STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, May 13, 2014

Zahoro Pazi hajui lolote Simba

WINGA machachari wa klabu ya Simba, Zahoro Pazi, amesema hana taarifa zozote za kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotakiwa kuachwa ndani ya timu hiyo kwa msimu ujao.
Aidha mchezaji huyo ambaye ni mtoto wa mmoja wa makocha wa timu hiyo, Idd Pazi 'Father' amesema yeye bado ana mkataba na klabu hiyo na kama itakuwa kweli hatakiwi Msimbazi hana neno.
Akizungumza na MICHARAZO, Pazi alisema amekuwa akisoma na kusikia taarifa dhidi yake zikitolewa au kunukuliwa kutoka kwa kocha wake, Zdrakov Logarusic, lakini hajafahamishwa rasmi na viongozi.
"Sina taarifa yoyote rasmi ya kutaka kutemwa Simba, kwa vile nina mkataba na klabu yangu naendelea kujitambua kama mchezaji wa Simba nikiendelea kujipanga kwa msimu ujao," alisema.
Nyota huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Azam na JKT Ruvu alisema hata kama Simba itaamua kuuvunja mkataba wao, hatakuwa na neno zaidi ya kutuliza akili yake ili kujipanga upya kuendeleza kipaji chake.
Pazi aliyesajiliwa na Simba msimu ulioisha hivi karibuni alikuwa akipata wakati mgumu mbele ya Logarusic, japo katika mechi za lala salama za ligi hiyo alikuwa akipewa nafasi na kufunga mabao.
Hivi karibuni iliripotiwa kuwa Pazi na baadhi ya wachezaji zaidi ya 10 wapo kwenye mipango ya kutemwa ndani ya Simba kutokana na pendekezo la kocha Logarusic lililopo katika ripoti yake kwa viongozi.

No comments:

Post a Comment