STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, July 3, 2014

Cameroon yachunguzwa kwa upangaji matokeo Brazil

TIMU ya soka ya taifa ya Cameroon, inachunguzwa kwa tuhuma za upangaji wa matokeo katika mechi zao za Kombe la Dunia waliotolewa hatua ya makundi nchini Brazili.
Maafisa wa Cameroon watapelelezwa kutokana na madai kwamba saba kati ya wachezaji wa timu ya taifa hilo walihusika katika kupanga mechi katika Kombe la Dunia linaloendelea nchini Brazil.
Kamati ya maadili ya shirikisho la kandanda la taifa hilo litachunguza shutuma za "udanganyifu" wa "wachezaji saba wabaya" katika mechi zao tatu za makundi.
Madai hayo yametolewa na gazeti moja la kijerumani na mtu aliyehukumiwa kwa kuhusika na kupanga mechi nchini Singapore.
Cameroon ilipoteza mechi zote za kundi A, ikiwemo ile waliolazwa na Croatia kwa mabao 4-0.
Mchezaji wa 'The Indomitable Lions' Alex Song, alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumgota Mario Mandzukic mgongoni katika mechi hiyo, huku wachezaji wenzake Benoit Assou-Ekotto na Benjamin Moukandjo wakizozana baadaye katika mechi hiyo.
Ripoti kutoka katika shirikisho la kandanda la Cameroon lilisema: "Madai yaliyotolewa majuzi kuhusu udanganyifu katika mechi tatu za mwanzo za Cameroon katika Kombe la Dunia la 2014, hasa kati ya Cameroon na Croatia, na vile vile 'kuwepo na wacheza saba wabaya katika timu yetu ya taifa' hayaambatani na maadili na kanuni zinazopendekezwa na usimamizi wetu, pamoja na kanuni za Fifa na maadili ya taifa letu.
"Tuna nia kuu ya kutumia mbinu zote zinazostahili ili kutatua swala hili linalosumbua kwa muda mfupi iwezekanavyo."
Fifa haikusema iwapo ilikuwa ikichunguza swala hilo au la, kwani bodi hiyo inayosimamia kandanda ulimwenguni "ilitaka uchunguzi uwe wazi".

No comments:

Post a Comment