STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 11, 2013

Pan Africans kwafukuta moto, IDFA yaamua kuingilia kati

Jengo la makao makuu ya klabu ya Pan African
WANACHAMA wa klabu ya Pan African wameushtaki uongozi wao kwa Chama cha Soka Wilaya ya Ilala (IDFA) kwa madai ya kukiuka katiba wakishindwa kuitisha mikutano tangu walipoingia madarakani mwaka 2009.
Kwa mujibu wa barua yao kwenda ya Machi 30, 2012 kwenda kwa Katibu Mkuu wa IDFA, wanachama hao wa Pan wanadai tangu uongozi wao ulipoingia madarakani Aprili 18, 2009 hawajaitisha mkutano wowote wala kushirikisha wanachama katika baadhi ya maamuzi waliyoamua kuyafanya.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na mmoja wa wanachama wa klabu hiyo kwa niaba ya wenzake, Abbas Ally (kadi namba 0075), imedai mbali kutoshirikishwa katika maamuzi yanayofanywa na uongozi huo, pia klabu imekuwa haina ofisi.
"Japo jingine linalotutisha ni klabu kutokuwa na ofisi wake tuna jengo letu ambalo uongozi umelipangisha lote kiasi sisi wanachama kukosa mahali pa kupata huduma za klabu au kupata taarifa na kulipia ada za uanachama," taarifa hiyo ilisema.
Iliongeza kwa kuiomba IDFA kama mlezi wa klabu za Ilala kuushinikiza uongozi kuitisha mkutano wa wanachama na wao (IDFA) wakiwepo kama shahidi juu ya uongozi lazima uwasilishe mambo manne kwao siku hiyo.
Moja na mambo hayo ni ripoti ya mapato na matumizi kwa kipindi chote walichokaa madarakani na ukaguzi juu ya mapato hayo, taarifa ya sababu zilizoufanya uongozi huo kupangisha jengo lote kiasi cha kukosa ofisi na  mengine.
MICHARAZO liliutafuta uongozi wa Pan kufafanua madai hayo, ambapo  Makamu Mwenyekiti, Ally Hemed alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo badala yake akataka atafutwe Katibu Mkuu wake Saad Mateo ambaye simu zake hazikupatikana hewani.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa IDFA, Daud Kanuti ilithibitisha juu ya kupokea barua ya wanachama hao wa Pan na kudai kamati yao ya Utendaji ilishakutana na kuamua kuziita pande mbili zinazosigana kukaa meza moja kuzungumza.
Kanuti alisema kikao hicho kitafanyika Jumamosi ili kuzisikiliza pande zote mbili kwa kuipitia katiba ya klabu hiyo kisha kutoa maamuzi yatakayoleta suluhu ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

No comments:

Post a Comment