STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, August 2, 2012

Simba wamalizana na Azam kuhusu Ngassa, mwenyewe adai haendi kokote kwa vile hajashirikishwa

MABINGWA wa soka wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba wametangaza kumsajili mshambuliaji nyota wa Azam na timu ya Taifa (Taifa Stars), Mrisho Ngassa kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja. Hata hivyo Ngassa mwenyewe amesisitiza kuwa hajashirikishwa katika 'dili' hilo na kudai kama uongozi wa Azam haumtaki katika klabu yao imvunjie mkataba na kumlipa chake kuliko kumpeleka kwenye klabu ambayo hajawahi kuitoa kuichezea. Uongozi wa Simba na Azam jana ulinukuliwa kwamba umefanikisha mpango wa Ngassa kutua Msimbazi baada ya kuwazidi kete Yanga waliokuwa tayari kulipa Sh Milioni 20, milioni tano pungufu na zile walizotoa Simba. Awali, uongozi wa Azam ulishatangaza kuwa uko tayari kumuuza winga huyo kwa klabu yoyote itakayotoa dau la dola 50,000 (sawa na zaidi ya Sh. milioni 80), jambo ambalo limeonekana kuwa gumu kabla ya Simba kumpata mchezaji huyo kwa ofa ya mkopo ya Sh. milioni 25. Ngassa ambaye alitakiwa sana na kocha wa Simba, Milovan Circkovic, anatarajiwa kuichangamsha safu ya ushambuliaji ya timu yake mpya katika ligi kuu ya Bara na pia katika michuano itakayoanza mapema mwakani ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika. Akizungumza jana jijini Dar, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kuwa wamemsajili Ngassa kwa mkopo na tayari wamefikia makubaliano na Azam, hivyo mchezaji huyo ataichezea timu yao katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo inatarajiwa kuanza Septemba Mosi. Kaburu alisema kuwa wamemsajili mshambuliaji huyo kutokana na maelezo ambayo walipewa na Cirkovic ili kuziba nafasi ya Emmanuel Okwi ambaye sasa anaelekeza nguvu zake katika kusaka timu atakayoichezea soka la kulipwa barani Ulaya. "Usajili wa Ngassa umeshakamilika, ni mali yetu kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kukamilisha usajili wake wa kuichezea Simba kwa mkopo," alisema Kaburu. Naye Meneja wa Azam, Patrick Kahemele, alinukuliwa akisema wameamua kumpeleka Ngassa Simba kutokana na maelezo ya Cirkovic kumuhitaji ambapo wanaamini ataendeleza kipaji chake na kuendelea kuisaidia Taifa Stars. Kahemele alisema kuwa Azam ilifikia maamuzi ya kumuuza mshambuliaji huyo baada ya kuonyesha hadharani mapenzi aliyonayo na mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga, lakini alidai Yanga imekwama kumpata kwa vile iligoma kuongeza dau katika fedha ilizotaka kutoa. Azam ilitangaza kwamba iko tayari kumuuza Ngassa kwa gharama ya Dola za Marekani 50,000 baada ya nyoya huyo kuonyesha mapenzi yake kwa Yanga kwa kuvaa na kuibusu nembo ya klabu hiyo wakati akishangilia goli aliloifungia Azam katika mechi yao ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ngassa aliyeihama Yanga mwaka juzi aliisaidia Azam kumaliza kwenye nafasi ya pili katika msimu wa ligi uliopita ambapo mwakani itashiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya Kombe la Shirikisho yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF). Akizungumza na MICHARAZO, Ngassa alisema hana taarifa za kupelekwa Simba na kudai kwa tararibu anazopfahamu alipaswa kushirikishwa katika mazungumzo ya klabu hizo mbili kabla ya kufikiwa maamuzi. "Kama ni kweli wamefanya hivyo hawajanitendea haki, nilipaswa kushirikishwa na kama klabu ya Azma hainitaki basi inilipe changu nijue wapi pa kwenda na sio kunipeleka sehemu kama mzigo usio na maamuzi," alisema Ngassa mtoto wa kiungo wa zamani wa Pamba na Simba, Khalfan Ngassa. Ngassa alisema yeye anauheshimu mkataba wake na Azam ambao umesaliwa muda wa mwaka mmoja, lakini ni vigumu kwake kukubali kirahisi kupelekwa Simba, ingawa hakuweka bayana atachukua hatua gani katika sakata hilo ambalo kwa kiasi fulani linataka kufanana na lile la wachezaji Mohammed Banka aliyekuwa Simba na Ramadhani Chombo wa 'Redondo' wa Azam ambao walitolewa kwa mkopo na klabu zao kwa klabu za Villa Squad na Moro United lakini wakagoma kwa vile hawakushirikishwa katika uhamisho huo.

No comments:

Post a Comment