STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, March 15, 2015

Wenger anaamini wataing'oa AS Monaco

http://d.ibtimes.co.uk/en/full/110907/arsene-wenger.jpg
Kocha Wenger
KOCHA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anaamini kikosi chake kinaweza kuing’oa Monaco katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kufungwa mabao 3-1 katika mchezo wao wa kwanza. Arsenal inatarajiwa kucheza na Monaco Jumanne ijayo huku kukiwa hakuna timu ambayo ilifanikiwa kusonga mbele baada ya kipigo kama hicho katika mashindano hayo.
Akihojiwa, kocha Wenger amesema anajua changamoto kubwa iliyopo mbele yao lakini watajitahidi kufanya kila wanaloweza ili kuhakikisha wanasonga mbele.
Kocha huyo aliendelea kudai kuwa anajua Monaco wanapewa nafasi kubwa lakini wanaweza kubadili hilo kama wakitumia maarifa na ujuzi wao wote.
Ili waweze kusonga mbele Arsenal wanatakiwa walau wafunge mabao matatu huku wakijitahidi kudhibiti lango lao.
Mechi nyingine kwa siku hiyo ya Jumanne itazikutanisha timu za Atletico Madrid dhidi ya Bayer Leverkusen walioshinda nyumbani kwao bao 1-0.
Jumatano ijayo kutakuwa na mechi nyingine mbili kwa Juventus ya Italia kuwafuata Borussia Dortmund iliyolala ugenini 2-1 na Barcelona wataialika Manchester City ambao waliwafumua 2-1 katika mechi ya kwanza mwezi uliopita kwa mabao ya Luis Suarez.

CHELSEA WANG'ANG'ANIWA NYUMBANI

BANNER-Chelses-Southampton-v5.jpg
Muunganiko wa picha zilizochapishwa na Daily Mail wakati Chelsea wakilazimishwa sare nyumbani
VINARA wa Ligi Kuu ya England, Chelsea wameshindwa kutamba nyumbani baada ya kung'ang'aniwa na Southampton na kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mfululizo wa ligi hiyo.
Chelsea walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 11 kupitia bao la kichwa cha Diego Costa aliyemalizia krosi murua ya beki Branislav Ivanovic.
Dakika nane baadaye Southampton walifanikiwa kurejesha bao hilo kwa mkwaju wa penati baada ya Namanja Matic kucheza madhambi na Dusan  Tadic.
Kipa wa Chelsea aliucheza mpira huo kwa miguu, lakini kasi yake ulimzidi na kutinga wavuni na matokeo yalibaki hivyo hivyo licha ya wenyeji kucharuka na kulifikia lango la wageni wao, lakini kipa Fraser Forster alikuwa kikwazo kupata magoli ya kuwapa pointi tatu muhimu.
Hivi punde Everton watawalika dimbani Newcastle na Manchester United baadae itaikaribisha Tottenham Hotspur.

MIZANI YA KIBAHA MWISHO JUMANNE, TANROADS KUIFUNGA

http://1.bp.blogspot.com/-IdmavKJ4NFc/T_hmawYRw6I/AAAAAAAAWH8/hcDM2RYvvOc/s1600/mizani+ya+kibaha.jpgWAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS), umesema kuanzia Machi 17 mwaka huu mzani wa kupimia magari Kibaha hautaendelea kutoa huduma kwa magari na huduma hiyo itahamia katika mzani mpya wa Vigwazwa.
Hayo yalisemwa na Mtendaji Mkuu wa Tanroads Mhandisi Patrick Mfugale wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Alisema mzani wa Kibaha ulikuwa unatumia dakika moja na nusu kupima gari moja hali ambayo ilikuwa inasababisha msongamono ila mzani wa Vigwaza utakuwa unatumia sekunde 30 kwa gari moja.
Mhandisi Mfugale alisema kituo hicho cha Vigwazwa ni cha kisasa kina Mtambo wa Kuchambua magari (Weight-in- Motion) kwa kupima magari yakitembea.
Pia Mfugale alisema hicho kina Mzani Mkubwa (Multi-deck) unaweza kupima gari lolote kwa mkupuo hali ambayo itasaidia kupunguza msongamano.
"Mzani wa Vigwaza umekamilika na juzi ulianza kazi kwa majaribio ila tunatarajia kusitisha huduma ya upimaji uzito eneo la Kibaha kesho, hivyo ni vyema madereva wakajiandaa kwa hilo," alisema.
Alisema barabara ya za kuingia katika mzani huo ambazo zina kilometa 1.8 zimekamilika ambazo zina upana wa milikita 200 na kudumu kwa miaka zaidi ya 50.
Mtendaji Mkuu huyo alisema mzani huo utakuwa unaelekeza magari ambayo yamezidisha mzigo wapi yakapaki na yale ambayo hayana tatizo yaendelee kwa safari.
Alisema magari yanayotakiwa kupima uzito ni kuanzia yale yenye uzito kuanzia tani 3.5 ambapo aliwataka madereva kufuata taratibu na sheria za barabara kwa kuacha nafasi ya mita 30 kati ya gari na gari.
Mhandisi Mfugale alitoa rai kwa wamiliki wa magari kuhakikisha kuwa wanatengeneza magari yao ili kuepusha kuharibika katika eneo hilo kwani watapigwa faini.
Mfugale alisema mzani huo umegharimu bilioni 11 ambapo jitihada zao ni kuendelea na ujenzi katika mzani nyingine ili ziweze kuwa na ubora kama wa Vigwaza.

Angalia kituko alichofanya Wayne Rooney dhidi ya Phil Bardsley

Video iliyotolewa hadharani na The Sun akipigana jikoni na rafikie na hatimaye kupigwa konde lililomzimisha kwa sekunde kadhaa, huku wachezaji wa kulipwa wakizuiwa kushiriki michezo ya hatari kama ngumi n.k
Tukio hilo linadaiwa lilirekodiwa kitambo kabla ya kufichuliwa na The Sun

YANGA MPAKA RAHA, YAUA WAZIMBABWE 5-1

Tambwe ameendelea kuongeza idadi ya mabao katika michuano hiyo ya Afrika baada ya leo kufunga bao la tatu
http://www.herald.co.zw/wp-content/uploads/2015/02/ABDD.jpg
Wazimbabwe waliofumuliwa 'mkono'na Yanga kwenyue uwanja wa Taifa leo
AMA kweli Yanga ya sasa ni ya Kimataifa baada ya jioni hii kuifumua timu ya FC Platinum ya Zimbabwe kwa mabao 5-1 katika pambano la kwanza la raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ikikosa huduma za nyopta wake kadhaa akiwamo nahodha, Nadir Haroub 'Cannavaro', Yanga ilipata karamu hiyo kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kujiweka nafasi nzuri ya kutinga raundi ya pili.
Mabao ya Salum Telela aliyekuwa nahodha wa Yanga leo uwanjani, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe na mawili ya 'Uncle' Mrisho Ngassa yalitosha kuwanusisha vijana wa Jangwani raundi ijayo ambayo huenda wakavaana na ama Etoile du Sahel ya Tunisia au Benfica de Luanda ya Angola.
Mpaka mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-1 kabla ya kipindi cha pili kuongeza mengine na kuwapa wasaa nzuri kwa mechi ya marudiano wiki mbili zijazo, Yanga wakihitaji sare yoyote kusonga mbele.
Tofauti na ilivyotarajiwa mapema kwamba huenda Platinum waliyoing'oa Sofapaka ya Kenya kwa jumla ya mabao 4-2 ingewapeleka puta Yanga, mambo yamekuwa tofauti kwa wenyeji kuwapeleka mchakamchaka.

HAKUNA UFISADI UNUNUZI KIVUKO CHA MV DAR ES SALAAM

Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Eng. Mercelin Magesa
WAKALA wa Ufundi na Umeme (TEMESA) umesema hakuna ufisadi wowote ambao umefanyika katika mchakato mzima wa ununuzi wa Kivuko cha Mv Dar es Salaam.
Kauli hiyo Temesa imetolewa na Mtendaji Mkuu wa wakala huo Mhandisi Marcelin Magesa ikiwa ni siku moja baada ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuilalamikia Serikali kwa uamuzi wake wakununua Kivuko hicho wakati hakina tija kwa jamii.
Magesa alisema maandalizi ya awali ya ununuzi wa Kivuko hicho yalishirikisha wadau wote ambapo lengo lake ni kutoa huduma ya usafiri wa majini katika ukanda wa bahari ya Hindi.
Mtendaji Mkuu huyo alisema mpango wa ununuzi wa Kibuko hicho uliwasishwa katika Bunge la Bajeti la mwaka 2012/13 ambapo ulitengewa fedha ambapo fedha zingine zilitengwa bajti ya 2013/14 na 2014/15.
"Napenda kuweka wazi suala hili kwani juzi habari zilizotoka kwenye baadhi ya vyombo vya habari zinaonesha kuwa kuna mapungufu lakini utaratibu ulifuatwa kwa kutangazwa zabuni ambapo kampuni ua Ms. Johs Gram-Hanssen ya Denmark ndio ilishinda zabuni ya ujunzi wa Kivuko hicho kwa dola za Kimarekani 4,980,000 sawa na fedha za Tanzania sh.bilioni 7.916,955,000," alisema Magesa.
Alisema ujenzi wa Kivuko cha Mv Dar es Salaam, ulifanyika hatua kwa hatua ambapo kilifanyiwa ukaguzi mara nne Novemba 2013, Februari 2014, Julai 2014 na Septemba 2014 ambapo kiliingizwa majini kufanyiwa majaribio.
Magesa alisema kutokana na utaratibu wa ukaguzi huo ni dhahiri kuwa Kivuko hicho ni kipya, na kauli kuwa sio kipya zinahitaji kupuuzwa.
Mtendaji Mkuu alisema lengo la Kivuko hicho ni kupunguza msongamano ambao umekuwa ukiongezeka katika jiji la Dar es Salaam.
Alisema kwa sasa Temesa inaendelea kutoa huduma za usafiri nchini katika vituo mbalimbali 28  ambapo tangu mwaka 2012 wamenunua vivuko vitano vipya.
Mhandisi huyo alivitaja vivuko hivyo kuwa ni Mv Kilambo, Mv Mafanikio vinavyotoa huduma Mtwara, Mv Malagarasi Kigoma, Mv Tegemeo Mwanza na Mv Dar es Salaam