STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 19, 2011

Nyalawila apigiwa debe, Cheka ajipanga





MAPROMOTA wa Ngumi za Kulipwa nchini, wameombwa kujitokeza kumuandalia pambano la utetezi Bingwa wa Dunia wa WBF, Karama Nyalawila, ili asipoteze taji hilo.
Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBO, Yasin 'Ustaadh' Abdalla, alisema ili kumuepushia Nyalawila asipoteze taji lake alilotwaa mwishoni mwa mwaka jana nchini Ukraine ni vema mapromota wakajitokeza kumuandalia pambano la utetezi.
Ustaadh, alisema kwa kanuni zilizopo katika mchezo huo, bingwa yeyote akikaa muda mrefu bila kupigana, hupoteza sifa ya kushikilia taji na hivyo anahofia yasije yakamkuta Nyalawila.
"TPBO tunawaomba waratibu wa michezo ya ngumi za kulipwa nchini kumuandalia pambano Nyalawila ili kutetea taji na kuepuka kulipoteza taji hilo lenye hadhi kubwa katika mchezo huo duniani," alisema Usraadh.
Rais huyo alisema oganaizesheni yake ipo tayari kufanya kazi na promota yeyote atakayekuwa tayari kumuandalia bingwa huo wa WBF pambano hilo kwa lengo la kutaka Tanzania iendelee kung'ara kimataifa.
Alisema kwa kitambo kirefu mabondia wa Tanzania wameshindwa kung'ara kimataifa na hivyo ni vema Nyalawila, Francis Cheka na wengine wanaoshikilia mataji wakawa wanapewa kipaumbele kuandaliwa michezo.
Katika hatua nyingine, bingwa wa dunia wa WBC, UBO, ICB, Francis Cheka, anajifua kujiandaa na pambano lake la kuwania taji la IBF litakalofanyika April 2, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Micharazo toka Morogoro, Cheka, alisema pambano lake litafanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee na atapigana na Mmarekani, Marcus Upshaw.
"Natarajia kupanda ulingoni April 2 kwa kuzichapa na Mmarekani ambaye jina lake limenitoka, katika kuwania mkanda wa IBF uzito wa kilo 72," alisema.
Hilo litakuwa pambano la kwanza kwa Cheka tangu alipomshindwa kwa pointi Bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Mada Maugo katika pambano lisilo la mkanda lililochezwa Januari Mosi, kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar.

Mwisho

Msama Promotion yawasaidia Wahanga wa Mabomu Gongo la Mboto






WAHANGA wa milipuko ya mabomu yaliyotoka eneo la Gongo la Mboto, wameendelea kupewa misaada, baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka nchini, Alex Msama kutoa misaada ya vyakula.
Misaada hiyo yenye thamani ya karibu Sh. Mil. 3, ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Msama kupitia kituo cha runinga cha Cloud's, kwa lengo la kufikishwa kwa waathirika na milipuko hiyo iliyotokea katikati ya wiki kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania, JWTZ, kikosi cha 521 KJ.
Msama alisema kama sehemu ya jamii walioguswa na tukio la milipuko hiyo ya mabomu wameamua kutoa misaada hiyo kuitikia wito wa serikali, huku akiwahimiza watu wengine wenye uwezo kufanya hivyo.
"Tusiiachie serikali pekee yake kufanya kazi hii, ndio maana sisi kama sehemu ya jamii tumeamua kutoa msaada huu japo mdogo, lakini uwasaidie wenzetu walioathirika na tukio hilo linalosikitisha," alisema Msama.
Msaada huo uliotolewa ni magunia manne ya Mchele, Unga wa Ngano gunia 10, gunia mbili za Maharage na Sukari pamoja na ndoo mbili za mafuta ya Gunia za maharage na ndoo mbili za mafuta ya kupikia.
Msama alisema, pamoja na msaada huo, kamati yao inafanya mipango zaidi ya kuongeza misaada yao kwa wahanga hao kwa nia ya kuisaidia serikali na asasi nyingine zilizojitolea kwa hali na mali kuwafariji waathirika wa mabomu hayo.
Tukio la ulipukaji wa mabomu la Gongo la Mboto ni la pili katika kipindi cha karibu miaka miwili, baada ya awali kulipuka April 29, mwaka juzi kambi nyingine ya jeshi eneo la Mbagala, pia jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo la pili, karibu watu 20 wakiwemo watoto wameripotiwa kupotea uhai wao, huku wengine wanaokadiriwa kufikia 400 wakijeruhiwa, mbali na kusababisha uharibifu wa mali na miundo mbinu kadhaa.
Tayari serikali imetangaza kuwalipa fidia wote walioathirika na tukio hilo, ambalo lilitokea majira ya usiku, siku ya Jumatano na kuleta taharuki kwa wakazi wengi wa jijini na wale wa mikoani.

Mwisho