MASHINDANO ya Taifa ya Ngumi za Ridhaa yaliyokuwa yafanyike mwezi ujao yameota mbawa baada ya Shirikisho la mchezo huo nchini (BFT) kutangaza kuyasogeza mbele hadi Novemba.
Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga aliiambia MICHARAZO kuwa, michuano hiyo iliyokuwa ianze kutimua vumbi lake kati ya Oktoba 8-14 sasa yataanza Novemba 3-8 kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wao.
Mashaga alisema alisema wameamua kuahirisha michuano hiyo ili kupisha mashindano ya ngumi ya kimataifa yanayoandaliwa na Chama cha Ngumi cha wilaya ya Temeke (TABA) ambayo yatafanyika mwezi ujao.
Katibu huyo alisema wameona siyo busara kuendesha michuano ya taifa na mashindano hayo ya kimataifa ambayo yamedhaminiwa na kampuni ya mtandao wa simu za mkononi ya Zantel.
"Tumeamua kuahirisha mashindano ya taifa ya ngumi hadi Novemba kupisha michuano ya kimataifa iliyoandaliwa na wanachama wetu mkoa wa Temeke, kuahirishwa huko kwa mwezi mzima ni fursa nzuri kwa mikoa kujipanga vema kabla ya kuja jijini Dar," alisema.
Mashaga alisema BFT inawatakia kila la heri timu za mikoa ambazo wameshawajulisha juu ya kuahirishwa kwa mashindano ya taifa, pia wakiipongeza Zantel kwa kujitolea kudhamini mashindano hayo ya kimataifa ya Temeke kwa kutoa Sh. Milioni 10.
"BFT inawapongeza wadhamini wao na kuhimiza makampuni mengine kuiga mfano huo kwa lengo la kusaidia kuinua mchezo huo wa ngumi ambao umekuwa ukipambana kurejesha heshima ya Tanzania katika mazingira magumu," alisema Mashaga.
Katibu huyo wa BFT alisisitiza kuwa taratibu nyingine za mashindano ya Taifa yanaendelea kama kawaida na kwamba michuano hiyo itafanyikia kwenye uwanja wa Ndani wa Taifa.
No comments:
Post a Comment