STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, April 7, 2012

MAMIA WAFURIKA MSIBA WA STEVEN KANUMBA





MEYA wa Manispaa ya Kinondoni na Ilala, Yusuf Mwenda na Jerry Slaa ni miongoni
mwa viongozi waliojitokeza kwenye msiba wa nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba aliyefariki juzi usiku nyumbani kwake baada ya kuanguka katika mzozo na mpenzi wake.
Aidha umati mkubwa ulijitokeza kwenye msiba wa msanii huu uliopo nyumbani kwake
Sinza Vatican, jana ulisababisha msongamano mkubwa kiasi cha kuziba barabara ya
Makanya na kuwalazimisha askari polisi kufanya kazi ya ziada kuweka mambo sawa.
MiCHARAZO lililokuwepo msibani hapo, liliwashuhudia mameya hao na viongozi wengine kama Katibu wa Kamati ya Uchumi na Fedha CCM-Taifa, Mwigulu Nchemba na Diwani wa Kata ya Sinza, Renatus Pamba wakiwa na nyuso za huzuni wakitoa pole zao.
Viongozi hao kila mmoja alikuwa akiwapa pole wasanii waliofanya kazi na Kanumba
pamoja na watu wengine kabla ya baadhi yao kuondoka na kuwaacha mamia ya watu
wakiwemo wasanii nyota wa filamu wakiendelea na msiba huo.
Kutokana na wingi wa watu waliojitokeza kwenye msiba huo, iliwalazimisha waratibu wa msiba huo, kuwahamishi waombelezaji hao kwenye ukumbi wa Vatican Hoteli, huku wakiwazuia wengine kuingia ndani na kuleta tafrani za hapa na pale.
Mratibu wa Bongo Movie, Steven Mengele 'Steve Nyerere' alisema waliamua kuhamishia watu hotelini hapo kutokana eneo la nyumba ya marehemu Kanumba kutotosha kwa wingi wa waombolezaji waliojitokeza waliosababisha msongamano mkubwa.
Msongamano huo wa waombelezaji ulisababisha hata magari yanayotumia barabara ya
Makanya kushindwa kupita vema na kuwapa kazi ya ziada askari polisi wa kawaida na
wale wa barabarani kuyaongoza magari hayo.
Wasanii mbalimbali walikielezea kifo cha Kanumba kama pengo litakalochukua muda
mrefu kuziba katika tasnia ya sanaa hasa uigizaji wa filamu ambayo marehemu aliifanya kwa muda mrefu wa maisha yake tangu akiwa shuleni.
Mayasa Mrisho anayefanya kazi nyingi na Kanumba, alisema mpaka sasa haamini kama
Kanumba kafariki kwa namna kifo chake kilivyokuwa cha ghafla.
'Siamini, kama ni kweli Kanumba kafa," alisema huku akilia. Aliongeza Kanumba
amefariki wakati wakitoka kumalizia kazi yao mpya iitwayo 'Mr Price', huku pia
wakijiandaa kuingiza sokoni filamu yao mpya iitwayo 'Ndoa Yangu'.
Wasanii wengine kama Patcho Mwamba, Rajabu Jumanne 'Chilli', Issa Kipemba, Fatuma Makongoro 'Bi Mwenda' walisema itawachukua muda mrefu kumsahau mwenzao ambaye alikuwa mtu wa watu, asiye na makuu licha ya umaarufu mkubwa aliokuwa nao.
Nalo Baraza la Sanaa la Taifa, kupitia Katibu Mkuu wake, Ghonce Materego, walitoa
salamu za rambirambi kutokana na kifo hicho cha Kanumba wakidai kimeshtua na
kuwaachia pengo kubwa katika fani ya sanaa nchini.
"BASATA inaungana na familia za wafiwa na wasanii wote nchini kwa maombolezo ya msiba huu mkubwa na wa kihistoria. Kufiwa na msanii huyu mahiri kwenye tasnia ya filamu ni pengo kubwa kwa familia, Sekta ya sanaa na Taifa kwa ujumla kutokana na
ukweli kuwa, aliweza kuutangaza utamaduni na sanaa yetu nje ya mipaka," sehemu ya
rambirambi hiyo ya Basata inasomeka hivyo.
Steven Charles Kanumba, aliyezaliwa Januari 8, 1984 huko Shinyanga, alifariki usiku wa kuamkia jana kwa kile kinachoelezwa alisukumwa na kuanguka sakafuni na aliyekuwa
mpenzi wake, Elizabeth Michael 'Lulu' ambaye kwa sasa anashikiliwa na jeshi la Polisi.
Msanii huyo, aliyesoma Shule ya Msingi Bugoyi na Shule za Sekondari Mwadui, Dar
Christian Seminary na Jitegemee kabla ya kuanza kutamba kwenye sanaa kupitia kundi la Sanaa alilojiunga nalo mwaka 2002 hadi 2006 alipojiengua na kucheza filamu mbalimbali.
Baadhi ya kazi zake ni 'She is My Sister', 'Dar to Lagos', 'Cross My Sin', 'The Director', 'Hero of the Church', Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Dar to Lagos, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears, Unfortunutes Love, My Valentine, The Shock, Deception na kazi ya mwisho kuitoa sokoni ni 'Kijiji Chatambua Haki'.

mwisho

No comments:

Post a Comment