STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, July 6, 2013

Kaseja kuanika timu atakayoibuka badala ya Simba


Kaseja akiwajibika kwenye mazoezi wa Stars

SIKU chache baada ya kutemwa na Simba, golikipa namba moja wa timu ya taifa 'Taifa Stars' Juma Kaseja amesema atataja hivi karibuni timu yake mpya atakayochezea msimu ujao.
Kaseja ambaye mkataba wake wa kuichezea Simba umemalizika na uongozi kuamua kutomuongeza, alisema muda sahihi utakapofika atataja timu atakayochezea.
"Mengi yanazungumzwa kwa sasa, mimi wakati wangu ukifika nitaongea kila kitu... nitaendelea kucheza mpira," alisema Kaseja bila kuweka wazi ni timu gani atachezea msimu ujao.
Alisema pamoja na kuachwa na Simba bado hajakata tamaa ya mpira kwa kuwa anaamini bado ana kiwango kizuri cha kuchezea timu yoyote.
Kaseja ambaye yupo kwenye kambi ya 'Taifa Stars' inayojiandaa na mchezo dhidi ya Uganda wa michuano ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani, CHAN, alisema anajua anachokifanya.
Awali naodha huyo wa Stars alihusishwa na klabu za Azam na Yanga. Hata hivyo viongozi wa klabu hizo walikanusha uvumi wa kutaka kumsajili mchezaji huyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Yanga, Abdallah bin Kleb, alisema hakuna uwezekano wa kumsajili mchezaji huyo kwa kuwa anapingwa na wajumbe wengi wa klabu hiyo.
Bin Kleb alisema kuwa nafasi ya golikipa imeshachukuliwa na Deogratias Munishi aliyejiunga na timu hiyo akitokea Azam FC.
Kwa upande wake, Katibu mkuu wa Azam FC, Idrisa Nassoro, alisema kuwa timu hiyo kusajili kwa mapendekezo ya kocha Stewart Hall ambaye hajaomba kumsajili golikipa huyo.
Mbali na timu hizo za Azam na Yanga, pia Kaseja anahusishwa kuwindwa na timu ya Coastal Union ya Tanga na Mtibwa Sugar.
NIPASHE 

No comments:

Post a Comment