STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 16, 2013

Aden Rage kupinduliwa Simba akiwa ughaibuni?

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage

SIKU za mwenyekiti Ismail Aden Rage kuongoza Simba zipo hatarini kumalizika kesho baada ya wanachama karibu 700 wa klabu hiyo kuitisha mkutano mkuu ambao utajadili, pamoja na jingine, kutokuwa na imani na uongozi uliopo madarakani.
Mkutano huo unakuja siku chache baada ya makamu mwenyekiti Geofrey Nyange 'Kaburu' na mjumbe wa kamati ya utendaji Zakaria Hans Pope kujiuzulu wiki iliyopita.
Rage yupo kwenye matibabu nchini India kwa gharama za Bunge akiwakilisha jimbo la Tabora Mjini (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, mratibu wa mkutano huo, Mohamed Wandi alisema utafanyika Mnazimmoja "kujadili namna ya kuinusuru" klabu hiyo inayosumbuliwa na migogoro.
Alisema wanachama 698 wameitisha mkutano huo kwa sababu ni haki yao kikatiba na kwamba wamezitaarifa mamlaka mbalimbali zikiwamo polisi, Shirikisho la Soka (TFF) na uongozi wa Simba kuhusu kufanyika kwa mkutano huo.
“Tulishamwandikia barua (siku nyingi) mwenyekiti tukimwomba aitishe mkutano mkuu wa dharura lakini hataki," alisema Wandi.
"Tumeamua kuuitisha wenyewe kwa sababu ibara ya 22 ya katiba yetu inatamka wazi kwamba wanachama wasiopungua 500 wana haki ya kuandaa mkutano mkuu kama mwenyekiti hayuko tayari kuuitisha ndani ya siku 30.”
Alisema mkutano huo utakuwa na agenda mbili ambazo ni mwenendo wa timu katika michuano inayoshiriki na kutokuwa na imani na uongozi wa Rage.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana jijini Dar es Salaam jana kuwa uongozi umepata taarifa za kuitishwa kwa mkutano huo lakini umejipanga kuhakikisha kuwa haufanyiki kwa sababu ni batili.
“Katiba yetu iko wazi, mwenyekiti pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuitisha mkutano mkuu na mkutano mkuu wa dharura," alisema na kueleza zaidi:
"Mwenyekiti wetu hajakataa kuitisha mkutano. Tangu aiingie madarakani amekuwa akiitisha mkutano mkuu wa kila mwaka na tayari alishasema ataitisha mkutano mkuuu wa dharura.
“Mkutano wa Jumapili (kesho) ulioitishwa na wanachama hautafanyika kwa sababu ni batili. Uongozi tayari umesharipoti kwenye kituo cha Polisi Msimbazi kuuzuia."


CHANZO:NIPASHE

No comments:

Post a Comment