STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 27, 2012

Mashindano ya ngumi yaota mbawa mpaka mwakani

MASHINDANO ya ngumi za ridhaa ya klabu bingwa ya taifa yaliyopangwa kuanza kufanyika jana Novemba 26 hadi Novemba -30 mwaka huu yamesogezwa mbele hadi Januari 29 hadi Februari 3 mwakani.
Katiku Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa nchini (BFT), Makore Mashaga alisema juzi kuwa, wamelazimika kusogeza mbele mashindano hayo hadi mwakani kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na timu shiriki kushindwa kukamilisha taratibu, ikiwa ni pamoja na kutothibitisha ushiriki wake katika tarehe iliyopangwa.
Kwa mujibu wa Mashaga, sababu zingine ni timu shiriki kushindwa kuwasilisha majina na picha za mabondia wake pamoja na kulipa ada ya ushiriki ya sh. 200,000.
"Hadi leo hakuna hata timu moja iliyokamilisha utaratibu huo kwa nia ya kupanga mashindano vizuri ili yawe na hadhi ya taifa kwa kuzingatia sheria za Chama cha Ngumi za Ridhaa cha Dunia (AIBA)," alisema.
"Sababu kama hizi mara nyingi zimesababisha mashindano mengi kuendeshwa kwa kiwango cha chini na lawama nyingi kuelekezwa kwa BFT bila ya kufahamu sababu za msingi," aliongeza.
Mashaga alisema pia kuwa, kozi ya waamuzi iliyopangwa kuanza Novemba 11-30 mwaka huu ilishindwa kufanyika kutokana na washiriki kushindwa kukamilisha taratibu za ushiriki ikiwa ni pamoja na kulipa ada kwa wakati.
Kutokana na BFT kuwa na majukumu mengine, Mashaga alisema kozi hiyo sasa imepangwa kufanyika Januari 15 hadi Februari 4 mwakani na mazoezi ya vitendo yatafanyika wakati wa mashindano ya klabu bingwa.
Mashaga alisema kwa sasa, BFT imeweka nguvu kubwa katika usajili wa makocha, waamuzi, mabondia na madaktari ili waweze kutambulika kwa ajili ya kujiunga na mashirikisho ya ngumi za kulipwa.

No comments:

Post a Comment