STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, December 27, 2011

Villa kuchagua mwenyekiti Februari

UCHAGUZI mdogo wa klabu ya soka ya Villa Squad ya jijini Dar es Salaam kuziba nafasi ya Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati ya Utendaji unatarajiwa kufanyika mwezi Februari.
Makamu Mwenyekiti wa Villa, Ramadhan Uledi, aliiambia MICHARAZO kuwa, uchaguzi huo mdogo utafanyika mwanzoni mwa Februari mara baada ya duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara kuchanganya kasi.
Uledi, alisema mwezi ujao kupitia kamati yao ya uchaguzi itatangaza taratibu za uchaguzi huo, ili kufanyika kwake na kuikamilisha safu ya uongozi wa klabu yao.
"Uchaguzi mdogo wa kumpata mwenyekiti na wajumbe wawili wa kamati ya utendaji utafanyika mara baada ya duru la pili la ligi kuu kuanza, nadhani itakuwa mapema Februari mwakani," alisema Uledi.
Aliongeza, kwamba wangeweza kuitisha mapema uchaguzi huo hata sasa, lakini hali mbaya ya ukata waliyonayo na maandalizi ya ligi inayowakabili ndio maana wameona wavute muda hadi baadae huku akisisitiza ni lazima ufanyike katika muda huo.
Mbali na kuwahimiza wanachama wa klabu hiyo kuanza kukaa mkao wa kula kujitokeza kuwania nafasi hizo, ambazo zilishindwa kuwapata washindi wake kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Juni, mwaka huu pia aliwataka wajitokeza kuichangia Villa.
"Wanachama na wadau wa Villa wasaidie kuichangia timu yao kwa ajili ya ushiriki wa duru lijalo, sambamba na kujiweka tayari kuziba nafasi hizo zilizo wazi kwenye uchaguzi huo mdogo," alisema.
Villa ilishindwa kumpata Mwenyekiti wakati wa uchaguzi wake mkuu, kufuatia Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kumuengua aliyekuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo, Abdallah Majura Bulembo kwa kilichoelezwa kukosa sifa stahiki.

Mwisho

No comments:

Post a Comment