STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, October 12, 2013

Mimi ndiye niyeyaruhusu Rai, Mwananchi-Waziri Makalla

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Amos Makalla 'Mtu wa Watu'
 SIKU moja tu baada ya serikali kuyaonya magazeti ya Mwananchi kwa kukiuka adhabu ya kufungiwa na kuamua kutoa habari kwa njia ya mtandao huku gazeti la Mtanzania, kutumia gazeti la wiki la Rai kuchapishwa kila siku , Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Amosi Makala ameibuka na kusema ndiye aliyeyaruhusu kufanya hivyo.

Katika habari iliyochapishwa jana na gazeti moja la kila siku (siyo NIPASHE), lilinukuu agizo la serikali likionya mmiliki wa Mtanzania kuzingatia ratiba ya kutoa gazeti lao kila siku ya Alhamisi, la Rai na mmiliki wa Mwananchi, kuacha kuchapisha gazeti lao katika mtandao kama amri ya kufungiwa ilivyoainishwa.

Hata hivyo, wakati kauli za Waziri na Naibu wake, Makala, zikitofautiana, gazeti la Mwananchi limemaliza adhabu yake jana ya kufungiwa kwa siku 14.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Naibu waziri Makala, alisema yeye ndiye aliruhusu Gazeti la Mwananchi kuendelea na utoaji wa taarifa/habari kwenye tovuti yake, pia Gazeti la Rai kutoka kila siku.

“Ninalazimika kutoa ufafanuzi kwa njia ya maandishi kutokana na kupigiwa simu nyingi na waandishi wa habari kuhusiana na tamko jipya la Mkurugenzi wa Habari – Maelezo, Assah Mwambene kuhoji uhalali wa Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku, badala ya mara moja kwa wiki (Alhamisi),” alisema.

Makala alisema Oktoba 4, alifanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) na New Habari Corporation (2006) Ltd kwa upande mmoja na msajili wa magazeti kwa upande mwingine.

Alisema katika kikao hicho cha pamoja na viongozi wa Magazeti ya Mwananchi na Mtanzania waliomba waziri apitie upya adhabu iliyotolewa kwa magazeti hayo, ambapo yeye (Makala) aliwaambia kwamba mwenye mamlaka juu ya suala hilo ni waziri mwenye dhamana na masuala ya habari pekee.

Kuhusu ombi la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku badala ya kutoka siku ya Alhamisi, alisema New Habari walieleza kuwa siku zilizopita waliwahi kuomba kwa maandishi kwamba gazeti la Rai litoke kila siku. Maelezo ya Naibu Msajili wa Magazeti katika kikao hicho yalikuwa kwamba, kulikuwa na tatizo la kiufundi katika kurejea maombi hayo na akakiri kuwa hakuna kinachozuia gazeti la Rai kutoka kila siku. Kutokana na maelezo hayo mimi niliridhia gazeti hilo sasa liruhusiwe kutoka kila siku.

Aidha, alisema kuhusu gazeti la Mwananchi kuwa online, Naibu Msajili alisema hakuna sheria yoyote inayoweza kuzuia gazeti hilo kuwa online ila aliwataka lisionekane gazeti zima kama lilivyo, pia wabadili nembo (Master Head) kwa kuweka ya MCL na siyo ya gazeti husika ambalo limefungiwa. “Pia baada ya maelezo hayo niliridhia gazeti hilo liwe mtandaoni kwa kuzingatia angalizo lililotolewa na Naibu Msajili wa Magazeti,” alisema.

Alisema hoja ya tatu ilikuwa ni ile ya Serikali kupitia Idara ya Habari - Maelezo kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya habari, ili kuepuka misuguano isiyo ya lazima, ambapo pendekezo hilo alilipokea na kuliwasilisha kwa Waziri wa Habari kwa hatua zaidi, likiwamo suala la kupitia upya adhabu na ushauri wa kujenga uhusiano na vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa masuala ya gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai kutoka kila siku, alilitolea uamuzi siku hiyo hiyo. “Na uamuzi ni kwamba niliwaruhusu baada ya kuridhika kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa sheria yoyote uliofanywa na waombaji.”

“Nimeamua kuweka sawa jambo hili kutokana na taarifa ya Mkurugenzi wa Maelezo ambayo ninaamini kwamba kutolewa na kusambazwa kwake ni kukosekana kwa mawasiliano kati yake kwa upande mmoja na Mhe. Waziri, Naibu waziri na Naibu Msajili wa Magazeti kwa upande mwingine.

“Hivyo aliyeruhusu Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai ni mimi na ndiyo maana kuanzia tarehe 5/10/2013 Gazeti la Rai lilianza kuchapwa kila siku na kusambazwa, na Gazeti la Mwananchi likaanza kuwa mtandaoni kwa kuzingatia maelekezo ya Naibu Msajili wa Magazeti,” alisema katika taarifa hiyo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment