STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, December 27, 2011

Kocha Papic 'aivua' nguo Yanga, Niyonzima mh!




KOCHA Kostadian Papic wa Yanga amefichua ubabaishaji mkubwa uliopo katika klabu yake na kuonya kuwa kamwe asitafutwe mchawi pindi watakapoboronga kwani hadi sasa hakuna maandalizi yoyote ya maana waliyoanza kuyafanya kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na pia kwa mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Papic maarufu kama 'Clinton' alisema, hali ngumu ya maisha klabuni hapo ni tatizo kwani wachezaji wake hawahakikishiwi maslahi yao kwa wakati na hadi sasa wanashindwa hata kupata chakula cha uhakika.
Papic alisema kuwa kukosa fedha kumeifanya timu hiyo kushindwa kufanya mazoezi kwa siku saba sasa kwavile hawana hata fedha za kukodisha uwanja wa kufanyia mazoezi.
"Kwa hali hii ya ukata, siwezi kuahidi matokeo mazuri kwa mashabiki wetu... ukweli ni kwamba hivi sasa wachezaji wamepoteza morari ya mazoezi kwa kukosa fedha zao na chakula. Hali hii inasikitisha kwa sababu hivi sasa tunashindwa hata kwenda gym kwa kukosa fedha," alisema Papic.
"Wanayanga wasije wakawalaumu wachezaji au kocha wakati watakapoona timu inafanya vibaya. Pengine si habari nzuri, lakini hiyo ndio hali halisi klabuni," aliongeza Papic.
Papic alisema kuwa kutokana na hali mbaya waliyo nayo kifedha, sasa anakosa nguvu ya kuwabana wachezaji wake kufanya mazoezi kwa kuwa anafahamu hali ngumu wanayokabiliana nayo.
Ppic alianika zaidi udhaifu mwingine klabuni kwao kuwa ni wamawasiliano duni kati ya benchi la ufundi na uongozi wa klabu hiyo.
Kuhusiana na maslahi yake, Papic alisema kuwa mambo mengi waliyokubaliana awali na uongozi kwenye mkataba wao hayajatekelezwa na hivyo hata yeye anakabiliwa na wakati mgumu.
Katika hatua nyingine, Papic alisema kuwa pamoja na timu hiyo kuwa mbioni kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi (visiwani Zanzibar), hadi sasa bado hajapewa taarifa rasmi za kuandaa timu yake kwa ajili ya mashindano hayo.
"Sifahamu chochote kuhusu mashindano hayo... nasikia juu juu tu," alisema Papic.
Papic alisema kuwa wametuma majina ya wachezaji 28 kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kwa ajili ya klabu bingwa Afrika, lakini amemtema kiungo Rashidi Gumbo kwa maelezo mafupi kuwa mchezaji huyo hayupo tayari kwa mashindano hayo.
Papic alisema vilevile kuwa baada ya ratiba iliyotolewa na CAF kuonyesha kuwa watacheza dhidi ya Zamalek, aliomba kupatiwa mikanda ya video ya timu hiyo ili iwasaidie katika maandalizi yao lakini hadi sasa hawajaipata kutokanan na sababu ileile ya uklata inayokwamisha pia harakati nyingine za maandalizi ya kikosi chake.
"Inatakiwa dola za Marekani 10,000 ili kuipata mikanda niliyokuwa nikiitaka... jambo hili hadi sasa limeshindikana," alisema Papic.
Kuhusiana na kiungo wao wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima, ambaye hajaripoti hadi sasa tangu alipomaliza mapumziko waliyopewa baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Chalenji, Papic alisema kuwa atamuadhibu ili fundisho kwa wengine.
"Mara kwa mara amekuwa akitoa visingizio kuwa ana matatizo ya hati yake ya kusafiria.. nitamwadhibu na kumkata mshahara wake ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine," alisema Papic.
Hata hivyo uongozi wa Yanga ulipoulizwa juu ya madai hayo ya Papic, Afisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu, alisema kuwa hawezi kuzungumzia chochote kuhusiana na suala hilo kwa kuwa ni la kiutendaji.
“Hilo suala ni kubwa kwangu. Ni la kiutawala zaidi na hivyo naomba mumtafute katibu au mwenyekiti. Wao ndio wanaoweza kuwajibu,’ alisema Sendeu.
Pia Sendeu alidai kushangazwa na kocha wao kukimbilia kwenye vyombo vya habari wakati angeweza kutoa malalamiko yake kwa uongozi ili kumaliza tatizo.
Naye Katibu wa Yanga, Celestine Mwesigwa, alijibu kwa kifupi kuwa watatoa ufafanuzi juu ya taarifa za kocha wao, ambazo ni kama kuwavua nguo mbele ya wadau wa soka.

No comments:

Post a Comment