STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 10, 2014

Muumin airejesha tena Double M Sound

* Alihama jiji kujichimbia Kahama
* Ambeba Ally Akida 'Tetenasi'
Mwinjuma Muumin 'Kocha wa Dunia' akizungumza leo jijini Dar
"Siyo lazima watu wote tuwe Dar, tutakuwa tunakuja kurekodi au kufanya maonyesho Dar lakini kwetu Kahamaaaa"
Waimbaji mpya wa Double M Sound, Furaha Mkwama na Vampire wakiwapa vionjo wanahabari (hawapo pichani)
Furaha (kushoto) achana naye ana sauti siyo mchezo...!
Muimbaji mwingine mpya, Shazi (kulia) akitoa vionjo huku akiangaliwa na Vampire, Muumin na Drumer Boy, Chocholii
Shazii akiendelea kuonyesha maujuzi yake
Muumin akifafanua jambo
Vampire
Sehemu ya kikosi kipya cha Double M Sound wakishoo baada ya mkutano wa pamoja
Vampire
Chocholii
Chocholii na Queen Vero unamkumbuka mnenguaji huyu...naye ndani ya nyuma
Furaha Mkwama katika pozi, mdada huyu nouma kwa sauti
Siyo sauti tu, bali hata mvuto wa sura na umbo hajamboo!
Mimi ndiye Chocholii Machine a.k.a Drumer Boy
NYOTA wa muziki dansi nchini, Mwinjuma Muumin 'Prince' a.k.a Kocha wa Dunia ametangaza rasmi kuirejesha bendi yake ya zamani ya Double M Sound 'Wana Mshikemshike' lakini wakilihama jiji la Dar es Salaam na kutua mjini Kahama, mkoani Shinyanga.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Muumin alisema ameamua kwenda kujichimbia Kahama, baada ya kubaini mjini huko ndiko penye mafao ya kutosha na mahali pa kurejesha heshima mjini baada ya kitambo kirefu cha ukimya wake.
Muumin anayefahamika pia kama Mzee wa Chelsea, alisema bendi yake hiyo mpya itaundwa na wanamuziki 14 na mafundi mitambo wawili ambao baadhi ya wanamuziki hao  walitambulishwa kwa wanahabari katika mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Vijana Social.
"Baada ya kutafakari kwa kina na hasa baada ya kupokewa vyema na wakazi wa Shinyanga, nimeamua kuirejesha Double M Sound na tunatarajia kuondoka asubuhi ya kesho kwenda kuweka makazi ya kudumu tukiwa tumekamilika," alisema.
Alisema wataanza kuwasha moto kuelekea kwenye sikukuu ya Pasaka kwa kufanya onyesho lao la kwanza April 18 katika ukumbi wa The Dreams, uliopo Kakola machimboni Kahama kabla ya kuelekea Ngara kuwasha moto siku inayofuata kwenye ukumbi wa City Center.
"Baada ya hapo siku ya Pasaka tutakuwa ukumbi wa Manispaa huko Kibondo mkoani Kigoma na kumaliza burudani yetu siku ya Jumatatu ya Pasaka, FM Hall, Kasulu na kurejea Kahama kujifua kwa mazoezi kabla ya kuingia studio kurekodi nyimbo zetu za kwanza," alisema.
Muumini alisema Double M itazitumia nyimbo zote za zamani na zile mpya ambazo amezitunga na kuziimba katika bendi mbalimbali wakati wakijipata kutoa kazi mpya na kudai kitu kipya cha kuanzia kitakuwa 'Utafiti wa Mapenzi'.
Muumin alisema hakuona haja ya kutafuta jina jipya katika ujio wake mpya wakati Doun]ble M Sound ilikuwapo na ilijijengea jina kubwa kabla ya kuzimika baada ya uzinduzi wa albamu ytake ya 'Titanic'.
Juu ya kikosi chake, Muumin alisema kwenye safu ya uimbaji yupo yeye mwenyewe kama nahodha akisaidiana na Richard Magige, Sherri 'Shazi' Abubakar na wadada Furaha Mkwama na Nana Mwashauya 'Vampire'.
"Kwenye solo yupo Ally Akida 'Tetenasi' ambaye pia hupiga Rhythm atakalosaidiana na David Shidodo ambaye pia hupiga besi kumsaidia mcharaza gitaa hilo zito, Said Bell, huku mpapasa kinanda ni Pascal Kiinuka na tumba yupo Husseni Ngalawa na drum kuna Chocholii Machine.

Ramsey kuivaa Wigan FA Cup

http://i.telegraph.co.uk/multimedia/archive/01738/aaron_ramsey_1738865c.jpg
MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amethibitisha kuwa Aaron Ramsey yuko tayari kuanza katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Wigan Athletic Jumamosi. 
Kiungo amekuwa nje ya uwanja toka Desemba 26 mwaka jana kutokana na majeraha ya msuli lakini aliingia kama mchezaji wa akiba katika kipindi cha pili kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Everton Jumapili iliyopita.
Wakati huohuo, Mesut Ozil na Laurent Koscielny wote hawatakuwepo katika mchezo huo utakaochezwa Wembley wakati Kieran Gibbs, Tomas Rosicky na Alex Oxlade Chamberlain nao wakiwa katika hatihati ya kuukosa mchezo huo kutokana na majeruhi. 
Wenger amesema Ramsey yuko tayari kuanza katika mchezo dhidi ya Wigan lakini ana wasiwasi na Gibbs, Rosicky na Oxlade-Chamberlain kama watakuwa tayari kwa ajili ya mchezo huo. 
Kocha huyo aliendelea kudai kuwa anategemea kila mchezaji atatoa mchango wake kwasababu wana uzoefu wa kutosha na wamecheza mechi kubwa zaidi ya hiyo katika michuano ya FA.

Pigo Real Madrid kuivaa Barca bila Ronaldo

Ronaldo
KLABU ya Real Madrid imepata pigo kufuatia habari kuwa Cristiano Ronaldo anaweza akaukosa mchezo wa fainali ya Kombe la Mfalme dhidi ya Barcelona wiki ijayo kutokana na majeraha ya msuli. 
Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno alitolewa nje katika dakika za mwisho katika mchezo dhidi wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund ambao Madrid walishinda 3-0. 
Majeruhi yamepelekea nyota huyo kupumzishwa katika mchezo wa La Liga dhidi ya Real Sociedad na alikuwa mchezaji wa akiba asiyetumika katika mchezo wa marudiano dhidi ya Dortmund ambao Madrid walichapwa kwa mabao 2-0. 
Sasa imethibitika kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 kwamba ameumia msuli wa paja la mguu wake wa kushoto na kuna uwezekano akakaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki mbili hivyo kuukosa mchezo huo wa muhimu wa Kombe la Mfalme Jumatano ijayo.

Tanzania yazidi kuporomoka FIFA

Taifa Stars
LICHA ya kuambulia sare ya 1-1 ugenini na Namibia mwezi uliopita, Tanzania imezidi kuporomoka kwenye orodha ya viwango vya soka vya FIFA baada ya kushuka kwa nafasi tano toka nafasi yake ya awali.
Baada ya kuteleza kwa nafasi moja mwezi uliopita, Tanzania imeanguka tena kwa nafasi tano na kukamata nafasi ya 122 katika viwango vya soka vya dunia vya kila mwezi vilivyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) jana.
Tanzania iliyotoka sare ya bao 1-1 ugenini katika mechi iliyopita ya kirafiki dhidi ya Tunisia, sasa inakamata nafasi ya 37 barani Afrika huku ikishika nafasi ya tatu Afrika Mashariki na Kati, na nafasi ya nne katika Ukanda wa Cecafa wa Afrika Mashariki na Kati.
Hispania imeendelea kuongoza 10 bora ikifuatwa na Ujerumani, Ureno, Colombia, Uruguay, Argentina, Brazil, Uswisi, Italia na Ugiriki.
10 bora barani Afrika inaongozwa na Ivory Coast iliyoko nafasi ya 21 duniani ikifuatwa na Misri (24), Algeria (25), Ghana (38), Cape Verde (42), Nigeria (45), Tunisia (49), Cameroon (50), Guinea (51) Mali inayokamata nafasi ya 59 duniani.
Uganda iliyoshuka kwa nafasi moja, bado inaongoza Ukanda wa Cecafa ikiwa nafasi ya 18 Afrika na 86 duniani, ikinyemelewa na Ethiopia (27 Afrika, 101 duniani), Kenya (29/106), Sudan (33/117), Tanzania, Burundi (38/125), Rwanda (39/129), Shelisheli (48/177), Eritrea (51/200), Sudan Kusini (52/201), Somalia (53/202) na Djibout inayofunga pazia Afrika ikiwa nafasi ya 204 duniani.

Azam yakata tiketi ya CAF, Ruvu kumbe debe tupu!

Azam ilipokuwa ikishiriki Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza mwaka jana
KLABU ya soka ya Azam imekuwa klabu ya kwanza kukata tiketi ya michuano ya CAF baada ya jioni yua leo kuifumua timu ya Ruvu Shooting kwa mabao 3-0 na kubakisha hatua chache kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mabao ya kipindi cha kwanza yaliyowekwa kimiani na Gaudence Mwaikimba katika dakika ya 8 kwa kichwa na jingine na dakika ya 37 kupitia Himid Mao, yaliifanya Azam iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Mu Ivory Coast, Kipre Tchetche akipigilia msumari wa mwisho sekunde chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili katika jeneza la Ruvu iliyokuwa imetamba kuwa ya kwanza kuwatungua Azam ambayo imecheza mechi 24 bila kupotea hata mchezo mmoja baada ya kufunga bao la tatu.
Kwa ushindi huo Azam imefikisha pointi 56 ambazo haziwezi kufikiwa na klabu yoyote ya Ligi Kuu zaidi ya Yanga waliopo nafasi ya pili na pointi 52.
Ushindi huo pia, umeifanya timu hiyo kukaribia kutwaa taji hilo kwani imesaliwa na mechi moja tu kati ya mbili kuweza kutangazwa kuwa bingwa kwa mara ya kwanza katika ligi hiyo na piaa kuweza kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuiwakilisha mara Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Uhakika wa Azam kuwa bingwa au la itafahamika Jumapili watakapoifuata Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati Yanga watakaribishwa na Oljoro JKT jijini Arusha.

Azam kuzidi kuiacha Yanga leo?

* Inapepeta na Ruvu mechi ya kiporo
Azam
Ruvu Shooting inayowania kuwepo kwenye Top 5
 AZAM ina nafasi ya kuzidi kuiacha mbali Yanga wakati leo itakaposhuka dimbani kucheza mechi yake ya kiporo dhidi ya Ruvu Shooting baada ya mvua kubwa iliyonyesha jana kuuzuia mchezo huo kufanyika kama ulivyokuwa umepangwa.
Yanga jana ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na kupunguza pengo la pointi kutoka nne hadi moja na kufufua matumaini ya kutetea taji hilo, ambapo leo itakuwa na kazi kubwa ya kuiombea mabaya wapinzani wao hao walale kwa maafande wa Ruvu ili kujiweka pazuri.
Azam wanaoongoza msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 53, Yanga wakiwafuata wakiwa na pointi 52 baada ya ushindi huo wa jana, lakini pengo linaweza kuongezeka kama Azam itashinda kwa maafande hao ambao hawajapoteza mchezo kwenye dimba la nyumbani msimu huu.
Ruvu kupitia Msemaji wake, Masau Bwire amesisitiza kuwa, wao ndiyo watakaokuwa wa kwanza kuwatengua 'udhu' Azam kwa kuwanyuka baada ya klabu nyingine 12 kushindwa kufanya hivyo mpaka sasa.
Bwire mmoja wa wasemaji wenye mvuto kwa vyombo vya habari, alisema kuahirishwa kwa mchezo huo jana kwa sababu ya mvua haina maana kama Azam wamepona bali wameahirishwa adhabu leo na kudai itakuwa maradufu zaidi na walivyopanga.
Alisema timu yao inapigana kuingia kwenye Top 4 kwani kama itashinda leo itaishusha Kagera Sugar kwa kufikisha pointi 35, mbili zaidi na ilizonazo Simba waliopo nafasi ya nne kwa muda mrefu.
Hata hivyo viongozi wa Azam wakiongozwa na Katibu Mkuu wake, Idrissa Nassor 'Father' amesema bayana kwamba wao lengo lao ni kutwaa taji hivyo hawajali kama wanacheza ugenini au nyumbani vipigo wanagawa sawasawa.
Baada ya mechi hiyo ya leo Azam itasafiri kuelekea Mbeya kwa ajili ya kuwahi pambano lao na Mbeya City wanaokamata nafasi ya tatu, huku Yanga wenyewe watawafuata Oljoro JKT katika mechi itakayopigwa Jumapili kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Siku hiyo pia kutakuwa na mechi nyingine kadhaa ikiwamo ya Simba dhidi ya Ashanti United, na Mgambo Shooting kupepetana na Kagera Sugar uwanja wa Mkwakwani-Tanga.

Danny Lyanga ajinadi Simba na Yanga

Danny Lyanga (kulia) akikokota mpira katika mechi ya Ligi Kuu
MSHAMBULIAJI nyota wa Coastal Union, Danny Lyanga amesema yupo tayari kutua katika klabu za Simba, Yanga au Azam iwapo zitakuwa zimevutiwa na kumhitaji kuzichezea kwani yeye 'habagui'.
Mfungaji Bora huyo wa Coastal kwa msimu uliopita alipofunga mabao saba, anasema soka ndiyo kila kitu kwake hivyo hana jeuri ya kuchagua timu ya kuichezea kama itamvutia kimasilahi.
Lyanga ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji walioirejesha Coastal kwenye Ligi Kuu misimu miwili iliyopita, alisema wapo baadhi ya watu huwatia hofu wachezaji kujiunga na klabu kubwa.
Lakini kwake yeye hawezi kutishwa na hofu ya kuuliwa kipaji chake kwa kujiunga na timu hizo kubwa kwa madai anajiamini uwezo mkubwa alionao katika kusakata kandanda.
"Kokote nipo tayari kucheza, ninachoangalia ni masilahi kwa vile soka la sasa ni ajira, hivyo wachezaji hatupaswi kuchagua timu za kuzichezea kwa kisingizio cha mapenzi kwani ni kujitia umaskini."
Lyanga alisema na kuongeza, kuendekeza mapenzi katika soka ndicho kilichosababisha baadhi ya mastaa wa zamani kufa maskini kwa kuhofia kuhamia kwingine hata kama kuna masilahi zaidi.
"Siangalii timu kwangu masilahi kwanza kwa vile maisha yangu ya baadaye yapo mikononi mwangu mwenyewe, nikizembea kidogo inaweza kula kwangu na hatimaye kuja kuchekwa," anasema.
Kumekuwa na dhana mbaya kwa baadhi ya mashabiki na wachezaji wakitishika wachezaji chupukizi kujiunga na klabu kubwa wakiamini wataua vipaji vyao, ingawa hakuna ukweli wowote.

Man U yafa Ujerumani, Barce aibu tupu kwa Atletico Madrid

Franck Ribery akipiga shuti langoni mwa Manchester United
Bayern Munich
Oyooo bayern Munich wakishangilia ushindi wao dhidi ya Mashetani wekundu ambao wachezaji wake (kushoto) wakiwa katika simanzi
Neymar akiipigania Barcelona mbele ya wachezaji wa Atletico Madrid
Koke scores for Atletico Madrid v Barcelona
Koke akiifungia Atletico bao pekee
BAO pekee lilifungwa katika dakika tano na Koke lilitosha kuitoa nishai Barcelona katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuivusha Atletico Madrid katika Nusu Fainali ya michuano hiyo huku Manchester United ikishindiliwa mabao 3-1 na Bayern Munich na kung'olewa michuanoni.
Koke alifunga bao hilo akimalizia krosi ya Adrian na kuwafanya vinara wa Ligi ya Hispania kuiondosha Barcelona kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya mechi ya awali kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Atletico sasa inaungana na timu za Real Madrid, Chelsea na Bayern Munich iliyoifumua Manchester United kwa mabao 3-1 na sasa wanasubiri droo ya kujua nani atacheza na nani katika hatua hiyo.
Katika mechi ya mjini Munich, Ujerumani wenyeji na mabingwa watetezi wa michuano hiyo walikunjua makucha yao kwa Mashetani Wekundu kwa kuifumua mabao 3-1, baada ya mechi yao ya awali kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
United ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 57, mfungaji beki wake Mfaransa, Patrice Evra aliyefumua shuti kali kwa guu la kushoto baada ya kupokea pasi ya Antonio Valencia.
Hata hivyo wenyeji walilisawazisha bao hilo sekunde 22 baadaye kupitia kwa Mario Mandzukic baada ya kutumia fursa ya wachezaji wa United kufurahia bao lao.
Thomas Muller aliifungia  Bavarian bao la pili dakika ya 68 kwa pasi ya Arjen Robben ambaye katika mchezo wa jana aliisumbua ngome ya Mashetani kabla ya kufunga mwenyewe katika dakika ya 76 na kuzima ndoto za vijana wa David Moyes kufanya maajabu kwenye michuano hiyo ya Ulaya.