STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 19, 2011

Msama Promotion yawasaidia Wahanga wa Mabomu Gongo la Mboto






WAHANGA wa milipuko ya mabomu yaliyotoka eneo la Gongo la Mboto, wameendelea kupewa misaada, baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka nchini, Alex Msama kutoa misaada ya vyakula.
Misaada hiyo yenye thamani ya karibu Sh. Mil. 3, ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Msama kupitia kituo cha runinga cha Cloud's, kwa lengo la kufikishwa kwa waathirika na milipuko hiyo iliyotokea katikati ya wiki kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania, JWTZ, kikosi cha 521 KJ.
Msama alisema kama sehemu ya jamii walioguswa na tukio la milipuko hiyo ya mabomu wameamua kutoa misaada hiyo kuitikia wito wa serikali, huku akiwahimiza watu wengine wenye uwezo kufanya hivyo.
"Tusiiachie serikali pekee yake kufanya kazi hii, ndio maana sisi kama sehemu ya jamii tumeamua kutoa msaada huu japo mdogo, lakini uwasaidie wenzetu walioathirika na tukio hilo linalosikitisha," alisema Msama.
Msaada huo uliotolewa ni magunia manne ya Mchele, Unga wa Ngano gunia 10, gunia mbili za Maharage na Sukari pamoja na ndoo mbili za mafuta ya Gunia za maharage na ndoo mbili za mafuta ya kupikia.
Msama alisema, pamoja na msaada huo, kamati yao inafanya mipango zaidi ya kuongeza misaada yao kwa wahanga hao kwa nia ya kuisaidia serikali na asasi nyingine zilizojitolea kwa hali na mali kuwafariji waathirika wa mabomu hayo.
Tukio la ulipukaji wa mabomu la Gongo la Mboto ni la pili katika kipindi cha karibu miaka miwili, baada ya awali kulipuka April 29, mwaka juzi kambi nyingine ya jeshi eneo la Mbagala, pia jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo la pili, karibu watu 20 wakiwemo watoto wameripotiwa kupotea uhai wao, huku wengine wanaokadiriwa kufikia 400 wakijeruhiwa, mbali na kusababisha uharibifu wa mali na miundo mbinu kadhaa.
Tayari serikali imetangaza kuwalipa fidia wote walioathirika na tukio hilo, ambalo lilitokea majira ya usiku, siku ya Jumatano na kuleta taharuki kwa wakazi wengi wa jijini na wale wa mikoani.

Mwisho

No comments:

Post a Comment