STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 3, 2013

Vipimo halisi vya kifo cha Ngwair vyatoka



https://fbcdn-sphotos-e-a.akamaihd.net/hphotos-ak-ash3/p480x480/579293_526768957387103_1440212486_n.jpg
Albert Mangwea 'Ngwair' enzi za uhai wake

RIPOTI ya vipimo halisi vya kifo cha msanii wa Bongofleva, Albert Mangweha a.k.a Ngwair, imetolewa baada ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi na madaktari wa hospitali ya St. Hellen Joseph mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Akizungumza na NIPASHE jana saa 9:50 jioni maeneo ya Mbezi Goig jijini Dar es Salaam ambako msiba wa msanii huyo upo, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, ambaye alitembelea familia ya marehemu, alisema kuwa tayari madaktari wameshabaini chanzo cha kifo cha Ngwair na kwamba vipimo vitakabidhiwa kwa familia ya marehemu.

Msuya alisema kuwa ndugu wa marehemu ndiyo wenye mamlaka ya kuviweka wazi ama kutoiambia jamii kilichomo kwenye ripoti hiyo ya madaktari.

"Serikali imeshtushwa na kifo cha msanii huyu kwa sababu ni kijana. Tumepoteza mtu muhimu kwa sababu alikuwa balozi mzuri wa Tanzania anapokuwa nje ya nchi," alisema Msuya.

Alisema kuwa mwili wa marehemu umechelewa kuwasili nchini kwa sababu ya taratibu za vifo na mazishi nchini Afrika Kusini ambazo zinatofautina kwa kiasi kikubwa na taratibu za Tanzania.

"Mwili wa marehemu ungesafirishwa mapema lakini kilichochelewesha ni 'death certificate' (cheti cha kifo). Afrika Kusini mazishi hufanyika kwa siku za Jumamosi na Jumapili tu na sheria zao za vifo ni tofauti kabisa na za kwetu," alisema.

"Kinachoendelea kwa sasa ni 'booking' ya ndege. Kufikia kesho asubuhi zoezi hilo litakuwa limekamilika na mwili utawasili nchini kesho (leo) ama keshokutwa (kesho)," aliongeza balozi huyo.

Msuya alisema kuwa endapo mwili wa marehemu utasafirishwa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini, utafika jijini Dar es Salaam leo saa moja jioni, lakini utafika kesho saa mbili asubuhi kama ukisafirishwa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.

Aidha, balozi huyo aliwapa pole ndugu, jamaa, marafiki na wasanii waliokuwa kwenye msiba wa marehemu kisha akazungumza na kamati ya mazishi inayoongozwa na Adam Juma.

Ngwair, aliyepata umaarufu mkubwa nchini kupitia tungo zake kali zikiwamo za 'Ghetto Langu' na 'Mikasi' alifariki Jumanne iliyopita nchini Afrika Kusini ambako alienda kwa ajili ya maonyesho ya muziki.

Mitandao ya kijamii na magazeti mbalimbali nchini (siyo NIPASHE) vilikurupuka kuchapisha ripoti 'feki' iliyozagaa kwenye internet ikidaiwa kuwa ndiyo chanzo cha kifo cha msanii huyo nyota ilhali hata vipimo vilikuwa havijafanyika.

Hadi kufikia jana hali ya msanii mwenzake Ngwair, M 2 The P ambaye naye amelazwa baada ya kuzidiwa pamoja na rapa huyo, ilikuwa ikiendelea vyema nchini Afrika Kusini.

Chanzo:NIPASHE

No comments:

Post a Comment