STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 15, 2014

Japenese:Muimbaji anayetamba ughaibuni aliyetamani kuwa daktari

MASHABIKI wa muziki wanamfahamu kwa jina la Japanese, ingawa majina yake halisi ni Amina Kassim Ngaluma, mmoja wa waimbaji mahiri wa kike wa muziki wa dansi nchini anayefanya kazi ughaibuni.
Japanese, aliyewahi kuziimbia bendi mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa sasa anafanya shughuli zake za muziki akiwa na bendi ya Jambo Survivors iliyopo Thailand, Mashariki ya Mbali barani Asia.
Mwanadada huyo anakiri licha ya kipaji cha muziki cha kuzaliwa, lakini alijikuta akipenda kuwa mwanamuziki kwa kuvutiwa na muimbaji nyota wa zamani wa Kongo, Mbilia Bell.
Anasema sauti na uimbaji wa Mbilia ulikuwa ukimkuna na kutamani kuwa kama muimbaji huyo, hivyo kuja kuangukia mikononi mwa nyota wa taarab nchini, Bi. Shakila Said, aliyemnoa kwenye uimbaji.
"Siyo siri nilimzimia mno Mbilia Bell, nikatamani kuwa kama yeye na kwa bahati nikaangukia mikononi mwa Bi Shakila aliyeninoa na kuwa hivi nilivyo kupitia kundi la JKT Taarab," anasema.
Anasema hata hivyo alipata wakati mgumu kwa vile mama yake hakupenda awe mwanamuziki badala yake kutaka afanye kazi za ofisi, tofauti na baba yake aliyemuunga mkono hadi leo ukubwani.
Japanese anasema baada ya kuiva kwa Bi Shakila pale JKT Taarab alihamia katika muziki wa dansi akianzia Less Mwenge-Arusha kisha   kukimbilia Kenya alipojijengea jina akizipigia bendi mbalimbali.
"Niliizipigia bendi za Sayari iliyokuwa chini na Badi Bakule 'Mkandarasi', Sky Sound iliyoongozwa na Mwinjuma Muumin, kisha Mangelepa ya Evanee kabla ya kurejea Tanzania," anasema.
Anasema aliporejea nchini alijiunga na African Revolution 'Tamtam' iliyomjengea jina kabla ya kwenda Double M Sound kisha TOT-Plus kabla ya kuhamia Jambo Survivors alionao mpaka sasa.
Japanese anaitaja bendi ya African Revolution kama ilimtambulisha katika ulimwengu wa muziki, ila bendi ya mafanikio na maendeleo kwake ni Jambo Survivors iliyomuinua kiuchumi toka alipokuwapo.

MKALI
Japanese aliyekuwa mahiri kwa mchezo wa Netiboli alioucheza kwa mafanikio kabla ya kutumbukia kwenye muziki, pia ni mahiri kwa utunzi wa nyimbo baadhi ya tungo zake ziliwahi kutikisa muziki wa Tanzania.
Baadhi ya nyimbo alizotunga mwanadada huyo mwenye ndoto za kuja kumiliki bendi binafsi akishirikiana na mumewe ambaye pia ni mwanamuziki Rashid Sumuni ni; 'Mapendo', 'Manyanyaso Kazini', 'Ukewenza', 'Wajane' na Mwana Mnyonge'.
Pia alishawahi kupakua albamu binafsi iitwayo 'Jitulize' aliyoizindua mkoani Morogoro ikiwa na nyimbo sita baadhi ni 'Jitulize', 'Uombalo Hutopata', 'Pete ya Uchumba', 'Mapenzi ya Kweli' na 'Tulia Wangu'.
Japanese anayefurahia tukio la kufunga ndoa na mumewe Rashid Sumuni na kulizwa na kifo cha kaka yake, Mashaka Ngaluma aliyeuawa na majambazi kwa kupigwa risasi akiwa kazini kwake.
"Kwa kweli matukio haya ndiyo yasiyofutika kichwani mwangu, nilipofunga ndoa na mume wangu kipenzi, Rashid Sumuni na siku kaka yangu alipouawa kwa risasi akiwa kazini," anasema.
MAFANIKIO
Japanese asiyefuatilia soka aliota kuja kuwa Daktari ila muziki ukaja kumbeba jumla, ingawa hajutii kwa namna fani hiyo ilivyomsaidia kwa mambo mengi ya kujivunia.
Anasema mbali na kupata rafiki wengi, kutembea nchi mbalimbali duniani na kujifunza tamaduni tofauti, pia muziki umemwezesha yeye na mumewe kumiliki miradi kadhaa ya kiuchumi, nyumba na magari.
Hata hivyo anasema bado hajaridhika hadi atakapoanzisha bendi yao ya Skwensa hapa nchini itakayokuwa ikipiga mahotelini na kurekodi kazi zake katika studio yao binafsi.
Pia angependa kuwasaidia waimbaji wa kike ili kusaidia kuongeza idadi yao katika muziki wa dansi alikodai imekuwa ikizidi kupungua kwa sababu wengi wao hawapendi tabu wala kujifunza muziki.
"Waimbaji wa kike hawapendi dansi kwa ugumu wake hivyo huona bora wajikite kwenye muziki wa kizazi kipya, ila kujifunza muziki wa dansi hasa upigaji ala husaidia kujitangaza kimataifa," anasema.
JUMBE
Japanese alizaliwa Nov 29, mjini Morogoro akiwa ni mtoto wa tatu kati ya tisa wa Baba Kassim Ngaluma na Mama Khadija Abdallah, watatu kati yao wakiwa wameshatangulia mbele ya haki ya kubakia sita tu.
Mkali huyo yupo Jambo Survivors inayopiga muziki wake katika hoteli iitwayo Banthai Beach Resort & SPA akiwa na Hassan Shaw, Eshter Lazaro, Ramadhani Kinguti, Yuda Almasi na mwana BSS Edson Teri.
Mwanadada huyo anasema kwa hapa nchini anawazimia wanamuziki  Hussein Jumbe na Nyota Waziri.
"Hawa ndiyo wanaonikosha na umahiri wao katika muziki," anasema.
Japanese anayewataka wanamuziki wenzake kuwa wabunifu ili kwenda na mabadiliko ya dunia na kuiomba serikali kuutupia macho muziki wa dansi anamshukuru Mungu kwa kumsaidia kufika alipo.
Pia anawashukuru wazazi wake kwa sapoti kubwa anayompa, mumewe Rashid Sumuni pamoja na mwalimu wake Shakila Said bila kuwasahau wote walio bega kwa bega katika fani yake kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment