STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 14, 2013

Tamasha la filamu la Grand Malt kufanyika Mwanza




 Msanii wa Filam, nchini, Jaqueline Wolper, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Tamasha hilo, wakati wa mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam




Meneja Habari na Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari, wakati wa mkutano huo (kushoto) ni Mkurugenzi wa Sophia Records walio waandaaji na waasisi wa tamasha hilo, Musa Kissoky.

**************************************

Na Mwandishi Wetu

TAMASHA la Wazi la Filamu Tanzania maarufu kama ‘Grand Malt Tanzania Open Film Festival’ mwaka huu linatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Sahara jijini Mwanza.



 Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa tamasha hilo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa kinywaji cha Grand Malt, Consolata Adam alisema, wanaamini litafanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mikakati waliyoiweka.



Consolata alisema, tamasha hilo linatarajiwa kufanyika katika viwanja hivyo kuanzia Julai 1-7, mwaka huu huku kukiwa na filamu mbalimbali zitakazoonyeshwa katika kipindi hicho.


“Tumejipanga kufanya uhamasishaji wa kutosha ili kuwawezesha wakazi wa Mwanza na maeneo ya jirani kuweza kuhudhuria tamasha hili. Tunawakaribisha watu wote wenye mapenzi na filamu zetu za Tanzania kufika na kushuhudia tamasha hili ambalo mwaka huu limeboreshwa zaidi,” alisema Consolata.


Naye Meneja Habari na Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi alisema kwa ushirikiano na kampuni ya Sophia Records, ambao ndio waandaaji na waasisi wa tamasha hilo, wanaamini litafana na kufanikiwa zaidi mwaka huu.



“Tumeona jinsi wananchi wanavyozipenda filamu za Tanzania maarufu kama ‘Bongo Movies’ na jinsi walivyo na kiu ya kuwaona wasanii wa filamu ana kwa ana,” alisema.



Edith alisema waliingia mkataba wa miaka mitatu wa kudhamini tamasha hilo na kwa sasa wanalipeleka mikoa mingine kama walivyofanya kwa kulipeleka Mwanza kutoka Tanga lilikofanyika mwaka jana.



 “Tunawaahidi Watanzania wote kwa ujumla, kuwa tamasha hili litakuwa na mvuto wa aina yake na hatimae kutumika kulitangaza Taifa letu kupitia tasnia hii ya filamu ambayo kwa sasa inakua kwa kasi kubwa,” alisema Edith na kutaka kampuni au taasisi nyingine kujitokeza ili kuwa wadhamini wenza.



Naye Mkurugenzi wa Sophia Records walio waandaaji na waasisi wa tamasha hilo, Musa Kissoky alitoa shukrani kwa Grand Malt kulidhamini hivyo kuliboresha kwa kiasi kikubwa.



“Tunawashukuru sana Grand Malt na wasanii wa Bongo Movie, hususan uongozi wao, kwa ushirikiana mkubwa wanaotupatia katika kuhakikisha tamasha hili linafanikiwa.”

 

 Tamasha hilo litakuwa likianza asubuhi hadi usiku na kutakuwepo na burudaniu mbalimbali zitakazosindikiza na hakutakuwa na kiingilio, huku akisema bendi ya Extra Bongo watakuwepo siku ya uzinduzi.



Wasanii wote maarufu wa filamu wanatarajia kutua Mwanza Juni 29, ambapo siku hiyo watajumuika na wakazi wa Mwanza ndani ya Club Lips na siku inayofuata watashiriki katika shughuli za kijamii katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, ambapo watatoa vyandarua zaidi ya 1000.



Akizungumzia tamasha hilo, mwigizaji Jacqueline Wiolper alisema, wana furaha kubwa na wanaamini watapata mengi zaidi wakati wote wa tamasha hilo.



Tamasha hilo linadhaminiwa kwa mwaka wa tatu sasa na kinywaji kisicho na kilevi cha Grand Malt kinachozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

No comments:

Post a Comment