STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 13, 2014

Machaku asema hana mkataba JKT Ruvu zinazomtaka zimfuate

MSHAMBULIAJI nyota wa JKT Ruvu, Salum Machaku 'Balotelli' amesema hana mkataba wowote na timu hiyo na hivyo kuiacha milango wazi kwa klabu yoyote inayomhitaji kuzungumza naye.
Machaku aliyewahi kutamba na timu za Simba, Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro, alisema yupo tayari kutua katika klabu yoyote itakayokuwa ikimhitaji mradi waridhiane katika suala la masilahi.
Mshambuliaji huyo aliyemaliza msimu huu akiwa na mabao manne alisema kwa sasa amekaa tayari kupokea maombi kutoka kwa timu yoyote ili kuweza kujiunga nayo au ikiwezekana kubaki JKT.
Alipoulizwa kama timu yake ya zamani ya Polisi Moro iliyorejea Ligi Kuu ikimfuata ili kumrejesha kikosini, alisema angefurahia kwa sababu hakuondoka kwa ugomvi katika timu hiyo iliposhuka daraja.
"Nipo tayari kurudi Polisi Moro, ni timu ninayoiheshimu, pia maisha yangu yanategemea soka sina cha kuchagua wala kubagua ila nimefurahi kuona wamerejea tena ligi kuu," alisema.
Machaku, mmoja wa watoto wa nyota wa zamani wa muziki wa dansi aliyewahi kutamba na bendi za Dar International na DDC Mlimani Park, Salum Machaku, alisema anaamini ligi ya msimu ujao itakuwa ngumu kuliko ya msimu huu ambayo haikutabirika kirahisi.
"Ligi ya msimu huu ilikuwa ni noma, siyo kwa timu za juu wala mkiani. Hapakuwa na iliyokuwa na uhakika wa itakachovuna hadi dakika za mwisho," alisema.

No comments:

Post a Comment