STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, May 23, 2012

Msondo Ngoma kupeleka mpya Masasi, ikienda kuzindua ukumbi wa Emirates

BENDI kongwe ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, inatarajiwa kuipeleka albamu yake mpya ya 'Suluhu' mjini Masasi, Mtwara watakapoenda kuzindua ukumbi mpya mjini humo. Msemaji wa Msondo, Rajabu Mhamila 'Super D' alisema bendi yao itaenda kuzindua ukumbi huo uitwao Emirates, siku ya Juni 2 ambapo watatumia nafasi hiyo kutambulisha albamu hiyo mpya na nyimbo zao za zamani. Super D, alisema Msondo imepewa fursa hiyo ya kwenda kuzindua na kutumbuiza ukumbini hapo baada ya maombi ya mashabiki wao wa Masasi kuililia bendi hiyo iende kuwapa burudani. Alisema, msafara wao utaongozwa na mkongwe Muhidini Gurumo 'Kamanda' aliyerejea upya kupanda jukwaani baada ya kitambo kirefu kusumbuliwa na maradhi. "Kamanda Gurumo ndiye atakayeongoza jahazi sambamba na Dokta Said Mabela ambapo tutatambulisha albamu yetu kwa mashabiki hao wa Masasi, sawi na kukumbushia vibao vyetu vya zamani," alisema. Albamu hiyo ya Msondo Ngoma ina nyimbo sita ambazo ni 'Suluhu', 'Lipi Jema', 'Dawa ya Deni', 'Baba Kibene' 'Nadhiri ya Mapenzi' na 'Kwa Mjomba Hakuna Urithi'. Mwisho

Twiga kupaa kesho Ethiopia

Timu ya soka ya Taifa ya wanawake 'Twiga Stars' inatarajia kuondoka nchini kesho Mei 24 kwa ndege ya Ethiopian Airlines kwenda Addis Ababa kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia. Pambano baina ya timu hizo mbili linatarajiwa kuchezwa Mei 27 mwaka huu mjini Addis Ababa. Kwa mujibu wa taarifa toka TFF, msafara wa Twiga Stars utakuwa na watu 25 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi. Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Lina Kessy ndiye atakayeongoza msafara huo. Twiga Stars itarejea nyumbani Mei 28 mwaka huu kusubiri mechi ya marudiano itakayochezwa Juni 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mshindi ndiye atakayepata tiketi ya kucheza Fainali za Nane za AWC zitakazochezwa Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.

Joto la usajili laanza kuwachoma nyota, Simba, Yanga Azam

JOTO la usajili wa klabu kwa ajili ya msimu ujao, limeanza kuwaunguza baadhi ya nyota wa Simba na Yanga kutokana na taarifa za kuonyeshwa milango ya kutokea, huku Coastal Union ikitangaza kuwatema washambuliaji wake, Ben Mwalala na Ally Ahmed 'Shiboli'. Japo viongozi wa Simba na Yanga wamekuwa wasiri wa panga wanalotarajia kutembeza kwa baadhji ya wachezaji wake, lakini taarifa tulizonazo ni kwamba kuna wachezaji sita wa Simba na 15 wa Yanga wataonyeshwa mlango wa kutimka katika klabu hizo. Wachezaji hao ni wale ambao walishindwa kuonyesha makali yao katika msimu huu kutokana na kuwa majeruhi au kukosa nafasi katika vikosi vya kwanza vya timu hizo mbili. Taaifa hizo zinasema kuwa wachezaji ambao bado wana mikataba na klabu hizo watapelekwa kwa mikopo mahali pengine na wale ambao mikataba yao inaisha wameshajitambua hawana chao na kuanza kutafuta mahali pa kukimbilia kabla ya kutupiwa virago vyao. Hata hivyo Coastal wenyewe wameshaweka bayana wachezaji iliyoachana nao wakiwemo Mwalala na Shiboli, kama mikakati yao ya kuimarisha kikosi chao. Azam wenyewe wamekuwa wakisisitiza kupitia viongozi wao kwamba wanamsubiri kocha wao mkuu, Stewart John Hall arejee toka mapumziko aje kukipangua kikosi chao. Hata hivyo mpaka sasa wameshawanyakua wachezaji wawili ambao ni kipa Deogratius Munishi 'Dida' na George Odhiambo 'Black Berry' kutoka Kenya.

Samata, Ulimwengu waiongezea nguvu Stars

Washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaocheza mpira wa kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamejiunga na kambi ya timu ya Taifa (Taifa Stars) juzi. Wachezaji hao ambao ndiyo pekee kutoka nje walioitwa na Kocha Kim Poulsen kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika dhidi ya Ivory Coast itakayochezwa Juni 2 mwaka huu jijini Abidjan waliwasili juzi saa 1.30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways. Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaendelea na mazoezi jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya Karume na Taifa itacheza mechi ya kirafiki Mei 26 mwaka huu dhidi ya Malawi. Mechi hiyo itafanyika Uwanja wa Taifa, na Malawi itawasili nchini Mei 24 mwaka huu. Baadaye Malawi itakwenda Zanzibar kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Zanzibar Heroes itakayofanyika Mei 28 mwaka huu kabla ya kuondoka Mei 30 mwaka huu kwenda Uganda ambapo Juni 2 mwaka huu itcheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika. Katika hatua nyingine, kiungo wa timu hiyo, Nurdin Bakar atalikosa pambano la kirafiki dhidi la Malawi kutokana na kuchanika nyama ya paja hali inayomfanya awe nje kwa wiki moja kabla ya kurejea tena dimbani. Bakari, alipata majeraha hayo katika mazoezi ya timu hiyo inayoendelea kujivua kwenye viwanja vya Karume, Ilala Dar es Salaam.

Azam yapewa 'shavu' Kagame Cup

WASHINDI wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam FC watashiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame Julai, mwaka huu, Dar es Salaam, imeelezwa. Kuingia kwa Azam kwenye michuano hiyo, iliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1974, kunamaanisha Tanzania Bara, wenyeji watawakilishwa na timu tatu, nyingine zikiwa ni mabingwa watetezi wa Kombe hilo, Yanga na mabingwa wa Ligi Kuu, Simba SC. Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema jana mjini Dar es Salaam kwamba maandalizi ya michuano hiyo, yanaendelea vizuri na tayari wadhamini wamekwishapatikana na watatangazwa katika Mkutano maalum hivi karibuni. Azam inayoshikilia pia taji la Kombe la Mapinduzi, itakuwa ni mara yao ya kwanza kushiriki michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Timu nyingine za Tanzania Bara zitakazoshiriki michuano hiyo ni mabingwa watetezi wa taji hilo, Yanga na mabingwa wapya wa Tanzania, Simba.