STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, December 5, 2013

Tanzanite ikiitoa Afrika Kusini kuwavaa Nigeria au Tunisia


WAKATI kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Afrika Kusini U20 kikitua leo kwa ajili ya pambano la awali dhidi ya wenyeji wa Tanzanite, timu hiyo ya Tanzania kama itafanikiwa kuiondosha wapinzani wao itakuwa na kibarua kingine kigumu dhidi ya mshindi kati ya Nigeria au Tunisia kukata tiketi ya Fainali za Dunia za 2014.
Fainali hizo za Kombe la Dunia kwa timu za U20 wanawake zitafanyika nchini Canada, na mechi za kupata wawakilishi wawili wa Afrika zinatarajiwa kufanyika kati ya Januari 10-24 mwakani.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo timu nyiungine zilizopo katika hatua ya 8 Bora mpaka sasa ukiziondoa Tanzania na Afrika Kusini ni Nigeria, Tunisia, Ghana, Uganda, Zambia na Equatorial Guinea.
Tanzania imefika hatua hiyo baada ya kuiondosha patupu Msumbiji katika mechi za raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 15-1 baada ya awali kuitandika mabao 10-0 jijini Dar es Salaam kabla ya kuisulubu nyumbani kwao kwa mabao 5-1.
Jumamosi itashuka dimbani kuikaribisha Afrika Kusini iliyoing'oa Botswana kwa mabao 7-2, mechi hiyo itachezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kiingilio cha chini siku hiyo ni Sh. Elfu Moja (1,000) tu.
Tanzanite itaifuata Afrika Kusini wiki mbili baadaye na iwapo itafanikiwa kushinda mechi hizo na kuitoa Afrika Kusini, itasubiri kujua hatma yake dhidi ya mshindi kati ya Nigeria na Tunisia ambazo wikiendi ijayo nazo zitapepetana nchini Nigeria.
Kikosi hicho cha U20 kinanolewa na kocha Rogasian Kaijage kwa sasa kinaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Karume na ule wa Taifa kujiandaa kwa mechi hiyo na kambi yake ipo  Msimbazi Hotel baada ya kutoka Ruvu mkoani Pwani.
Watanzania wamekuwa na imani kubwa na Tanzanite kutokana na kuonekena kuelekea kuziba nafasi ya Twiga Stars na bila shaka Jumamosi itaendelea kuwapa RAHA watanzania katika pambano hilo dhidi ya Afrika Kusini ambalo litachezeshwa na refa Nabikko Ssemambo kutoka Uganda.
Waamuzi wasaidizi katika mchezo huo ni  Gebreyohanis Trhas kutoka Ethiopia ,Nakitto Nkumbi na Irene Namubiru wote kutoka Uganda na kamishna atakuwa John Muinjo kutoka Namibia.
Muinjo pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Namibia (NFA) na mjumbe wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)..

No comments:

Post a Comment