STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, October 20, 2013

Juma Luizio amchimbwa mkwara Tambwe

Juma Luizio (kushoto) alipokuwa katika mazoezi ya Taifa Stars nchini Uganda hiviu karibuni
MSHAMBULIAJI chipukizi anayekuja juu nchini anayeichezea Mtibwa Sugar, Juma Luizio 'Ndanda' amemchimba mkwara mkali wa mabao wa Simba Amissi Tambwe akimwabia asahau kuhusu kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora msimu huu kwani hicho ni mali yake.
Luizio amesema anataka kuwa mfungaji bora msimu huu na kumuapia Tambwe kuwa atakula naye sahani moja.
Akizungumza na MICHARAZO hivi punde, Luizio ambaye jana alifunga mabao mawili wakati Mtibwa Sugar ikizamisha Mgambo JKT kwa mabao 4-1 na kufikisha jumla ya mabao saba moja nyuma ya Tambwe mwenye mabao nane, alisema lengo lake ni kufunga jumla ya mabao 17.
Chipukizi huyo aliyeanza kuitumikia timu ya wakubwa ya Mtibwa Sugar mwaka jana baada ya kupandishwa kutoka kikosi cha vijana, alisema amekuwa akitupia mipira nyavuni kwa lengo la kuwa Mfungaji Bora na kunyakua kiatu cha dhahabu.
Luizio alisema kila Mtibwa inapokuwa dimbani akili zake uziweka katika kutikisa nyavu na ndiyo maana amekuwa akifunga karibu kila mechi na kudai lengo ni kuwa mfungaji bora na siyo kuwasindikiza wenzake.
"Nafunga kwa sababu nataka kuwa mfungaji bora, nimepanga msimu huu nitupie jumla ya mabao 17 ambayo naamini yatanibebesha kiatu hicho, yakizidi haitakuwa neno," alisema.
Kuhusu kinara wa mabao kwa sasa Mrundi Amissi Tambwe wa Simba, Luizio alisema hana hofu naye kwani atamkamata na kumpita kutokana na kasi yake kuongezeka siku hadi siku.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kuzichezea timu za Docks na Polisi Morogoro kabla ya kutua Mtibwa baada ya kung'ara kwenye michuano ya Taifa Cup na kuwa Mfungaji Bora namba mbili wa Uhai Cup mwaka uliopita, alisema ligi ni ngumu lakini atapigana kutimiza lengo.
Luizio alifichua siri ya mafanikio yake ya kufumania nyavu ni kuaminiwa na makocha na kuiga kwake mbinu za Zlatan Ibrahimovic anayemzimia.

No comments:

Post a Comment