STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, January 6, 2014

Boti ya Kilimanjaro yaua 6,. miili yatambuliwa


WATU kumi wamefariki dunia katika ajali mbili tofauti  katika Bahari ya Hindi.
Katika ajali ya kwanza, watu sita walifariki baada ya boti ya Kilimanjaro II ilipokumbwa na dhuruba kali katika mkondo wa Nungwi, Zanzibar wakati ikitokea Pemba kwenda kisiwani Unguja jana asubuhi.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Riziki Juma, alisema jana jioni kuwa maiti sita zilipatikana na kwamba abiria watatu waliokolewa wakiwa hai huku uokoaji ukiendelea.
Awali, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yusuph Ilembo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa kazi ya kuwatafuta watu wanaohofiwa kupotea imeanza kufanywa na mabaharia kwa kushirikiana na wananchi.
Alisema boti hiyo ilipofika katika mkondo wa Nungwi ilipigwa na wimbi moja kubwa na injini kuzimika na watu waliokuwa wamekaa juu wakiwamo watoto waliteleza na kuhofiwa kutumbukia ndani ya bahari.
Alisema kuwa boti hiyo baada ya injini zake kuzimika ilibakia ikielea baharini na kwamba Nahodha wake alifanikiwa kuziwasha tena na kuendelea na safari na abiria waliobakia walifika salama.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Omar Maalim, alisema wazamiaji waliondoka jana mchana kuungana na baadhi ya wananchi huko Nungwi kufanya kazi ya kutafuta watu wanaohofia kupotea baada ya ajali hiyo.
Hata hivyo, alisema ZMA itatoa taarifa baada ya kukamilika uhakiki wa majina ya abiria kwa meli zote zilizosafiri jana kutoka kisiwani Pemba pamoja na wazamiaji kufika katika eneo la tukio na kufanya kazi ya kutafuta watu hao.
Hata hivyo, wakati mkuu huyo wa wilaya akisema hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Khalfan Mohamed Mshangi, alisema baadaye kuwa zimepatikana maiti tano na tatu zimetambuliwa.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Akram Khamis issa (11), mkazi wa Mwanakwerekwe; Masoud Hamad Abdallah (30), mkazi wa Wete na Nashra Khamis (9), mkazi wa Mombasa, Zanzibar.
Aliongeza kuwa boti hiyo ilikuwa na abiria 396 wakiwamo watoto 60 na kwamba abiria ambao hawajapatikana ni 18.
Baadhi ya mashuhuda waliohojiwa  walisema mkasa huo ulitokea sasa 2:30 asubuhi wakati boti hiyo ilipofika eneo la Nungwi na kupigwa wimbi kali na kuelemea upande mmoja.
Suleiman Muhammed Said, abiria katika boti hiyo, alisema baada ya boti hiyo kuelemea upande mmoja, baadhi ya watu walidondoka baharini pamoja na mizigo na kwamba boti iliendelea na safari baada ya kukaa sawa.
Alisema boti hiyo iliondoka Pemba majira ya saa 2:00 asubuhi na kwa mujibu wa  ratiba, boti ilitarajiwa kufika Unguja saa 4:00 asubuhi, lakini kutokana na hitilafu hiyo, ilifika saa 6:00 mchana.
Alisema boti ilipoondoka Pemba, hali ya bahari haikuwa nzuri na ilipofika Nungwi hali ya bahari ilizidi kuchafuka na boti kuyumba.
Alisema hadi boti inafika bandarini, ndugu zake wawili hawakuonekana pamoja na mizigo waliyokuwa  nayo katika boti hiyo.
“Nilikuwa na ndugu zangu wawili na mizigo, baada ya meli kutaka kuzama mizigo na baadhi ya watu walidondokea baharini, lakini meli ilipoibuka iliendelea na safari bila ya kuwatafuta,” alisema Suleiman huku akitokwa machozi.
Baadhi ya watu walifika bandarini Malindi waliangua vilio na sura zao kujaa na huzuni kutokana na kutowaona ndugu na jamaa zao.
Abdallah Mohammed Abdallah, aliyefika bandarini kumtafuta mtoto wake ambaye bado hakuwa na taarifa zake, alisema alipokea simu ya mtoto wake aliyekuwamo katika boti saa 2:30 asubuhi kuwa boti inazama.
“Nilipokea simu ya mtoto wangu, alikuwa akilia na kuniambia baba baba tunakufa, meli huku inazama, baada ya hapo simu yake ikawa haipatikani” alisema Abdallah.
Aidha alisema alifika bandarini kupata taarifa sahihi, lakini hakupewa jibu linaloridhisha kutokana na boti kufika bila kumuona mtoto wake.

No comments:

Post a Comment