STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, December 4, 2014

Mgendi aachia Wema ni Akiba, 'audio' albamu kabla ya X-mass


MUIMBAJI nyota wa muziki wa Injili ambaye pia ni muigizaji wa filamu, Jennifer Mgendi ameachia wimbo mpya uitwao 'Wema ni Akiba' ikiwa ni utambulisho wa albamu yake mpya ijayo.
Tayari wimbo huo wa Mgendi umeanza kutamba kwenye vituo vya redio na katika mitandao ya kijamii baada ya kuuachia mapema wiki hii.
Akizungumza na MICHARAZO Mgendi alisema kuwa albamu yake ijayo itakuwa na nyimbo saba na ameutanguliza uliobeba jina kwa nia ya kuitambulisha kabla ya kuja kuiachia rasmi baadaye.
"Nimeachia wimbo wangu mpya ambao ni utambulisho wa albamu ijayo itakayofahamika kwa jina la 'Wema ni Akiba' itakayokuwa na nyimbo saba," alisema Mgendi.
Muimbaji huyo alizitaja baadahi ya nyimbo za albamu hiyo kuwa ni 'Wema ni Akiba', 'Usiniache Njiani', 'Nimempata Yesu', 'Nani Kama Mungu' na 'Kimbilia Msalabani'.
Albamu hiyo mpya imekuja wakati albamu ya msanii huyo iitwayo 'Hongera Yesu' ikiwa bado haijachuja sokoni ambayo aliiachia mapema mwaka huu.
Kuhusu video ya albamu hiyo, Mgendi, amesema ataanza zoezi la upigwaji picha za video Januari mwakani kabla ya albamu hiyo kuachiwa sokoni Juni, 2015.
Alisema uchukuaji wa video utahusisha nyimbo zote saba zitakazokuwa katika albamu hiyo inayokuja baada ya kutamba na 'Hongera Yesu'.
Jennifer alisema ataanza kurekodi video ya wimbo wa 'Wema ni Akiba' ambao tayari ameshauachia hewani ili kuitambulisha albamu hiyo ambayo ni ya nane kwake.
"Mchakato wa kurekodi video ya albamu yangu ijayo utaanza mapema Januari na nitaitoa rasmi Juni 2015, ila kwa sasa nimeachia 'audio' ili kuwapa ladha mpya ya Jennifer Mgendi," alisema muimbaji huyo ambaye pi ni muigizaji, mtayarishaji na muongozaji filamu.
jennifer alifafanua kuwa 'audio' albamu ya Wema ni Akiba itaachiwa ndani ya mwezi huu kabla ya Sikukuu ya Xmass.
"Audio albamu ya Wema ni Akiba nitaiachia sokoni kabla uya Krismasi ila video yake ndiyo itatoka Juni baada ya kuanza kurekodi mwezi ujao," alisema Jennifer.
Jennifer ambaye kitaaluma ni mwalimu, alianza kutamba kwenye muziki wa Injili mwaka 1995 akitoa albamu saba sambamba na filamu zilizomjengea jina kubwa miongoni mwa wasanii wa kike nchini.

No comments:

Post a Comment