STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 15, 2011

TAMAGSARAI na mikakati yao dhidi ya uboreshwaji masoko


KUTOKANA na kuona hawana sauti ya pamoja na mahali pa kusemea matatizo na kero zinazowakabili katika shughuli zao, wauzaji wa mazao ya nafaka katika soko maarufu la Tandale waliamua kuunda umoja wao kama njia ya kupigania na kutetea haki zao.
Umoja huo wa wauza nafaka hao unafahamika kwa kifupi kama TAMAGSARAI ambao ni kifupi cha Umoja wa Wauza Nafaka na Wawekezaji wa Soko la Tandale kwa lugha ya Kiingereza na ulianzishwa rasmi mwaka 2000 ingawa usajili wake ulipatikana mwaka 2003.
Malengo makubwa ya umoja huo ulioasisiwa na watu 45 chini ya Uenyekiti wa Abeid Hamad Lunda na katibu Abdul Kambaya, mbali na kuwa sauti ya pamoja katika utatuzi wa kero na matatizo yao, pia kutaka kubadilisha mazingira na hali ya soko hilo na mengine Tanzania.
Mwenyekiti wa sasa wa umoja huo, Juma Dikwe, alisema masoko mengi nchini likiwemo lao la Tandale yana mazingira duni, machafu na hayavutii, kiasi kwamba yamekuwa yakikimbiwa na baadhi ya watu wanaoenda kwenye masoko ya kisasa maarufu kama 'Super Market'.
Dikwe, alisema kitu cha kinachowauma ni kwamba pamoja na masoko kuwa katika mazingira duni na machafu, kosi na ushuru utozwa kila siku na hazijulikani wapi zinapoenda wakati zilihitajiwa kuboresha masoko husika.
"Tunalipishwa kodi na ushuru, tegemeo letu fedha hizo zingerudi tena kwetu kwa kuboresha maeneo yetu ya kazi, lakini cha ajabu masoko yanakuwa machafu na kuhatarisha maisha yetu," alisema Dikwe.
Mwenyekiti huyo, alisema hata hivyo wanashukuru miaka karibu 10 tangu umoja wao uanzishwe wameweza kuielewesha serikali na kusaidia kuboresha soko lao na wanapigana zaidi kuona masoko mengine nayo yanakuwa katika na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
Alisema karibu masoko yote nchini hufanana kimazingira na hivyo ni vema yakafanyiwa marekebisho kuendana na wakati, ili kusaidia biashara kufanyika vema na kusaidia kuinua kipato cha wafanyabiashara, wakulima na taifa kwa ujumla.
Tangu umoja huo ulipoanzishwa hadi sasa una wanachama 105 ikiwa ni ongezeko la wanachama zaidi ya 60 kwa kipindi cha miaka saba iliyopita, huku ukiwa umesaidia kuandaa semina na mafunzo mara tatu kwa lengo la kuwaelimisha wanachama wao.
Semina ya kwanza ilifanyika mwaka 2007 iliyohusumu Elimu ya Utawala Bora iliyowahusisha viongozi wa serikali za mitaa na wanachama wao kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa shughuli za serikali kwa ufanisi ikiwemo sekta ya masoko.
Kisha mwaka 2009 waliandaa mafunzo mengine yaliyohusu ufuatiliaji wa fedha za umma zilizotengwa kwa ajili ya sekta ya Masoko na mwaka huu waliandaa nyingine iliyohusu Usimamiaji wa Miradi na Rasilimali za Masoko ikiwa ni mradi wa miaka mitatu mfululizo.
Dikwe, alisema mradi huo, semina na mafunzo ya awali yaliandaliwa na umoja wao kwa msaada na ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, The Foundations for Civil Society na imekuwa ikiwahusisha wanachama wao na wachuuzi wengine wa masoko ya jijini Dar es Salaam.
"Mradi huu Usimamiaji wa Rasilimali za Masoko, ni wa miaka mitatu na tunashirikisha wachuuzi wa masoko karibu yote ya wilaya tatu za mkoa wa Dar es Salaam kwa vile matatizo ya masoko yanafanana kwa kiasi kubwa," alisema.
Mbali na kuendesha miradi na semina hizo, TAMAGSARAI pia huwasaidia wanachama wao wanapopata matatizo kama ya kufiwa na mengineyo kupitia fedha zinazopatikana toka kwa wafadhili wao na zile za michango ya ada inayotozwa kwa kila mmoja wao.
Pia husimama kama wadhamini kwa wanachama wao katika hupatikanaji wa mikopo toka kwa asasi za kifedha, ili kurahisisha kuboresha shughuli zao na kuihimiza serikali kuboresha masoko kwa kujenga mabanda ambayo yanakithi haja ya matumizi ya binadamu.
"Mabanda mengi yaliyopo kwenye masoko yetu ni mafupi na hayana ubora na imekuwa chanzo cha vifo vya wanachama na wachuuzi wengine kutokana na magonjwa ya kuambukiza kama Kifua Kikuu, na Kipindupindu na Homa ya Matumbo nyakati za mvua," alisema.
Alisema kwa takwimu za haraka kwa kipindi cha miaka saba, wanachama na wachuuzi wenzao 15 kati ya 50 walioathirika kwa ugonjwa wa Kifua Kikuu walifariki, huku wengine wakinusurika vifo wakati wa msimu wa mvua kutokana na ugonjwa wa Kipindupindu.
"Kwa kweli soko la Tandale na mengineyo nchini ni machafu na yanatisha nyakati za mvua na ndio maana TAMAGSARAI tumekuwa tukipigania kuboreshwa kwake, ili kuwaokoa watumiaji wake yaani wauzaji na wateja ambao wengi wanayakambia na kutukosesha mapato," alisema.
Moja ya mikakati yao kwa sasa ni kutaka kuunganisha nguvu zaidi katika umoja wao na kupanua huduma zao kutoka soko la Tandale tu na kuwa la nchi nzima likiunganisha wachuuzi na wauzaji wote wa nafaka, kwa lengo la kuwa na sauti moja yenye nguvu.
Pia wanajaribu kusaka mbinu na kuwaelimisha wanachama wao na wachuuzi wengine kwa ujumla juu ya upakiaji na uuzaji wa bidhaa zao katika hali ya kisasa ili kuvutia wateja hata wale ambao wanayachukulia masoko mengi kama ya watu wanyonge na wasio na hadhi.
"Tuimeshaanza kuwapa mafunzo wanachama wetu ili kupakia bidhaa zao kisasa, badala ya kuendelea kutoa huduma kizamani ambayo inachangia watu kukimbilia Super Market wakiona ni usasa zaidi, ingawa bidhaa ni zile zile na pengine zetu ni bora zaidi, " alisema.
Msisitizo wa umoja huo wenye safu kamili ya uongozi uliochaguliwa baada ya kuongozwa kwa muda na viongozi waasisi ni kuitaka serikali kutumia kodi na ushuru wanaotoza kwenye masoko kuboresha mazingira na masoko hayo kusaidia ajira na vipato vya watumiaji wake.
"Pia tunataka fedha zinazotengwa na serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za masoko zitumike kwa malengo yaliyowekwa badala ya kufanyiwa ubadhilifu na wachache wenmye jukumu la kusimamia masoko," alisema Dikwe.
Aliongeza, pia ni vema masoko yakamilikishwa kwa vyama au wafanyabiashara wenyewe badala ya kuachiwa mawakala ambao wapo kifedha zaidi bila kuangalia uboreshaji wa mazingira ya masoko hayo kulingana na kodi na ushuru wanaotoza kila siku sokoni hapo.
Safu nzima ya umoja huo ambao kwa sasa unasaka soko la bidhaa zao nje ya nchi ni Mwenyekiti wake ni Juma Dikwe, Makamu wake, Juma Janga, Abdul Kambaya ndiye ni Katibu, wakati Sadiki Kubiga niu Mhazini.

Mwisho