STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 18, 2013

EXTRA BONGO KUANZA KUGAWA ZAWADI KWA MASHABIKI LEO

BENDI ya Extra Bongo 'Wana Next Level' chini ya Ally Choki leo inatarajiwa kuanza kugawa zawadi kwa mashabiki wao katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Meeda Club, Sinza Mori.
Extra Bongo imeanza wiki nne za kugawa zawadi kwa mashabiki wao, kama njia ya kurudisha shukrani zao kwa mashabiki hao ambapo washindi wa tatu watakaocheza vema miondoko ya bendi hiyo watazoa vitita vya fedha zipatazo 300,000.
Mgawanyo wa fedha hizo ni kwamba mshindi wa kwanza atazoa Sh 150,000 na wa pili kukamata kitita cha 100,000 na atakayekuwa wa tatu atambulia 50,000.
Choki alisema baada ya makamuzi hayo ya Meeda leo bendi yake itaelekea ukumbi wa Garden Breeze, Magomeni Mapipa kwa ajili ya bonanza lao kabla ya Ijumaa kugawa tena zawadi kwa mashabiki wa TMK.
Akizungumzia shoo ya Jumapili hii, Choki alisema, bendi yake imepania kuhakikisha inakonga nyoyo za mashabiki wao wa Magomeni na maeneo ya jirani na kwamba, kila atakayehudhuria atakubaliana na hilo.
“Kazi zetu zinatambulika, watakaokuja watashuhudia shoo kali kutoka kwa wanamuziki na wanenguaji mahiri wa dansi. Waje kwa wingi na kila atakayeingia Garden Breeze, hatojutia uamuzi wake wa kuja kujinafasi nasi wana wa ‘Next Level’ wikiendi hii,” alitamba Choki.
Aidha, mkongwe wa dansi Afrika Mashariki na Kati, Tshimanga Kalala Asosa, naye atafanya vitu adimu akiwa na bendi yake ya Bana Marquiz, watakapotumbuiza kwenye ‘kijiji hicho cha maraha’ cha Garden Breeze leo usiku.
Assosa maarufu kama ‘Mtoto Mzuri’, alisema, amejiandaa kukonga nyoyo za mashabiki kwa vibao vyake vipya na vya zamani, vikiwamo vile vilivyompa umaarufu mkubwa, kiasi cha kuitwa hapa nchini kuanzisha bendi kongwe ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ mwaka 1978.
“Nitawapa mashabiki vitu vipya na vile vyote nilivyopata kuimba katika bendi zangu tangu nikiwa Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), hadi hapa Bongo,” alisisitiza Assosa bila kutaja nyimbo hizo na kuwataka mashabiki wa muziki wa dansi kufurika Garden Breeze.

No comments:

Post a Comment