STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 31, 2013

Serikali kuondoa kodi vifaa vya michezo


Waziri Makalla
SERIKALI imeahidi kulifanyia kazi suala la kuondolewa kodi kwa vifaa vya michezo vinavyoingizwa nchini, hususani kwa matumizi ya shule na taasisi ya michezo.
Kauli hiyo ilitolewa juzi bungeni na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amosi Makalla alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage (CCM).
Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuhakikisha vifaa vya michezo vinafutiwa kodi.
Akijibu swali hilo, Makalla alisema serikali imechukua hoja hiyo kama changamoto na kwamba itawasilishwa kwa wanahusika, ili ione kama vifaa hivyo vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi kama vinaweza kufutiwa kodi, wakati wa kuingizwa kwake.
Awali, katika swali la msingi Mbunge wa Singida Magharibi, Mohamed Missanga (CCM), alitaka kujua serikali imefikia hatua ipi katika kuendeleza mchezo wa riadha nchini, ikiwa ni pamoja na kupelekwa kwa wataalamu kwenye nchi za Ethiopia na Kenya ili kujifunza mchezo huo.
"Nchi za Kenya na Ethiopia zinafanya vizuri katika mchezo wa riadha wakati Tanzania haifanyi vizuri, je, serikali imefikia wapi katika kutekeleza ushauri wangu niliotoa mwaka 2011 wa kupeleka wataalamu katika nchi hizo hili kujifunza mbinu na mikakati ya kukuza mchezo huu nchini?" alihoji Missanga
Akijibu swali hilo, Makalla alisema wizara hiyo imebaini kuwa nchi hizo zina mafanikio katika mchezo huo kwasababu ya kuzingatia mambo mbalimbali muhimu.
Makalla alisema miongoni mwa mambo hayo ni uhamasishaji na msingi wa kushiriki mchezo huo kuanzia katika umri mdogo katika ngazi za shule za msingi ikiwa ni pamoja na serikali sekta binafsi kuwekezaji katika mchezo huo.
Aliongeza kuwa mambo mengine muhimu yafanywayo na nchi hiyo katika kukuza mchezo huo ni uwapo wa vituo na shule maalum za kuendeleza mchezo huo, pamoja na uongozi thabiti wa mashirika ya mchezo huo.
Makalla alisema kwa kuzingatia mambo hayo, serikali imeanza kuyafanyia kazi kwa kadri ya uwezo wake kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Tanzania.

No comments:

Post a Comment