STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 25, 2013

SIMULIZI MBALI MBALI ZA KUTISHA KUTOKA MAUJI YA WESTGATE NAIROBI


MJAMZITO wa miezi nane na nusu ni miongoni mwa mateka waliouawa katika uvamizi wa kituo cha biashara cha Westgate jijini Nairobi Jumamosi, imefahamika.

Elif Yavuz ambaye ni msomi wa Chuo Kikuu cha Havard, Marekani aliuawa pamoja na mumewe Ross Langdon (33) ambaye ni msanifu majengo mwenye uraia pacha wa Uingereza na Australia.

Taarifa zilizopatikana jana kutoka eneo la tukio zilisema Langdon ameshiriki miradi mbalimbali barani Afrika, ikiwamo inayohusika na ujenzi upya wa hospitali ya Ukimwi nchini Kenya bila malipo yoyote.

Elif ambaye alikuwa akitarajiwa kujifungua wiki mbili zijazo, aliuawa sambamba na mumewe huyo ambaye alipata kuwa mshindi wa tuzo ya ujenzi.

Langdon alipata mafunzo ya ujenzi katika Chuo Kikuu cha Tasmania kisha Chuo Kikuu cha Sydney, na kufanya kazi katika kampuni kadhaa kabla ya kuanzisha Kampuni yake ya Regional Associates Ltd, Mei 2008.

Akizaliwa na kukulia Kusini Mashariki mwa Tasmania, miongoni mwa miradi aliyoshiriki iko Uganda, Rwanda na Tanzania.

Alikuwa mtaalamu wa masuala ya malaria akifanya kazi Kenya katika Wakfu wa Bill, Hillary and Chelsea, ulioanzishwa na Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, Yafuz pia alipata kufanya kazi na Wakfu wa Bill and Melinda Gates unaoendeshwa na bilionea muasisi wa Microsoft, Bill Gates.

Akizaliwa Uholanzi, Yavuz ameishi Cambridge, Massachusetts, wakati akisoma Chuo Kikuu maarufu duniani cha Havard. Esther Waters-Crane, mtaalamu wa Uingereza ambaye anamfahamu vizuri Elif, alielezea masikitiko yake kwa kumpoteza mama huyo mtarajiwa na jinsi Kenya ilivyoshughulikia shambulizi hilo lisilo na sababu.

Alisema: “Namsikitikia sana Elif. Tulikuwa tukiwasiliana mara kwa mara juu ya kujifungua kwake akiwa Nairobi na nahisi kuugulia, hasira na mshituko kwa janga hili, janga la kupoteza wapendwa wetu. “Niko nyumbani na milipuko ya Westgate inarindima, inatoa sauti kama iko katika barabara yangu hapa nje. Tumesambaratishwa na hili – ni muda wa huzuni kubwa Nairobi na kwa nchi pendwa Kenya.”

Mama wa Langdon, Linden alisema hasara iliyosababishwa na kifo cha mwanawe huyo haipimiki. Familia yake imeomba faragha wakati huu ikiomboleza kifo chake, cha mwenza wake na mtoto wa tumboni - lakini mama yake aliamua kutoa maneno machache kupitia mitandao ya kijamii kuuambia ulimwengu kuhusu huzuni ambayo ndugu zake wanayo.

“Tumepoteza mwanangu mzuri Ross, mwenza wake mpendwa, Elif na mtoto wao mpendwa wiki mbili tu kabla ya kuzaliwa,” Linden aliandika katika ukurasa wake wa Facebook. “Hasara hii haipimiki, inaumiza.”

Machinjio

Katika hatua ya kusikitisha mmoja wa walinzi wa usalama dukani hapo alisema siku hiyo aliona ghafla duka linageuka machinjio katika kipindi cha nusu saa, kutokana na magaidi hao kuua watu ovyoovyo.

Wanamgambo hao walichoma moto nyuso za mateka wao na kuwanyofoa mikono kwa lengo la kupoteza utambulisho na miili yao kurundikwa katika lango kuu ili kupunguza kasi ya mchakato wa uokoaji.

Taarifa zilizotolewa juzi kupitia mitandao zilisema mwanamke majeruhi aliyekwama ndani ya duka hilo chini ya watekaji alidhalilishwa kijinsia mbele ya mtutu wa bunduki na mbele ya mateka vijana kwa kubakwa na magaidi hao. Inadaiwa mwanamnke huyo alipigwa risasi begani huku mwanawe akiuawa katika uvamizi huo.

Inasemekana mama huyo aliwasiliana na mumewe mara nyingi nje ya kituo hicho cha biashara – lakini usiku wa juzi mumewe hakupata tena mawasiliano ya mkewe.

Shindano

Shuhuda mwingine, Kamille Kaur, alikuwa na watoto wengi wakishiriki shindano la upishi katika duka hilo lililokuwa likifanyika katika ghorofa ya pili wakati shambulizi linatokea.

Mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 12 na bintiye wa miaka minane, walijeruhiwa kwa risasi. Alisema watu wazima “waligeuka kama wanyama, wakikanyaga watoto katika juhudi za kujiokoa.”

Twitter ya kikundi cha al Shabaab, ambacho kimedai kuhusika na shambulizi hilo, ilisema washiriki wanatoka mataifa saba, yakiwamo ya Uingereza, Marekani na Canada.

Kikundi hicho hivi karibuni kiligawanyika katika vikundi viwili kutokana na mapigano makali baina yao. Wasiohusika na uvamizi wa Nairobi wanadaiwa kueneza taarifa potofu zinazozua maswali juu ya ukweli wa taarifa za awali kwamba wakazi wa London, Ahmed Nasir Shirdoon (24) na Liban Adam (23) ni miongoni mwa magaidi hao.

Mkuu wa Majeshi ya Kenya, Jenerali Julius Karangi, alisema wapiganaji kutoka nchi mbalimbali wamehusika katika mashambulizi hayo, lakini hakutaka kuzitaja nchi hizo.

“Tuna fununu za ni akina nani, uraia wao na hata idadi yao pia,” alisema na kuongeza kwamba wanamgambo hao ni mkusanyiko wa raia wa mataifa mbalimbali duniani…tuna fununu pia kwamba hili si tukio la ndani,” alisema na kuongeza: “ Hapa tunapambana na ugaidi wa kimataifa na tuna uhakika na tunachokisema.”

Wakenya juzi usiku walikuwa wanahofia kutokea mashambulizi mengine ya kigaidi baada ya kutokea madai kuwa wengi wa wanamgambo hao wanatoka katika kikundi hicho cha al Shabaab ambao waliingia nchini baada ya kuhonga wahusika.

Msemaji wa al Shabaab alisema Waingereza wote walioko Kenya ni ‘walengwa’ wao kwa sababu Uingereza inasaidia nchi hiyo kuingilia kijeshi Somalia.

Juzi Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron alirejea nyumbani mapema akitoka Balmoral, ambako alikuwa na Malkia, ili kuongoza kikao cha dharura cha ulinzi na Baraza la Mawaziri akiwamo Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg, Chansela George Osborne na Waziri wa Ulinzi, Philip Hammond.

Waislamu wauawa

Baba Mwingereza wa binti wa umri wa miaka minane juzi alisimulia kwa huzuni kubwa jinsi alivyopata taarifa za bintiye huyo Mwislamu na mkewe kuuawa na magaidi hao.

Louis Bawa (43), alisema bintiye huyo, Jennah na mkewe mzaliwa wa Kenya Zahira (41), waliuawa Jumamosi na ‘wanyama’ ambao walikuwa wakitumia “dini kama kisingizio cha kuua watu.”

Waziri Mkuu Cameron alisema inaonekana miongoni mwa waliouawa takribani sita ni raia wa Uingereza. Bawa, ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni moja ya Masoko aliiambia The Daily Telegraph, kwamba: “Watu waliofanya haya, ni wanyama…mwisho wa siku wanatumia dini kama kisingizio cha kuua watu.

Wanasema wanalenga watu fulani, lakini wanalenga mtu yeyote. Zahira na Jennah walikuwa Waislamu! “Lakini wanyama hawa waliwaua kama walivyofanya kwa wengine.

Awali nilishawishika kwamba wangekuwa salama. Nilikuwa na matumaini…. Hivi sasa naomba haki itendeke kwa wanyama hawa waliotenda haya.” Bibi wa Jennah, Shakuntna Bawa (63) juzi alisema familia yake imesikitishwa na kukatishwa tamaa na janga la Nairobi, akiwambia waandishi wa habari :”Tulishajua kuwa wamepotea. “Lakini tukasikia baadaye kwamba kwa bahati mbaya wameuawa.

Nimeshituka sana – familia yote iko kwenye mshituko. Kwa sasa siwezi kusema lolote. Inasikitisha – lakini tutafanyaje?” Aliongeza: “Dada yangu alimwona Louis akizungumza kwenye televisheni na kunipigia simu.

Wakati huo tulikuwa bado tukiamini kuwapo fursa nyingine ya Jennah na Zahira kuwa salama, kwa sababu watu wengi walikuwa wamepotea. “Lakini polisi wamethibitisha kwa Louis kwamba mkewe na bintiye wameuawa.

Alijaribu kwenda mochari kutambua miili yao, lakini kulikuwa na walinzi pale. Hata hivyo, baada ya saa kadhaa aliruhusiwa kuingia na kuthibitisha wamekufa. Sijamwona Jennah kwa miaka mitano tangu familia hiyo ilipohamia Nairobi… alikuwa mrembo.”

Wanne wa familia moja

Wakati huo huo, mfanyabiashara wa Uingereza alitangaza kuuawa kwa watu wanne wa familia yake katika shambulizi hilo. Samir Bharma, wa Spinney Hills, Leicester, alikuwa juzi akikamilisha maandalizi ya safari ya kwenda Nairobi.

Ndugu zake hao walikuwa Nairobi kurekodi kipindi cha televisheni kinachojulikana kama Masterchef Junior. Alisema: “Walikuwa vijana wakishiriki shindano la mapishi ambalo lilikuwa linafanyika katika kituo hicho. Bahati mbaya wote wameaga dunia. “Shangazi naye yuko mahututi hospitalini. Nimezungumza na baba ambaye yuko huko, lakini mawasiliano ni magumu. Ni wakati mgumu sana na napanga safari sasa.”

Mkazi mwingine wa Leicester alielezea jinsi wazazi, kaka na dada yake walivyokuwa dukani hapo wakati magaidi wakishambulia. Mtu huyo mwenye umri wa miaka 20 ambaye hakutaka kutajwa jina baada ya mama yake kumwambia kwamba magaidi wameingilia mawasiliano ya Facebook yake na wakimwonya kuwa “tunakufuatilia”.

Alisema mama yake alimpigia simu: “Alikuwa ghorofani juu wakati mambo yote yakifanyika ghorofa ya chini ndipo alipoona magaidi hao wakizungukazunguka kila mahali na kufyatulia watu risasi. Aliona rafiki yake akipigwa risasi kichwani. “Dada yangu alichanganyikiwa. Kaka yangu alimvuta nje hadi eneo la maegesho ya magari…wakati huo eneo hilo lilikuwa salama na watu waliweza kuondoka.

Kaka yangu aliona mwili wa rafiki yake nje. Ulikuwa umepigwa risasi.” Mtu huyo alisema wazazi wake walikwenda hospitalini hapo kusaidia wafanyakazi kuhudunia majeruhi.

Mtoto jasiri

Mtoto wa miaka minne Mwingereza Elliot Prior kutoka Windsor, Berkshire, alionesha ujasiri wa aina yake kwa kumkabili gaidi ambaye aliishia kumwomba radhi.

Elliot alimwambia gaidi huyo kwamba ‘ni mtu mbaya sana’ wakati akimzuia kumshambulia mama yake, Amber, ambaye tayari alishajeruhiwa mguuni na dada yake Amelie.

Kama muujiza, gaidi huyo alijisikia huruma kwa familia hiyo na kuwapa watoto hao biskuti kabla ya kuwambia: “Tafadhali nisamehe, sisi si majinamizi.”

Askari shujaa

Askari wa Kikosi Maalumu cha Anga (SAS) cha Uingereza ambaye hakuwa zamu siku ya tukio la utekaji nyara wa kituo cha biashara cha Westgate, Nairobi Jumamosi iliyopita aliibuka shujaa kwa kuokoa maisha ya watu 100 siku ya tukio.

Mwanajeshi huyo siku hiyo alikuwa akipata kahawa katika moja ya migahawa ya Westgate wakati magaidi walipovamia. Shujaa huyo anadaiwa kurudi dukani humo mara 12, kuokoa watu licha ya mashambulizi ya bunduki yaliyokuwa yakiendelea.

Shuhuda mmoja alisema: “Alichokifanya ni cha kishujaa. Alikuwa akinywa kahawa na marafiki zake wakati tukio hilo linatokea. Alirudi ndani mara 12 na kuokoa watu 100. Fikiria kurudi ndani huku ukijua kilichokuwa kikiendelea humo.”

Vyanzo vya habari vilisema askari huyo wa SAS hawezi kutajwa kutokana na sababu za kiusalama. Vikosi maalumu vya Uingereza vimekuwa kwa kawaida vikitoa mafunzo na kuendesha shughuli zao nje ya Kenya, na vimekuwa vikishirikishwa katika kufuatilia raia wa Uingereza walio katika hatari ya kushambuliwa na Waislamu hao wenye misimamo mikali Somalia na Yemen.

Baadhi ya waliokuwa katika vikosi hivyo zamani, wamekuwa wakitumika katika serikali za Uingereza na Kenya kwenye kampuni mbalimbali za usalama na ulinzi katika Afrika Mashariki.

Mashuhuda walieleza jinsi magaidi hao walioficha sura zao kwa skafu zenye maandishi ya Korani walivyoingia jengoni humo, wakirusha mabomu na kumiminia risasi wateja kwa bunduki aina ya AK-47.

Juzi picha katika mitandao ziliwaonesha wakiingia kwenye duka hilo huku wakiwanyooshea silaha wateja waliokuwa wamejawa na hofu.

Wauaji hao ambao walivalia kimagharibi, walisikika wakiamuru Waislamu kuondoka, kabla ya kuwauliza maswali kibabe, kuona kama mateka hao wanaweza kukariri vifungu vya Korani na kutaja jina la Mama wa Mtume Muhammad.

Maarufu walioshambuliwa Uingereza/Australia

Ross Langdon alikuwa msanifu majengo aliyefanya kazi Uganda, Rwanda na Tanzania, akijenga majengo katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya utalii.

Uholanzi

Mwenza wa Langdon, Elif Yavuz (33), alikuwa akitarajia kupata mtoto wa kwanza mapema mwezi ujao. Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Havard Idara ya Afya mwaka huu, alifanya na kukamilisha tasnifu yale juu ya malaria katika Afrika Mashariki na alikuwa akifanya kazi na Mpango wa Afya Bora wa Clinton.

Peru

Juan Ortiz-Iruri alikuwa mtaalamu mstaafu wa magonjwa ya kitropiki katika UNICEF ambaye ameishi miaka 25 Afrika, kwa mujibu wa UNICEF na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Peru, Alejandro Neyra.

Mwanawe Ricardo Ortiz aliiambia Radio RPP kwamba aliingia dukani humo akifuatana na bintiye wa miaka 13 aliyezaliwa Marekani. “Maelezo kutoka kwa dada yangu ni kwamba baba alianguka sakafuni na hakujitikisa tena,” Ortiz alisema.

Alisema dada yake alijeruhiwa mkono, lakini hali yake si mbaya. Ortiz-Iruri amefanya kazi Kenya, Malawi, Zimbabwe na Liberia.

Ghana

Kofi Awoonor, mshairi wa Ghana, Profesa na Balozi wa zamani nchini Brazil, Cuba na Umoja wa Mataifa, alikufa kutokana na majeraha aliyopata, Ofisi ya Rais ya Ghana ilithibitisha.

Wizara ya Habari ya Ghana ilisema mwanawe wa kiume alijeruhiwa na anatibiwa. Kazi ya Awoonor ilivutia kutokana na vionjo vya utamaduni wa kabila lake la Ewe.

Kenya

Mpwa wa Rais Uhuru Kenyatta, Mbugua na mchumba wake, nao ni miongoni mwa waliouawa.

India

Raia wawili wa India, Parmashu Jain (8) na Sridhar Natarajan (40), waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema.

Canada

Wakanada wawili, akiwamo mwanadiplomasia, waliuawa kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Stephen Harper. Alituma salamu za pole kwa waathirika na kusema ni hasara kutokana na kifo cha Annemarie Desloges, ambaye alipata kutumika katika Ubalozi wa Canada nchini Kenya.

Mumewe, Robert Munk alijeruhiwa, lakini ameruhusiwa kutoka hospitalini, vyombo vya habari vya Canada vimeripoti.

Uswisi

Serikali ya Uswisi ilithibitisha kwamba mmoja wa raia wake alijeruhiwa. Ilisema ubalozi wake jijini Nairobi unawasiliana na familia ya majeruhi huyo na maofisa wa Serikali, lakini haukutaja jina lake.

Uingereza

Takribani raia wanne wa Uingereza waliuawa, kwa mujibu wa Ofisi ya Mambo ya Nje, ambayo ilionya kwamba idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka.

Ufaransa

Wanawake wawili wa Ufaransa waliuawa, Rais Francois Hollande alisema.

Afrika Kusini

Raia wa Afrika Kusini aliuawa, kwa mujibu wa Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa.

China

Mwanamke raia wa China mwenye umri wa miaka 38 mwenye jina la ubini la Zhou ambaye alikuwa akifanya kazi katika tasnia ya milki majengo aliuawa, Shirika la habari la Xinhua liliripoti.

Mwanawe wa kiume alijeruhiwa na anaendelea na matibabu hospitalini, kwa mujibu wa Ubalozi wa China nchini Kenya. Marekani Wamarekani watano walijeruhiwa kwa mujibu wa maofisa wa Serikali ya Marekani.

New Zealand

Raia wa New Zealand, Andrew McLeran (34) ambaye alikuwa akisimamia kiwanda cha kutengeneza mafuta ya avocado – Olivado nchini Kenya, alijeruhiwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya New Zealand ilithibitisha. Amelazwa na anaendelea vizuri.

Tanzania

Raia wa Tanzania Vedastus Nsanzugwanko alijeruhiwa miguu na amelazwa Aga Khan, Nairobi na hali yake inaendelea vizuri kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Batilda Burian.

Korea Kusini

Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini ilisema mwanamke raia wa nchi hiyo ni miongoni mwa waliouawa hata hivyo haikufafanua.

Wasiojulikana uraia

Ruhila Adatia-Sood, ambaye mumewe alikuwa mfanyakazi wa kigeni wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani akiishi Nairobi aliuawa, shirika hilo lilisema katika taarifa yake. Alikuwa mfanyakazi mashuhuri wa redio na televisheni nchini Kenya.

Hali halisi jana

Jana vikosi vya Kenya vilionekana vikitegua mabomu yaliyotegwa na wapiganaji hao wa Kiislamu ndani ya duka hilo ambapo watekaji nyara waliendelea kudai kushikilia mateka, Polisi ya Kenya ilisema jana.

“Tunaondoa milipuko ambayo imetegwa na magaidi,” Jeshi la Polisi lilisema kupitia mtandao wa Twitter. Hata hivyo, hakuna ufafanuzi uliotolewa kuhusu ukubwa wa milipuko hiyo.

Jana asubuhi milio ya bunduki na milipuko mingine iliendelea kusikika, ambapo pia sehemu ya paa la duka hilo iliporomoka wakati wa shambulio hilo, kwa mujibu wa ofisa wa Zimamoto.

Watu 68 ndiyo bado idadi ya watu waliopoteza maisha na 175 kujeruhiwa katika shambulio hilo kwa mujibu wa Serikali, ingawa kuna hofu ya idadi kuongezeka, huku al Shabaab ikitamba kuwapo “idadi kubwa ya miili ambayo bado haijaondolewa ndani ya duka hilo.”

Wanajeshi watatu wa Kenya nao wamepoteza maisha kutokana na majeraha waliyopata katika shambulizi hilo. Al Shabaab ilisema wapiganaji wake bado wanadhibiti kituo hicho na mateka wanaowashikilia bado wako hai.

“Kuna idadi isiyohesabika ya miili iliyotapakaa ndani ya duka hilo, na mujahidina (wapiganaji) wanadhibiti eneo lao (Westgate),” ilisema kupitia Twitter yake. “Mateka ambao wanashikiliwa na mujahidina ndani ya duka wako hai, wamechanganyikiwa sana, lakini wako hai.”

Baadaye ilidai kuwa mateka wote wamevishwa mabomu yanayoweza kulipuliwa kwa rimoti. Hadi jana jioni Serikali ilitangaza kuua magaidi saba, ingawa haikutoa ufafanuzi.

Maafa! Kanisa lalipuliwa na kuua watu 75, zaidi 100 hoi

 
WAUAJI  wawili wa kujitoa mhanga wamelipua mabomu yao nje ya kanisa la kihistoria nchini Pakistan jana na kuua watu 75 kwenye shambulio baya zaidi kuwahi kutokea kwa Wakristo walio wachache wa nchini humo.
Taliban wa Pakistan wamekiri kuhusika na shambulio hilo lililotokea katika mji wa Peshawar, wakisema wataendelea kuwalenga wasio Waislamu hadi hapo Marekani itakapositisha mashambulizi katika mji huo wa kikabila nchini humo. Shambulio la hivi karibuni lilifanyika Jumapili pale makombora yalipopiga majengo mawili katika eneo la North Waziristan, na kuua watu sita wanaodhaniwa kuwa wanamgambo, maofisa wa intelijensia Pakistan walisema.
Shambulio kwenye Kanisa la All Saints, ambalo pia lilijeruhi watu 110, linatekeleza kitisho kilichotolewa na Taliban wa Pakistan wakati huku serikali ikitaka mpango wa amani na wanamgambo hao.
Shambulio hilo limetokea wakati mamia ya waumini wakiwa wanatoka nje ya kanisa hilo lililoko katika wilaya ya Kohati Gate mjini humo baada ya huduma ya kupata chakula cha bure aina ya wali.
"Kulikuwa na milipuko na kulikuwa na mateso kwetu sote," alisema Nazir John, ambaye alikuwa kanisani pamoja na takribani waumini wengine 400.
"Niliporejewa na fahamu zangu, sikuona chochote ila moshi, vumbi, damu na watu waliokuwa wakilia kwa uchungu. Niliona sehemu za miili zilizosambaratika na damu kuzunguka eneo lote."
Manusura walikumbatiana kila mmoja baada ya milipuko huko. 
Ukuta mweupe wa kanisa hilo, ambalo lilifunguliwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa miaka ya 1800, ulitapakaa mashimo yaliyochimbwa na vipande vya vyuma vilivyotoka katika mabomu ma kusababisha uharibifu mkubwa.
Damu ilitapakaa sakafuni na kusambaa kwenye ukutani. Sahani zenye wali zilitawanyika kila pembe za eneo hilo.
Shambulio hilo lilifanywa na watuhumiwa wawili wa kujitoa mhanga ambao walilipua mabomu yao kwa kupokezana. Mamlaka zimekuta sehemu za mwili na zilikuwa zikijaribu kutambua umri wao.
Milipuko hiyo imeua watu 75 na kujeruhi wengine 110. Waliokufa ni pamoja na wanawake na watoto.
Idadi ya majeruhi ni kubwa mno kiasi cha hospitali hiyo kuishiwa majeneza kwa ajili ya waliokufa na vitanda kwa ajili ya majeruhi, alisema Mian Iftikhar Hussain, waziri wa zamani wa habari wa jimbo la Khyber Pakhtunkhwa ambaye alikuwa katika eneo la tukio.
"Hili ni shambulio baya zaidi dhidi ya Wakristo katika nchi yetu," alisema Irfan Jamil, askofu wa mji wa mashariki wa Lahore.
Mmoja wa waliojeruhiwa, John Tariq, ambaye amepoteza baba yake katika shambulio hilo, aliwauliza washambulizi hao, "Tumewakosea nini watu hawa? Kwanini tumekuwa tukiuawa?"
Ahmad Marwat, ambaye alijitambulisha kama msemaji wa tawi la Jundullah la Taliban wa Pakistan, alidai kuhusika na shambulio hilo.
"Wote wasio Waislamu nchini Pakistan ni walengwa wetu na wataendelea kuwa hivyo kwa wakati wote Marekani inaposhindwa kusitisha mashambulizi katika nchini yetu," alisema Marwart kwa njia ya simu kutoka sehemu isiyojulikana.
Askofu wa Peshawar, Sarfarz Hemphray, ametangaza siku tatu za maombolezo kufuatia shambulio hilo na kuishutumu serikali na vyombo vya ulinzi kwa kushindwa kuwalinda Wakristo wa nchini humo.
"Endapo serikali itaonesha nia, inaweza kudhibiti ugaidi huu," alisema Hemphray. "Tumekuwa tukizitaka mamlaka kuimarisha ulinzi, lakini hazitilii maanani."
Waziri Mkuu wa Pakistani ameshutumu shambulio hilo katika taarifa iliyotumwa kwa waandishi wa habari, akisema, "Magaidi hawana dini na wanaolenga watu wasio na hatia ni kinyume cha mafundisho ya Kiislamu na dini zote."
"Matukio kama hayo ya kiwendawazimu ya ugaidi yanaakisi unyama na akili zisizo za kibinadamu za magaidi," alisema.

Wawili wanaswa na maiti yenye dawa za kulevya

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na maiti, iliyokuwa na pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin tumboni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova alitaja waliokamatwa kuwa ni Nasri Omari (36), maarufu kama Rajabu Robot na Mwanaisha Salim( 36), mkazi wa Kigogo Luhanga.

“Kila pipi ina urefu wa sentimita sita...tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa huko Tabata kuna mtu mmoja alifariki ghafla muda mfupi baada ya kutoka bafuni kuoga na tukaamua kulifuatilia tukio hilo” alisema.

Alisema makachero walifika eneo la tukio, nyumbani kwa Omari na kuhoji hatimaye kugundua uwepo wa maiti sebuleni ikiwa imelazwa chali katika godoro sakafuni huku akiwa hana nguo na amefunikwa na shuka.

“Omari ambaye ndiye mmiliki wa chumba kilichokutwa maiti, alisema marehemu anajulikana kwa jila la Rajabu Kandunda (43), maarufu kama Mashaka Mabruki” alisema.

Kamishna Kova alisema uchunguzi wa awali, ulionesha kuwa Kandunda alifika kutoka Mtwara Septemba 21 kwa maelezo kwamba alikuwa mgonjwa na alikwenda kuchukuliwa na watuhumiwa hao wawili.

Alisema uchunguzi huo, ulifanywa na jopo la madaktari wawili na kushuhudiwa na maofisa wa juu wa Polisi na ndugu wa karibu wa marehemu, ambapo katika uchunguzi huo wa mwili wa marehemu, tumboni zilikutwa pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin, zenye thamani ya mamilioni ya fedha.

“Zipo taarifa zinazoonesha kwamba alikuwa ni mhalifu mzoefu wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kwani kabla ya kurudi Tanzania alikuwa akitumikia kifungo nje ya nchi barani Asia” alisema.

Kova alisema uchunguzi zaidi unafanyika ili kujua mtandao mzima wa usafirishaji wa dawa hizo, ambao umemhusisha marehemu. Alisema wote watakaobainika kuhusika, watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha alisema baada ya upekuzi, marehemu huyo alikutwa na vielelezo vingine, ikiwemo fedha za Kenya Sh 700, Dola za Marekani 100 na fedha ya Ushelisheli.

Alisema operesheni ya kukamata dawa za kulevya, inaendelea. Aliomba raia wema kuendelea kutoa taarifa za dawa hizo, kwani zina madhara makubwa kwa wananchi, hasa vijana.

Serikali yawapongeza mashujaa wa ARS kuibeba Tanzania

Mkurugenzi wa Masoko wa Airtel, Levi Nyakundi akiongea wakati wa halfa ya kuwapongeza timu akiongea wakati wa halfa ya kuwapongeza wachezaji wa timu ya Airtel Rising stars mara baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya Airtel Rising Stars nchini Nigeria. halfa hiyo ilifanyika jana katika hoteli ya Hyatt.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah akiongea wakati wa halfa hiyo.
Wachezaji waliozawadia kwa kung'ara katika michuano ya Airtel Rising stars pamoja na Nahodha wao wa timu wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi  Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Leonard Thadeo (kulia) na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Nahodha wa timu ya Wasichana ya Airtel Rising Stars chini ya umri wa miaka 17, Stumai Abdallah akimkabidhi kombe la ubingwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Leonard Thadeo baada yakuwa mabingwa katika mashindano yaliofanyika nchini Nigeria jumapili. Kushoto ni mkurugenzi wa masoko wa Airtel Levi Nyakundi na katikati ni katibu mkuu wa shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF), Angetile Osiah.
***
Mkurugenzi wa maendeleo wa michezo nchini bw Leonard Thadeo ameipongeza timu ya wasichana ya Tanzania baada ya kutwaa ubingwa wa vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars yaliomalizika juzi nchini Nigeria.

Tanzania waliibuka mabingwa baada ya kuwafunga Kenya katika fainali, pia amewapongeza wavulana baada ya kufikia hatua ya nusu fainali. Mabingwa wamezawadiwa kombe pamoja na kitita cha dola za marekani 10,000.

Katika pongezi zake pia amewapongeza wafungaji kwa upande wa wasichna ni Shelda Boniface na  mvulana  ni Athanas Mdamu na pia amempongeza mchezaji bora kutoka timu ya wasichana ambae ni Tatu Iddi .

Katika mashindano haya Tanzania imetoa rekodi tatu , mfungaji bora kwa upande wa wasichana  magoli matano, mfungaji bora wa kiume magoli manne , mchezaji bora kwa upande wa wasichana na pia wachezaji watatu upande wa wavulana wamefunga magoli matatu katika mechi moja (hat-trik) na kuondoka na mpira kila mmoja.

Kabla ya kukabidhiwa kombe na mabingwa hao, Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo nchini, bw Leonard Thadeo amesema kuwa serikali kupitia wizara ya michezo itaendelea kusaidi mpira wa vijana wenye umri mdogo ili kuifikisha mbali Tanzania katika medani ya soka.

Akiongea kwa niaba ya msafara wa timu kocha Rogacian Kaijage amesema kua mashindano yalikua magumu ila wamefanikiwa kuchukua ubingwa , amewapongeza vijana wake , kocha mwenzie wa timu ya wavulana Abel Mtweve na pia ameishukuru Serikali , Airtel , TFF, pamoja na  DRFA

Mkurugenzi wa masoko wa Airtel bw Levi Nyakundi ameahidi kuwa Airtel itaendelea kudhamini mpira hasa wenye umri mdogo na pia kuongeza mikoa ya ushiriki  wa mashindano ya Airtel Rising Stars.

David Haye achanika jicho, ashindwa kumvaa Tyson

BINGWA wa zamani wa uzito wa juu, David Haye amelazimika kusogeza mbele mpambano wake na Tyson Fury uliopangwa kucheza Septemba 28, ambao ulitakiwa kufanyika jijini Manchester kutokana na kupasuka juu ya jicho lake la kushoto.
Haye ambaye alipoteza mkanda wake wa WBA Julai 2011 kwa bingwa Vladimir Klitschko wa Ukrain, alipasuka Ijumaa alipokuwa anafanya mazoezi na Mcroatia, Filip Hrgovic na kulazimika kushonwa nyuzi sita.
Promota wa Haye amesema katia taarifa yake kuwa kutokana na kushonwa nyuzi hizo ambazo zitatolewa baada ya siku saba ndipo watajua lini anaweza kupanda ulingoni kwa ajili ya pambano hilo, hadi sasa hakuna tarehe iliyopangwa.
"Pamoja na maandalizi kuwa yanakwenda vizuri," alisema Haye mwenye miaka 32. "Nilijiandaa vizuri sana na mambo yalikuwa yanakwenda sawa. Lakini kwa sasa, natakiwa kukabiliana na hali iliyotokea."

Mamlaka Mwanza zaahidi nyasi bandia Nyamagana

Rais wa TFF, Leodegar Tenga (wa pili kushoto) akiwa na ujumbe wa Mkoa wa Mwanza ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Evarist Ndikilo ulipomtembelea katika ofisi za TFF jana. Wa tatu kutoka kushoto ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula akifuatiwa na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hida Hassan.
  
Na Boniface Wambura
MAMLAKA za Mkoa wa Mwanza zimesema zitatimiza ahadi yao ya kuchangia dola 118,000 za Marekani (zaidi ya sh. milioni 190) ili kukamilisha mradi wa kuweka nyasi bandia kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza kabla ya Oktoba 15 mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo pamoja na Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula wametoa ahadi hiyo wakati wa kikao kati yao na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga kilichofanyika leo (Septemba 25 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF.

Wakuu hao wa Mwanza katika kikao hicho pia walifuatana na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hida Hassan.

TFF ilipeleka mradi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wa Goal Project IV wa nyasi bandia wa dola 500,000 za Marekani katika Uwanja wa Nyamagana.

Mradi huo ulipelekwa huko baada ya Mkoa wa Mwanza kuahidi kuchangia dola 118,000 ili kukamilisha thamani ya mradi mzima ambayo ni dola 618,000 za Marekani. Wamiliki wa uwanja huo ni Jiji la Mwanza.

Goal Project I ilitumika kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ya TFF (technical centre), Goal Project II nyasi bandia Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume wakati Goal Project III iliweka nyasi bandia katika Uwanja wa Gombani ulioko Pemba, Zanzibar.

Mashujaa wa ARS watua Bongo wakitokea Nigeria

Mabigwa wa michuano ya Airtel Rising Stars Afrika kwa upande wa wasichana Timu ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jana usiku.
Kikosi cha timu ya Airtel Rising Stars cha Tanzania wakiwa kwenye Bus tayari kwenda hotelini mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Julius Kambarage nyerere jana usiku.
Mzazi wa mchezaji wa kike, Donisia Daniel  akimpokea mwanae kwa furaha.
Afisa Uhusiano wa Airtel, Jane Matinde (mwenye rasta) akiwalaki wachezaji  mara baada ya kuwasili kutoka katika michuano ya Airtel Rising Stars nchini Nigeria. Pichani ni baadhi ya watu waliojitokeza usiku huo kuwapokea wachezaji hao.