito namna hii ilikuwa ni mwaka 1978 ambapo Simba ilimpoteza mchezaji wake mahiri Hussein Tidwa na ukweli ni kwamba wachezaji hawa tutawaenzi miaka yote na ndio sababu ya kutotumia tena jezi namba 30 kwa kuvaliwa na mchezaji yoyote,” alisema Rage. Rage alisema licha ya umahiri wa Mafisango Dimbani pia alikuwa mchezaji ambaye alitoa mchango mkubwa na hasa wachezaji wawapo nje ya nchi kutokana na umahiri wake wa kujua lugha mbalimbali ambapo alikuwa akiwasaidia wachezaji wenzake. “Ni pengo kubwa kwa kuwa mchezaji huyo alikuwa akijua lugha nyingi ikiwemo Kiswahili, Kingereza na Kifaransa na kuwasaidia wachezaji walipokuwa nje ya nchi tutamkubuka sana Mafisango,” aliongeza. Kutokana na machungu ya msiba huo Rage alishindwa kumaliza kusoma risala fupi ya marehemu mara baada ya kuishiwa nguvu na kumwaga machozi na kupelekea Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Godfrey Nyange ‘Kaburu’ kumsaidia kusoma risala hiyo. “Mfisango ni mchezaji ambaye alikuwa akijituma nje na ndani ya uwanja na kabla ya kutua Simba Marehemu aliwahi kucheza soka katika timu mbalimbali ikiwemo Tp Mazembe ya DRC, APR ya Rwanda , Azam na Simba za Tanzania na pia alikuwa Nahodha wa timu ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ alisema Kaburu. Wakati wa kutoa heshima za mwisho katika uwanja wa Sigara maelfu ya watu walijitokeza uwanjani hapo wakiongozwa na mchungaji Tito Kihame ambaye aliongoza ibada ya kuuga mwili wa marehemu, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara na viongozi mbalimbali wa serikali na viongozi kutoka klabu mbalimbali za hapa nchini. Mukangara aliwataka wachezaji wa Tanzania kujituma na kuwa na moyo kama ambao alikuwa nao Marehemu Mafisango kwa kujituma na kuwa na jitihada za zaidi nje na ndani ya uwanja kama ambavyo marehemu alivyokuwa akifanya. “Kifo chake ni pigo kubwa kwa Simba na Watanzania kwa ujumla na tunamshukuru kwa kuvuka mipaka na kuona umuhimu wa kuja na kucheza Tanzania na pia wachezaji wa Simba wasikate tamaa cha muhimu waendeleze kile ambacho alikiacha marehemu,” alisema Mukangara. “Ukweli ni kwamba katika familia ya soka hapa nchini tumepoteza mtu muhimu sana na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani,” alisema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF Angetile Osiah. “Sisi Simba ni watani zetu na tunakuwa pamoja katika shida na hivyo basi mimi kama kiongozi wa Yanga nimeiwakilisha klabu nzima na tutaendelea kuwa bega kwa bega na watani zetu katika kipindi hiki kigumu ila mchezaji Mafisango alikuwa ni mchezaji hodari uwanjani hivyo basi anastaili kuigwa na wachezaji wengine,” alisema Selestine Mwesigwa katibu Mkuu wa Yanga. Nao wachezaji mbalimbali kutoka timu ya Taifa Taifa Stars walijitokeza na kubeba jeneza la mchezaji mwenzao na kuliingiza katika viwanja vya Sigara wachezaji hao Juma Kaseja, Jonh Bocco, Mwinyi Kazimoto, Shabani Nditi, Amiry Maftah, Nurdin Bakari, Agrey Moris na Juma Nyoso. Profesa Philemon Sarungi akimsaidia Rage Mara baada ya nyota hao kuufikisha mwili wa marehemu katika sehemu husika ambayo ilipangwa Kazimoto na Kaseja iliwalazimu watu wa ziada kujitokeza na kuwapa sapoti mara baada ya kushindwa kutembea na kuwapeleka katika eneo husika ambalo walikuwa wamepangiwa kukaa. Naye Msemaji wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema msafara wa leo kwenda Kongo kuusafirisha mwili wa Mafisango, Haruna Moshi 'Boban' atawakilisha wachezaji wa klabu hiyo huku kwa uongozi atakuwa Mjumbe wao wa kamati ya utendaji Joseph 'Mzee Kinesi' Itang’are. Kamwaga alisema mwili huo ungeondoka asubuhi ya leo ukiambatana na mtoto wa marehemu Crespo Tabu Mutesa, mwenye umri wa miaka mitano na mchezaji wa Yanga Haruna Niyonzima ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda.

No comments:

Post a Comment