STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 10, 2014

Azam kuzidi kuiacha Yanga leo?

* Inapepeta na Ruvu mechi ya kiporo
Azam
Ruvu Shooting inayowania kuwepo kwenye Top 5
 AZAM ina nafasi ya kuzidi kuiacha mbali Yanga wakati leo itakaposhuka dimbani kucheza mechi yake ya kiporo dhidi ya Ruvu Shooting baada ya mvua kubwa iliyonyesha jana kuuzuia mchezo huo kufanyika kama ulivyokuwa umepangwa.
Yanga jana ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na kupunguza pengo la pointi kutoka nne hadi moja na kufufua matumaini ya kutetea taji hilo, ambapo leo itakuwa na kazi kubwa ya kuiombea mabaya wapinzani wao hao walale kwa maafande wa Ruvu ili kujiweka pazuri.
Azam wanaoongoza msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 53, Yanga wakiwafuata wakiwa na pointi 52 baada ya ushindi huo wa jana, lakini pengo linaweza kuongezeka kama Azam itashinda kwa maafande hao ambao hawajapoteza mchezo kwenye dimba la nyumbani msimu huu.
Ruvu kupitia Msemaji wake, Masau Bwire amesisitiza kuwa, wao ndiyo watakaokuwa wa kwanza kuwatengua 'udhu' Azam kwa kuwanyuka baada ya klabu nyingine 12 kushindwa kufanya hivyo mpaka sasa.
Bwire mmoja wa wasemaji wenye mvuto kwa vyombo vya habari, alisema kuahirishwa kwa mchezo huo jana kwa sababu ya mvua haina maana kama Azam wamepona bali wameahirishwa adhabu leo na kudai itakuwa maradufu zaidi na walivyopanga.
Alisema timu yao inapigana kuingia kwenye Top 4 kwani kama itashinda leo itaishusha Kagera Sugar kwa kufikisha pointi 35, mbili zaidi na ilizonazo Simba waliopo nafasi ya nne kwa muda mrefu.
Hata hivyo viongozi wa Azam wakiongozwa na Katibu Mkuu wake, Idrissa Nassor 'Father' amesema bayana kwamba wao lengo lao ni kutwaa taji hivyo hawajali kama wanacheza ugenini au nyumbani vipigo wanagawa sawasawa.
Baada ya mechi hiyo ya leo Azam itasafiri kuelekea Mbeya kwa ajili ya kuwahi pambano lao na Mbeya City wanaokamata nafasi ya tatu, huku Yanga wenyewe watawafuata Oljoro JKT katika mechi itakayopigwa Jumapili kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Siku hiyo pia kutakuwa na mechi nyingine kadhaa ikiwamo ya Simba dhidi ya Ashanti United, na Mgambo Shooting kupepetana na Kagera Sugar uwanja wa Mkwakwani-Tanga.

No comments:

Post a Comment