Bondia Yohana Mathayo 'Tembo Mtoto' (kulia) akichuana na Fadhili Awadh 'Mnyama
Chui' katika moja ya mapambano yake enzi za uhai wake.
Na Magendela Hamisi
SEPTEMBA 12 tasnia ya mchezo wa masumbwi ilimpoteza bondia mahili
wa uzito wa kilo kilo 66, Yohana Mathayo 'Tembo Mtoto' (23), akiwa
mazoezini kujindaa na pambano lake la ubingwa wa Taifa dhidi ya Abdallah
Mohammed 'Prince Nassib'.
Pambano hilo lilipangwa kufanyika Oktoba mwaka huu, jijini Dar es
Salaam na kusimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST),
lilionekana kuvuta hisia za mashabiki wengi.
Bondia huyo mahili ambaye jina lake lilianza kujulikana baada ya
kufanya vema katika mapambano yake mengi, tena kwa kushinda kwa KO,
wengi walimtabiri mafanikio makubwa kupitia mchezo huo.
Katika vitongoji vya Jiji la Dar es Salaam, hasa kwenye chimbuko la
mchezo masumbwi yakiwemo maeneo ya Keko, Manzese, Tandale, Mburahati,
Mabibo, Mwananyamala na maeneo mengine hakuna asiyefahamu jina la Tembo
Mtoto.
Kwani kabla ya kuanza kushiriki katika ndondi za kulipwa na
kuwatwanga mabondia wengi alitokea katika ujenzi wa mchezo huo kwenye
ngumi za ridhaa ambako ndiko wanapotokea mabondia bora Tanzania na
ulimwengu kwa ujumla.
Prince Nasseb ambaye ndiye anashikilia mkanda wa taifa wa PST, na
ndiye alitakiwa kuzitwangwa na Tembo Mtoto, anasema kifo cha bondia
huyo ni pigo kubwa kwake kwani aliamini ndio alikuwa mpinzani wake
aliyebaki katika uzito huo wa kilo 66, kutokana na wengi kuwa dhaifu
kwake.
"Sikuweza kuamini baada ya kusikia kifo cha mpinzani wangu, hali
ambayo ambayo hadi leo bado inanipa shida kuamini kama ni kweli Tembo
Mtoto amefariki, lakini kikubwa ni kumuombea Mungu ampumzishe kwa amani
katika makazi ya milele," alisema.
Mratibu wa pambano hilo ambaye ndiye alikuwa kocha wa Tembo Mtoto,
Faraji Ndame anasema kifo cha bondia huyo ni pigo katika klabu yake ya
Kwame iliyopo Mburahati kutokana na kuw,a kinara wa kusshinda mapambano
mengi.
"Ni bondia ambaye alikuwa na namtegemea katika mapambano mengi na
siku ambayo anafariki, kwa kweli sikuamini hadi nilipothibitishiwa na
daktari wa Hospitali ya Mwananyamala, kwani kabla hajaanguka wakati
alipokuwa akifanya mazoezi ya kupiga begi nilikuwa nikimtazama kwa
karibu.
"Hadi anaanguka nilikuwa nikimwona, nilipomfuata kumpa huduma ya
kwanza alikuwa akitokwa povu na kizuia meno akawa ameking'ata, mdomo
ukawa mgumu kufunguka, tulimtoa kizuia meno na kumvua viatu, kisha
tukampeleka Hospitali ya Mwananyala, lakini tukaambiwa amefariki,"
anasema.
Rais wa PST, Emmanuel Mlundwa akizungumza na Jambo Leo, kuhusu kifo
hicho, alisema wamepokea kwa mshtuko, lakini kazi ya Mola haina
makosa, kinachopaswa kila mmoja kumuombea.
Ninachokifahamu kwa Tembo Mtoto ni kwamba, alikuwa bondia bora
mwenye umri mdogo ambaye ndio kwanza alikuwa akiyafuta mafanikio, kwani
mapambano mengi aliyocheza alikuwa akishinda kwa KO.
"Katika pambano lake la mwisho ambalo alipigana na Kea Kea
alishinda kwa KO, nilikuwa mwamuzi wa mchezo huo, kikubwa ambacho naweza
kusema, alikuwa bondia mzuri na atakumbukwa kwa kufanya vema," alisema.
Kocha wa kimataifa wa mchezo huo, Rajabu Mhamila 'Super D', anasema
kifo cha Tembo Mtoto ni pigo kubwa katika tasnia ya ngumi kutokana na
bondia huyo kuonesha kila dalili za mafanikio katika mapambano yake
mengi.
"Kifo cha Tembo Mtoto, hakika kimenishtua kwani ni bondia
niliyekuwa nikimfahamu tangu akiwa katika ridhaa, alikuwa akifuata
ushauri kwangu," alisema.
"Alikuwa akiupenda mchezo husika, aliuheshimu, aliuthamini kama
sehemu ya kazi yake, huku akifanya mazoezi ya kutosha na kuuthamini
mchango wake," anasema Super D.
Dk. Kulwa Killaga ambaye mara nyingi huwapima mabondia kabla ya
mapambano, anasema kifo cha Tembo Mtoto kimemshtua, hasa baada ya
kukubaliana mambo mbalimbali.
"Nilipozungumza naye mara ya mwisho, aliniomba niwe meneja wake,
nikamshauri awe mbali na vitu vilivyo kinyume na maadili ya mchezo wa
ngumi kwa lengo la kuepuka athari zinazoweza kujitokeza," anasema.
Anasema kuwa, mara nyingi alikuwa akilalamika kuhusu waratibu
kuwapiganisha mabondia bila kufuata utaratibu wa muda wa pambano hadi
pambano, madhara yake ni vifo.
"Mfano bondia kapigana wiki moja au mbili, kabla hajafikisha miezi mitatu anapigana tena, hali hiyo ni mbaya sana," anasema.
Anasema kuwa, waratibu wanatakiwa kudhibitiwa katika hilo ili
kulinda maisha ya mabondia ambao wengi wao hawana elimu ya kutosha
katika hilo na ndicho kinachowagharimu wengi. Pia, anawataka waachane na
utumiaji wa bangi.
"Bangi ni kitu kingine kibaya kinachosababisha vifo kwa mabondia,
hivyo wadau wa mchezo huo wanatakiwa kuwashauri mabondia wanaotumia
madawa ya kulevya," anasema.
Bondia Fadhili Awadhi wa klabu ya Jitegemee, aliyewahi kutwangana
na Tembo Mtoto, mwanzoni mwa mwaka huu, alisema kifo cha mwanamasumbwi
huyo kimemhuzunisha.
"Niliwahi kupanda ulingoni na marehemu Tembo Mtoto enzi za uhai
wake, nikamshinda kwa KO katika raundi ya nne, kifo chake kinanipa
majonzi na wakati mwingine nashindwa kuamini," alisema.
Rekodi ya bondia huyo alipigana mapambano saba ya ngumi za kulipwa,
alishinda mara nne na kupigwa mara moja na kutoka sare mara mbili.
Tembo Mtoto alijiunga na ngumi za kulipwa mwaka 2011, akianza
safari yake ya masumbwi kutwangana na Seba Temba wa Morogoro, pambano
lingine lilikuwa Agosti na kufanikiwa kumtwanga Shujaa Keakea kwa TKO.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amin
No comments:
Post a Comment