STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 15, 2014

Azam haishikiki, Yanga yabanwa Prisons hoi

Yanga waliobanwa na Mtibwa mjini Morogoro
Azam iliyouia Coastal kwa mabao 4-0
Kagera Sugar iliyoitibulia Prisons-Mbeya rekodi ya kutofungwa duru la pili
WAKATI 'jinamizi' la kung'olewa Ligi ya Mabingwa Afrika likiendelea kuisumbua Yanga, Azam waliong'oka Kombe la Shirikisho wameendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuwacharaza Wazee wa Oman, Coastal Union kwa mabao 4-0.
Azam walipata ushindi huo kwenye uwanja wa Chamazi, jijini Dar es Salaam wakati Yanga ikilazimishwa suluhu na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro na kuendelea kurejea nafasi ya pili ikiiengua Mbeya City.
Katika mechi ya Yanga na Mtibwa, timu zote zilishambuliana na wenyeji walionekana kuusaka ushindi kutokana na mashambulizi makali yaliyokuwa yakiongozwa na Abdallah Juma ambaye hata hivyo alikuja kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 56.
Azam wanaouwania ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza, iliisasambua Coastal kwa mabao 4-0, mawili yakifungwa na Kipre Tchetche na jingine likiwekwa kimiani na John Bocco na jingine chipukizi wao Kelvin Friday.
Mjini Bukoba, Kagera Sugar iliitibua rekodi ya Prisons-Mbeya ya kutopoteza mchezo wowote kwqenye duru la pili baada ya kuichapa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Kaitaba.
Wenyeji walitanguliwa kufungwa bao katika dakika ya 37 kupitia Peter Michael lililodumu mpaka kipindi cha kwanza kilipomalizika.
Kipindi cha pili wenyeji walicharuka na kufanikiwa kusawazisha bao kwa mkwaju wa penati kupitia Salum Kanoni katika dakika ya 55.
Wakati mashabiki wakiamini kuwa mechi imeisha kwa sare Kagera iliongeza bao la ushindi lililofungwa dakika ya 88 na Benjamini Asukile na kuifanya timu yao kuvuna pointi tatu na kufikisha pointi 32 na kujiimarisha kwenye nafasi ya tano nyuma ya Simba.
Azam kwa ushindi wa leo imeendelea kujimarisha kileleni ikifikisha pointi 43, nne zaidi ya Yanga na Mbeya City ziliyo nafasi ya pili na tatu wakiwa na pointi 39 kila moja kabla ya kutofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

No comments:

Post a Comment