STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, March 2, 2011

INAFRIKA WAREJEA NA MBELEKO TOKA ULAYA




BAADA ya ziara ya miezi miwili na nusu ya maonyesho ya burudani katika nchi mbalimbali za Ulaya, bendi ya InAfrika imerejea nchini, ikijinadi kuwa, ziara yao ilikuwa ya mafanikio makubwa.
Bendi hiyo iliwasili jana majira ya saa 4 asubuhi, kupitia mmoja wa viongozi
na wanamuziki wake, Bob Rudala imesema itatumia siku chache kupumzika
kabla ya kuanza kuitambulisha albamu yao mpya mikoani.
Akizungumza na Micharazo mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, alisema albamu hiyo ya pili kwao baada ya ile ya 'Indege', inaitwa 'Mbeleko'.
Rudala aliyewahi kutamba na nyimbo binafsi kama 'Nimekuchagua Wewe', alisema albamu hiyo ina nyimbo 10 zilizopigwa katika miondoko mbalimbali ya ngoma asilia za Tanzania.
Rudala alisema utambulisho wa albamu hiyo utaanzia mkoa wa Arusha wiki ijayo, kabla ya uongozi wa bendi hiyo kupanga mahali pengine pa kufanya hivyo.
Kuhusu ziara hiyo, Rudala alisema ilikuwa ya mafanikio makubwa na kwamba watatumia utambulisho wa albamu hiyo kuudhibitishia umma wa Tanzania kuwa walienda kujifunza mambo mengi kuendeleza muziki nchini.
"Tunashukuru tumerejea salama, ila kwa kifupi tumefarijika na mafanikio makubwa tuliyopata katika ziara hiyo na tunapumzika kwa siku kadhaa kabla ya kabla ya kuanza kuitambulisha albamu yetu ya Mbeleko," alisema.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zilizopo kwenye albamu hiyo kuwa ni Mbeleko, Hatushangai, Jamila, Kitchen Party, Mimi Muafrika, Amina, Jua Limetua na kadhalika.
Aliongeza kuwa ziara yao waliyoifanya kuanzia Desemba mwaka jana, ilihusisha nchi tano za Uholanzi, Ujerumani, Uswisi, Austria na Romania ambapo mbali na bendi, pia InAfrika iliambatana na kikundi chao cha wanenguaji na wacheza sarakasi.
InAfrika ilianzishwa mwaka 1992 ikiwa na albamu ya kwanza ya 'Indege' ambayo pia hufahamika kama 'Omunwa'ambayo ilisaidia kuipandisha chati kwa nyimbo zake mchanganyiko zikiwemo zenye miondoko ya asili.

No comments:

Post a Comment