STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, July 3, 2014

Suarez azigonganisha Liverpool, Barcelona

MSHAMBULIAJI nyota wa Uruguay aliyefungiwa na FIFA kwa kitendo cha kumng'ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini, Luis Suarez amezigoinganisha klabu yake ya Liverpool na Barcelona inayowania saini yake.
Klabu hizo zinatarajia kuanza kufanya mazungumzo juu ya bei ya awali ya paundi milioni 80 ili kuuziana mshambuliaji  huyo.
Mtandao wa michezo wa Sportsmail unafahamu kuwa maofisa wa Liverpool, akiwemo mkurugenzi mtendaji, Ian Ayre, wamekubali kukutana na mkurugenzi wa michezo wa FC Barcelona, Raul Sanllehi,  mjini London ili kujadiliana thamani ya mchezaji huyo mwenye miaka 27.
Barcelona wanatazamiwa kutoa paundi milioni 60 kwa kuzingatia kuwa Suarez amefungiwa miezi minne kucheza soka baada ya kumng`ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini.
Liverpool hawapo tayari kushusha bei ya Suarez, lakini wanataka kumhusisha mshambuliaji wa Barcelona Alexis Sanchez kama sehemu ya makubaliano hayo.
Barcelona wanasema mchezaji wao wa kimataifa wa Chile ana thamani ya paundi milioni 35, lakini tayari wameshakataa ofa ya paundi milioni 20 kutoka kwa Juventus ya Italia iliyokuwa na nia ya kumsajili nyota huyo mwenye miaka 25.

Domayo nje Azam kwa miezi minne kisa upasuaji

MABINGWA wa soka nchini, Azam Fc, imesema kiungo wake Frank Domayo atakuwa nje ya uwanja wa muda wa miezi minne kufuatia upasuaji wa mguu aliofanyiwa nchini Afrika Kusini.
Akizungumzia jiji Afisa Habari wa Azam, Jaffar Idd  amesema uchunguzi wa afya wa kiungo huyo aliofanyiwa na mganga mkuu wa klabu hiyo Dk Mwamkemwa ulibaini kuwa Domayo ana matatizo ya msuli wa mguu wake wa kushoto na kwamba atatakiwa kufanyiwa upasuaji.
Domayo alipekwa na uongozi wa Azam wiki iliyopita nchini Afrika Kusini akiambatana na Dk Mwankemwa ambapo juzi alifanyiwa upasuaji katika hospitali ya Vicent Parent na imeelezwa kuwa anaendelea vizuri huku akitarajiwa kurejea nchini Jumapili.
  Afisa Habari huyio amesema kiungo huyo atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi miezi minne akiendelea kupata tiba na uangalizi wa karibu wa jeraha lake kabla ya kurejea uwanjani kuitumikia klabu yake hiyo mpya ambayo amejiunga nayo hivi karibuni.

Cameroon yachunguzwa kwa upangaji matokeo Brazil

TIMU ya soka ya taifa ya Cameroon, inachunguzwa kwa tuhuma za upangaji wa matokeo katika mechi zao za Kombe la Dunia waliotolewa hatua ya makundi nchini Brazili.
Maafisa wa Cameroon watapelelezwa kutokana na madai kwamba saba kati ya wachezaji wa timu ya taifa hilo walihusika katika kupanga mechi katika Kombe la Dunia linaloendelea nchini Brazil.
Kamati ya maadili ya shirikisho la kandanda la taifa hilo litachunguza shutuma za "udanganyifu" wa "wachezaji saba wabaya" katika mechi zao tatu za makundi.
Madai hayo yametolewa na gazeti moja la kijerumani na mtu aliyehukumiwa kwa kuhusika na kupanga mechi nchini Singapore.
Cameroon ilipoteza mechi zote za kundi A, ikiwemo ile waliolazwa na Croatia kwa mabao 4-0.
Mchezaji wa 'The Indomitable Lions' Alex Song, alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumgota Mario Mandzukic mgongoni katika mechi hiyo, huku wachezaji wenzake Benoit Assou-Ekotto na Benjamin Moukandjo wakizozana baadaye katika mechi hiyo.
Ripoti kutoka katika shirikisho la kandanda la Cameroon lilisema: "Madai yaliyotolewa majuzi kuhusu udanganyifu katika mechi tatu za mwanzo za Cameroon katika Kombe la Dunia la 2014, hasa kati ya Cameroon na Croatia, na vile vile 'kuwepo na wacheza saba wabaya katika timu yetu ya taifa' hayaambatani na maadili na kanuni zinazopendekezwa na usimamizi wetu, pamoja na kanuni za Fifa na maadili ya taifa letu.
"Tuna nia kuu ya kutumia mbinu zote zinazostahili ili kutatua swala hili linalosumbua kwa muda mfupi iwezekanavyo."
Fifa haikusema iwapo ilikuwa ikichunguza swala hilo au la, kwani bodi hiyo inayosimamia kandanda ulimwenguni "ilitaka uchunguzi uwe wazi".

Mbeya City, Prisons kuzipima tiketi za Electronic

Mbeya City
Prisons-Mbeya
TIMU za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) za Mbeya City na Tanzania Prisons zinacheza mechi ya kirafiki Jumamosi (Julai 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kuchezwa jijini Mbeya katika mfumo wa matumizi ya tiketi za elektroniki kwa washabiki wanaoingia uwanjani itaanza saa 10 kamili jioni.
Kiingilio ni sh. 3,000 kwa majukwaa yote ambapo tiketi zimeanza kuuzwa leo (Julai Mosi mwaka huu).
Wakati huo huo, keshokutwa (Julai 3 mwaka huu) kutakuwa na mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki yatakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuanzia saa 3 asubuhi.
Washiriki wa mafunzo hayo ni wasimamizi wa mechi katika uwanja huo, viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), meneja wa Uwanja wa Sokoine na msaidizi wake, makatibu wa Tanzania Prisons na Mbeya City, maofisa habari wa Mbeya City na Tanzania Prisons, Ofisa Usalama wa MREFA na wasimamizi wa milangoni (stewards).

Stars yapigwa 4 Botswana kujiuliza kwa Lesotho

TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) juzi ilikubali kichapo cha mabao 4-2 kutoka kwa wenyeji wao timu ya Botswana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika jijini Gaborone.
Mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa wa Gaborone, ilishuhudiwa hadi mapumziko Stars ilikuwa nyuma kwa mabao 3-0 licha kuonekana timu zote zikishambuliana kwa zamu.
Mabao ya Stars katika mchezo huo wa kirafiki yalifungwa na wachezaji wa klabu ya Azam, Khamis Mcha 'Vialli' na John Bocco 'Adebayor' kwa njia ya penalti.
Kikosi hichio cha kocha Mart Nooij kitashuka dimbani tena siku ya Jumamosi kupepetana na Lesothio katika pambano jingine la kirafiki la kimataifa kabla ya siku inayofuata kurejea nyumbani kujiwinda na mechi yao ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kucheza Fainali za Kombe la Afrika za mwakani.
Taifa Stars imeweka kambi ugenini kwa ajili ya kujiandaa na mechi yake ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Msumbiji itakayofanyika Julai 20 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Stars ambayo ilisonga mbele katika mashindano hayo baada ya kuifunga Zimbabwe mabao 3-2 na kama itafanikiwa kuing'oa Msumbiji katika mechi zao itaangukia kundi moja na timu za Zambia, Cape Verde na Niger ili kuwania kucheza fainali hizo za Afrika zitakazofanyika nchini Morocco.