STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, February 9, 2014

DAVID NAFTALI: Kiungo anayetaka viongozi wa soka kuacha mambo ya mwaka '47
David Naftali katia picha tofauti akiwa nchini Kenya
WAKATI wachezaji wenzake wanaocheza nje ya nchi wakirejea nyumbani, kiungo mkabaji David Naftal anasema hana mpango huo kwa sababu havutiwi na mfumo wa soka uliopo nchini.
Nyota huyo wa zamani wa timu za AFC ya Arusha na Simba anayeichezea Bandari ya Mombasa inayoshiriki ligi kuu ya Kenya anasema mfumo wa soka nchini hauthamini na kuwajali wachezaji kama ilivyo Kenya.
Anasema tangu atue nchini humo miaka mitatu iliyopita, hajawahi kusikia viongozi wa klabu wakiwatuhumu wachezaji kuzihujumu timu zao au kuuza mechi kama ilivyozoeleka hapa, hasa kwa Simba na Yanga.
"Huku matokeo ya aina yoyote yanachukuliwa sehemu ya mchezo," anasema. "Tanzania timu ikifungwa tu anatafutwa mchawi na watu wa kwanza huwa wachezaji bila kujali wanavyovuja jasho uwanjani kupigania timu."
Anasema vitendo vya kuwatuhumu wachezaji ni mambo ya kizamani yanayowavunjia heshima na kuwakatisha tamaa.
Naftal anayemudu nafasi nyingi uwanjani, anasema lazima viongozi wa soka wa Tanzania wabadilike na kutambua mchezo huo una matokeo matatu: kushinda, kufungwa na sare. Aidha, anasema, wasiamini timu zao ni bora kiasi cha kutofungika.
Mkali huyo anayefurahia kucheza Kenya na kuaminiwa na klabu yake ya Bandari, anasema kuwapo kwake nchini humo kumemfundisha mambo mengi ikiwamo tofauti iliyopo baina ya soka la Tanzania na nchi hiyo jirani.
Anasema Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji lakini wasimamizi wa soka wamejisahau na kuelekeza  macho mijini. Pia anadai mfumo wa soka wa Kenya na Tanzania kwa ngazi za klabu umetofautiana sana, Kenya klabu zikiendeshwa 'kisomi' kulinganisha na Tanzania licha ya kwamba mchezo huo unaingiza fedha nyingi zaidi nchini.
"Kenya klabu zake zipo kiprofesheno zaidi kulinganisha na Tanzania, ila kifedha Tanzania ipo juu ndiyo maana wachezaji wa kigeni wanamininika huko."
Naftal anasema ndoto zake ni kuzidi kusonga mbele na ndiyo maana hana mpango wa kurudi nyumbani.
Anasema kwa sasa anafanyiwa mipango na wakala wake kwa ajili ya kwenda kucheza nchini Afrika Kusini wakati mkataba wake ukielekea kugota ukingoni Septemba.
Naftal ambaye ni shabiki mkubwa wa klabu ya Manchester United lakini anayemzimia kiungo Yaya Toure wa Manchester City, na ambaye wakati akiwa Simba alianza kucheza kama mshambuliaji, anasema anafurahishwa na changamoto zinazotolewa na klabu za Mbeya City na Azam katika ligi kuu ya Bara kwa sababu "itasaidia kuvunja ligi ya timu mbili za Simba na Yanga."
Anasema kuibuka kwa Mbeya City ni dalili za wazi kwamba mikoani kuna wachezaji wenye vipaji na kama kutakuwa na wawekezaji wanaweza kuleta mapinduzi katika soka la Tanzania.
"Ni lazima TFF na serikali kutupia macho soka la mikoani, kule ndiko kunakoweza kupatikana akina Samuel Et'oo na Didier Drogba wa Tanzania,Mbeya City ni mfano halisi."
" anasema.
NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment