STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 6, 2014

Cheka na Kitime kabla ya Agosti

MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi nchini, John Kitime aliyejitosa kwenye utunzi wa vitabu, amesema kitabu chake kipya cha 'Cheka na Kitime' kitatoka kabla ya Agosti mwaka huu.
Akizungumza na MICHARAZO, Kitime anayepiga muziki katika bendi ya Kilimanjaro Band 'Wana Njenje', alisema kitabu hicho kilikwama kutoka mapema kutokana na sababu zilizo juu ya uwezo wake.
Alisema awali alikuwa amepata mfadhili ambaye angempiga tafu kukiingiza sokoni, lakini wakati mambo yakielekea pazuri mfadhili huyo alipatwa dharura na hivyo mipango yote ikavurugika na kuamua kutulia na kujipanga upya.
Alisema tayari amekamilisha kila kitu kwa ajili ya kukiingiza sokoni kitabu hicho chenye vichekesho na kwamba kabla ya Agosti kitakuwa mtaani na kufuatiwa na mfululizo wa matoleo mengine ya Vol 1 na 2 ambavyo ameshaviandaa mapema.
"Ningependa kuwaambia mashabiki kuwa kile kitabu cha vunja mbavu cha 'Cheka na Kitime' kipo njiani kutokana awali kukwama kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu," alisema.
Kitime alisema pia anaendelea kuandika vitabu vingine viwili tofauti na vunja mbavu vya 'Kilimanjaro Band' ambavyo ni maalum kwa ajili ya kuzungumzia histoari ya bendi yao ilipotoka ilipo na inapoenda sambamba na wasifu wa wanamuziki wake.
"Kitabu kingine cha tatu ni cha 'Haki Miliki', nimeamua kuandika kwa nia ya kuwazindua wasanii kufahamu haki zao katika miliki ya kazi zao," alisema mkongwe huo.
Kitime anakuwa mwanamuziki wa pili mkongwe kujitosa kwenye fani ya uandishi vitabu, baada ya Tshimanga Kalala Assosa, aliyetunga kitabu cha 'Jifunze Lingala' ambacho kinaendelea kutamba sokoni kwa sasa huku akiandaa kingine cha wasifu wake.

No comments:

Post a Comment