STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, March 30, 2014

JKT Ruvu yazidi kudimiza Rhino Rangers

JKT Ruvu
MAAFANDE wa JKT Ruvu chini ya kocha wao Fred Felix 'Minziro' wametoa kipigo kitakatifu kwa Rhino Rangers na kuzidi kuizamisha kwenye tope la kushuka daraja katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mchezo uliochezwa uwanja wa Chamazi.
Wenyeji JKT Ruvu ilianza kuandika bao la kwanza dakika za mapema kupitia kwa Idd Mbaga kabla ya Emmanuel Switta kuongeza bao la pili kwa mkwaju wa penati baada ya Sosteness Manyasi kuchezwa rafu na mabeki wa maafande hao wa JWTZ kutoka Tabora na kuifanya Ruvu iendee mapumziko ikiwa 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Rhino kupata penati iliyofungwa na Gideon na Ruvu kuongeza bao la gtatu kupitia kwa Samuel Kamutu na kuifanya timu ya Ruvu kufikisha jumla ya pointi 28 na kujiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuepuka janga la kushuka daraja msimu huu wakiwa na michezo mitatu mkononi.

Liverpool yaifumua Spurs na kukaa kileleni

Luis Suarez
Suarez akifunga bao lake la 29 katika ligi kwa msimu huu wakiizamisha Spurs kwa 4-0
VIJOGOO wa Anfield, Liverpool imekwea hadi kileleni mwa Ligi Kuu ya England wakiiporomosha Chelsea baada ya kuifumua bila huruma Tottenham Hotspur iliwatembelea kwenye uwanja wao.
Liverpool iliitambia vijogoo wenzao wa London kwa kuwakandika mabao 4-0, na kuwafanya wafikishe jumla ya pointi 71, mbili zaidi ya Chelsea ambao jana walifumuliwa bao 1-0 na Crystal Palace.
Wageni walianza kujitabiria janga baada ya Younes Kaboul kujifunga dakika ya pili ya mchezo kabla ya Luis Suarez kuandika bao la pili dakika ya 25 na wenhyeji kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Liverpool kuandika bao la tatu kupitia kwa Phillipe Countinho dakika ya 55 kabla ya Jordan Henderson katika dakika ya 75 na kuifanya Liverpool kukalia kiti cha uongozi kilaini.

Inauma! Ajali yaua waombolezaji 12


WATU 12 waliokuwa njiani kwenda kuomboleza msiba wa mtoto aliyepoteza maisha baada ya kusombwa na mafuriko, wamefariki dunia na wengine saba wamejeruhiwa, baada ya gari lao kugongwa na malori mawili kwa wakati mmoja.
Abiria hao walikuwa wanasafiri na gari dogo aina ya Toyota Pick Up namba T 170 AKZ kwenda kuhani msiba uliotokea katika kijiji cha Kongei kilichoko Hedaru mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro , Robert Boaz waliofariki ni Stella John (45), Salma Kizoka (33), Marry Senzige (49), Neema Daniel (52), Rehema George, (29), Sophia Mbike (51), Ritta Kallani (55) na Kallan Stephano (55), Kolina Mmasa (55) na Bahati Daudi (25),

Wengine ni Farida Kiondo (24) na Maria John (33) wote wakazi wa Kongei na kwamba miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya Wilaya ya Same.

Boaz aliwataja majeruhi kuwa ni Zubeda Mrindoko (42),Mipa Chediel (29) na Zubeda Mlita (32) ambao wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC kutokana na hali zao kuwa mbaya zaidi.

Wengine waliolazwa hospitalini Same ni Joyce Kandogwe (29), Subira Juma (22), Ramadhan Msangi (31) na Adinan Rajab (31).

Ajali hiyo ilitokea juzi saa 2:00 usiku katika barabara kuu ya Tanga-Moshi, nje kidogo ya mji wa Hedaru, ikihusisha magari matatu ambayo ni Fuso (T 299 ANM) ikitokea Moshi kwenda Dar es Salaam na Scania (T 737 AKW) pamoja na tela lake namba T 776 CCN ikitokea Dar es Salaam kwenda Moshi, kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi.

Alisema watu hao walikuwa wamepanda gari la Diwani wa Kata ya Hedaru (CCM), Gerald Gwena aliyekuwa amewapakia waombolezaji hao kwenye pick-up yake ambayo iligongwa kwa nyuma na Fuso na baadaye gari hilo kuparamiwa kwa nyuma na Scania na kisha kusababisha vifo na majeruhi.

"Waombolezaji hawa walikuwa wanakwenda na diwani kuifariji familia ya marehemu mzee Mwanga ambaye mtoto wake wa kiume, Dismas Mwanga alifariki baada ya kusombwa na mafuriko”, alisema.

Alisema Dismas mwenye miaka tisa aliyekuwa anachunga kondoo milimani alifariki dunia juzi mchana baada ya kusombwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zilizonyesha mfululizo.

Alisema hata, hivyo mpaka sasa haijafahamika iwapo mvua hizo zimesababisha vifo na hasara nyingine.

Kapufi alisema kamati yake ya ulinzi na usalama imekutana kwa dharura kujadili ajali hiyo na hatua ambazo wilaya hiyo itachukua.

Kamanda Boaz, alisema chanzo cha ajali hiyo ni kuzimika ghafla kwa  gari hilo mali ya diwani Gwena ambaye alikimbia baada ya ajali hiyo.

"Ajali hiyo ilitokea baada ya gari hilo kuzimika na Fuso iliyokuwa karibu kuteleza barabarani baada ya kujaribu kusimama ili isigongane na Pick Up iliyokuwa na waombolezaji, lakini lilivutwa na tope lililokuwa limejaa barabarani kisha kugonga kabla ya kupinduka na kuangukia upande wa kulia wa barabara ambako kulikuwa na lori la Scania.

Kamanda alisema watu 10 walikufa papo hapo , wawili walifia hospitalini na saba wamejeruhiwa.
Alisema juhudi za kuwasaka madereva  hao wa Fuso pamoja na diwani huyo zinaendelea.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Mbeya City yainyuka Prisons, Mtibwa yaifumua Coastal 3-1

Mbeya City
Mtibwa Sugar iliyoitungua Coastal kwa mabao 3-1
BAO pekee lililofungwa katika dakika ya pili ya mchezo na Paul Nonga, lilitosha kuipa ushindi muhimu Mbeya City dhidi ya mahasimu wao Prisons na kuipumulia Yanga kisogoni kwenye mbio za kuwania nafasi mbili za juu za Ligi Kuu Tanzania bara msimu huu.
Pambano hilo lililochezwakwenye uwanja wa Sokoine lilikuwa la vuta nikuvute, lakini ni Mbeya waliondeleza ubabe kwa wajelajela hao kwa kuwalaza kwa mara nyingine katika msimu wao wa kwanza wa ligi hiyo baada ya mchezo wa kwanza kuwanyuka 2-0.
Kwa ushindi huo Mbeya City imefikisha pointi 45 moja pungufu na Yanga waliolala 2-1 Mkwakwani Tanga dhidi ya Mgambo JKT.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa uwanja wa Manungu, Mtibwa Sugar ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wageni wao Coastal Union.
Mabao ya washindi katika mchezo huo yalifungwa na Jamal Mnyate dakika ya 14 kabla ya Coastal kusawazisha kupitia kwa Mbwana Hamis na Mussa Hassan kuipa uongozi wa 2-1 Mtibwa hadi wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili wenyeji waliongeza bao la tatu dakika nane kabla ya mchezo huo kuisha kupitia kwa Mohammed Mkopi aliyemalizia kazi nzuri ya Mgosi aliyekuwa nyota wa pambano hilo. Mtibwa kwa ushindi huo imefikisha pointi 31.
Nazo timu za Kagera Sugar na Ruvu Shooting zilishindwa kutambiana baada ya kushindwa kufungana katika pambano lililochezwa kwenye uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, na maafande wa JKT Ruvu wakiwa uwanja wa Chamazi wameichezeshwa kwata Rhino Rangers ya Tabora kwa kuwalaza mabao 3-1 na kuiweka mguu mmoja katika kaburi la kushuka daraja na kurudi Ligi daraja la Kwanza msimu ujao.

Wababe wa Chuoni watupwa Kombe la Shirikisho

http://cdn.pmnewsnigeria.com/wp-content/uploads/2014/03/Bayelsa-United-Team.jpg
Timu ya Bayelsa United ya Nigeria iliyoping'oa How Mine ya Zimbabwe,
WABABE wa Chuoni ya Zanzibar, How Mine ya Zimbabwe imeshindwa kuendelea kutamba katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kukwama kwa Bayelsa United ya Nigeria.
Timu hiyo jana ilikubali kipigo cha mabao 2-0 ugenini, baada ya awali kushindwa nyumbani kwao 2-1 na kuwaacha wapinzani wao wakitinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika ngazi za klabu.
Katika mechi nyingine wawakilishi pekee wa ukanda wa CECAFA, AS Kigali jana iling'oka kwenye michuano hiyo baada ya kukumbana na kipigo cha mabao 3-0 toka kwa Difaa el Jadida ya Morocco.
Kabla ya kipigo hicho Wanyarwanda hao walishinda nyumbani bao 1-0 na hivyo kutolew akwa jumla ya mabao 3-1 na kurejea Kigali kujipanga upya kwa msimu ujao.
Mabingwa wa zamani wa Afrika, Etoile Sahel ya Tunisia ilifanya kufuru baada ya kuibamiza Super Sport United ya Afrika Kusini nyumbani kwao kwa mabao 4-1, wiki moja baada ya kuitambia 1-0 mjini Tunis.
Etoile imesonga mbele kwa jumla ya mabao 5-1, huku Supersport wakitulia na kuendelea na michuano ya Ligi Kuu nchini mwao.
Mechi nyingine za kukamilisha ratiba ya hatua ya 16 Bora zinachezwa jioni hii.

Al Ahly wavuliwa taji Afrika, Vita kama TP Mazembe

Al Ahly waliokuwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika waliotemeshwa taji jana
MABINGWA watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri wametemeshwa taji hilo baada ya jana kupokea kipigo cha mabao 3-2 na Al Ahly Benghazi ya Libya.
Watetezi wao walioiondosha Yanga katika hatua ya 32 Bora kwa mikwaju ya penati ilikumbana na kipigo hicho cha aibu nyumbani kwao na kushindwa kuingia hatua ya makundi.
Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo, Al Ahly ya Misri ilifungwa 1-0 na Walibya ugenini na hivyo kung'olewa michuanoni kwa jumla ya mabao 4-2.
Katika mechi nyingine AS Vita ya DR Congo imefuzu hatua ya makundi kuungana na ndugu zao wa TP Mazembe waliofanya hivyo jana licha ya kufungwa 2-0 ugenini na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Vita ilishinda mechi ya kwanza wiki iliyopita kwa mabao 3-0 na hivcyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2, huku CS Sfaxien ikisonga mbele kwa kushinda nyumbani na ugenini kwa jumla ya mabao 3-0.
Timu hiyo ya Tunisia jana ilishinda nyumbani mabao 2-0, na katika mechi ya wiki iliyopita walishinda ugenini kwa bao 1-0.
Mechi nyingine zinatarajiwa kuchezwa leo Jumapili kuhitimisha idadi ya timu 8 zitakazochuana kwenye makundi kuwania mamilioni ya fedha za CAF.

Yanga yafa Mkwakwani, Azam yanusa ubingwa

Yanga
Azam
KLABU Ya Azam imejiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza baada ya jioni hii kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba, huku Yanga ikifa Mkwakwani.
Yanga ilikumbana na kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Mgambo JKT na kutoa nafasi kubwa kwa Azam kunyakua taji hilo kama itashinda mechi mbili kati ya tatu ilizosalia katika ligi kabla ya msimu kuisha.
Mabao ya Mcha Khamis 'Vialli' na John Bocco 'Adebayor' kwa kila kipindi yalitosha kuiwezesha Azam kuendeleza rekodi ya kutopoteza mechi kwa msimu huu na kufikisha pointi 53.
Bao la Simba lililokuwa la kusawazisha lilifungwa kwa kichwa na beki wake wa kati, Joseph Owino dakika chache kabla ya mapumziko.
Nako jijini Tanga bao la mapema la mshambuliaji mkali, Fully Maganga na jingine la mkwaju wa penati wa Malimi Basungu lililotosha kuizamisha Yanga kwenye uwanja wa Mkwakwani, bila kutarajiwa.
Yanga waliokuwa na matumaini makubwa kuibuka na ushindi dhidi ya 'vibonde' hao, walishindwa kuamini walipojikuta wakitafuta bao la kusawazisha licha ya Mgambo kucheza pungufu uwanjani.
Bao la Yanga la kufutia machozi lililokuwa la kusawazisha lilifungwa kwa mkwaju wa penati na Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Everton yaipumua Arsenal, yaifumua Fulham 3-1

Everton's Steven Naismith celebrates the opening goal at Fulham this afternoonTIMU ya Everton, imeendeleza wimbi lake la ushindi baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Fulham na kuitishia Arsenal waliopo juu yao kwa tofauti na pointi nne.
Everton imefikisha jumla ya pointi 60 ikiwa na mchezo mmoja mkononi zaidi ya Arsenal ambayo usiku wa jana ililazimishwa sare ya 1-1 na Manchester City.
Wageni walianza kupata neema dakika sita baada ya kuanza kwa kipindi cha pili baada ya David Stockdale wa Fulham kujifunga kabla ya Ashkan Dejagah kurejesha bao hilo dakika ya 71.
Hata hivyo Everton ikiwa na kiu ya kuwa miongoni mwa timu NNe Bora msimu huu ilicharuka na kuongeza mabao mawili katika dakika ya 79 na 87 kupitia kwa Kevin Mirallas na Steve Naismith na kuzidi kuizika Fulham katika kaburi la kushuka daraja msimu huu.
Fulham imeendelea kusalia mkiani ikiwa na pointi 24 kutokana na kucheza mechi 32 wakati ligi ikiwa imesaliwa na raundi sita kabla ya kukamilisha msimu wake.
Muda mchache baadaye Liverpool watakuwa wakijaribu kutafuta nafasi ya kukwea kileleni itakapoumana na Tottenham Hotspur kwenye uwanja wa Anfield katia mfululizo wa ligi hiyo.

AC Milan yapiga mtu 3-0, Balotelli kama kawa!