Mh Amos Makalla kushoto akiwa na Ofisa wa Executive Solutions, Waratibu wa Udhamini wa Simba na Yanga kutoka TBL, Michael Mukunza kulia |
SERIKALI imeziruhusu klabu za Simba SC, Yanga SC za Dar es Salaam na Super Falcons ya Zanzibar kwenda Sudan kushiriki michuano ya Klabu Buingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Amos Makalla amefanya Mkutano na Waandishi wa Habari mjini Dodoma asubuhi ya leo kusema wameruhusu klabu hizo ziende Sudan baada ya kuhakikishiwa na Serikali ya nchi hiyo kwamba itatoa ulinzi wa kutosha dhidi ya timu za Tanzania.
Makalla amesema wameandikiwa barua na Serikali ya Sudan ikiwahakikishia kwamba timu za Tanzania zitapewa ulinzi mkubwa zisiathirike na machafuko yanayoedelea Sudan.
Kufuatia tamko la Serikali kuziruhusu klabu hizo sasa ziende Sudan, sasa ni juu yao ya klabu hizo kuamua kwenda au kutokwenda.
Lakini Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Mkenya Nicholas Musonye amekwshatishia atazichukulia hatua kali klabu hizo zisipokwenda.
Juzi Serikali kupitia Makalla ilitoa tamko la kuzuia klabu za Tanzania kutokwenda Sudan kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo.
Kufuatia tamko hilo, jana Yanga, ambao ni mabingwa watetezi kwa miaka miwili mfululizo, walitangaza kuvunja kambi yao hadi wiki mbili baadaye, wakati Kombe la Kagame linaanza kutimua vumbi Juni 18, mwaka huu.
Yanga wamepangwa Kundi C katika michuano hiyo pamoja na Ports ya Djibouti, Express ya Uganda na Vital 'O' ya Burundi, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC wamepangwa Kundi A pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman ya Somalia na APR ya Rwanda.
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kufikia tamati Julai 2, mwaka huu mjini Khartoum, Sudan, mabingwa wa Kenya, Tusker wamepangwa Kundi B pamoja na wenyeji wengine, Al-Hilal, Falcons ya Zanzibar, Al Ahly Shandy ya Sudan na Al-Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Yanga wataanza kampeni zao za kutetea taji hilo Juni 20 kwa kumenyana na Express, wakati Simba SC itashuka dimbani Juni 21 kufungua dimba na El-Mereikh, na mechi zote zitachezwa Elfashar.
No comments:
Post a Comment